73210182Soka ni mchezo unaochezwa hadharani na kupindisha jambo lolote ni kutafuta kujidhalilisha kwa makusudi, hasa katika ulimwengu wa sasa ambao teknolojia imeshika hatamu.

Soka linachezwa uwanjani na wachezaji 22, lakini wanaotazama ni maelfu ya watu, na mamia ya kamera yanachukua picha tofauti za mchezo, sasa unapojaribu kupingana na kile kilichoonwa uwanjani ni kuleta vituko visivyo na ulazima. 

Soka ni mchezo unaojipambanua kama mchezo wa kiungwana na hivyo tendo lolote lisilo la kiungwana hujitenga na mchezo huo, kwa kifupi hakuna namna mchezaji, kocha au uongozi wa timu unaoweza kutenda au kutetea vitendo visivyo vya kiungwana na ikakubalika.

Katika mchezo wa kuwania Kombe la Ligi (Capital One Cup), Jose Mourinho alisikika akitetea utukutu wa mchezaji wake, Diego der Silva Costa, pale Darajani kwa kusema “Mwache Costa acheze mpira wake.”

Mourinho alitamka hayo ikiwa ni katika kutetea kitendo cha Costa kumkanyaga kwa makusudi mchezaji Emre Can wa Liverpool, katika mechi ambayo Chelsea iliibuka na ushindi.

Pamoja na jeuri ya Mourinho kujifanya hakuona kilichotokea, Chama cha Soka cha England (FA) kikapitia mchezo huo kupitia runinga zao na wakamtia hatiani Costa kwa kosa la kumkanyaga Can kwa makusudi.

Pamoja uamuzi ule uliozingatia ushahidi wa video ya mechi husika, bado Mourinho alidai mchezaji wake ameonewa. Kwa haraka tu unaweza kujiuliza ni kitu gani kilichomfanya Mourinho atetee upuuzi katika mchezo wa kiungwana?

Unaweza kufikiria majibu mawili tu kwa haraka; kocha ndiye anayemtuma kutenda hayo au yawezekana kocha mwenyewe si muungwana kwa hulka yake, hivyo haoni haja ya uungwana katika soka ila ushindi bila kujali ushindi umepatikanaje.

Wanasema mtoto umleavyo ndivyo akuavyo, Septemba 19, 2015 Chelsea katika mechi ya ushindi wa bao 2-0 dhidi ya Arsenal, Costa anaonekana waziwazi akimfanyia hila Gabriel Paulista wa Arsenal baada ya kuzozana kutokana na  kitendo chake cha kumchapa kofi Laurent Koscielny.

Paulista alikwenda nje kwa kadi nyekundu, na katika maana ya uungwana wa soka halikuwa jambo la kushabikia maana ilikuwa ni matokeo ya hila za Costa katika mchezo unaoitwa mchezo wa ‘kiungwana’. 

Baada ya mechi FA kikapokea rufani ya Arsenal dhidi ya kadi hiyo nyekundu na hatimaye wakaitengua na kumfungia Costa kucheza mechi tatu. Hapa nilitarajia walau Mourinho aoneshe uungwana wake kidogo ukiacha ule ulalamishi wake kwa kila jambo ikiwamo lawama za kufungwa kuzipeleka kwa daktari wa timu na waokota mipira, lakini haijawa hivyo. 

Mourinho amepayuka na kusema kuwa Costa ameonewa kwa kitendo cha kufungiwa mechi tatu. Hapa hata kama kitendo cha kutengua kadi nyekundu ya Paulista hakikuwa sawa bado alipaswa kukemea tabia ya Costa kama ambavyo Sir Alex Ferguson alivyopata kukemea tabia ya Cristiano Ronaldo kujiangusha nyakati hizo.

Kocha wa timu ni kama mzazi na anapaswa kulinda heshima yake na heshima wa mchezo wa soka kama mmoja wa wadau wa soka. 

Tazama, beki wa Chelsea, Zouma alifunguka na kusema hakushangazwa na kitendo cha Costa maana ni mtu muongo daima. Zouma alisutwa na uungwana ingawa baadaye aliamua kuomba msamaha kufuatia matamshi yake walau asionekane ametofautiana na bosi wake lakini ukweli amekwishasema.

Hapa unajiuliza, kama hata wachezaji wenzake wanamjua na kocha anatetea tabia hizo, basi tunapaswa kuamini kuwa kocha ndiye anayemtuma mchezaji wake huyo kuwaondoa wapinzani mchezoni kwa namna isiyo ya kiungwana. 

Lazima ujiulize hekima na busara ya Mourinho ilikopotelea, unaweza kufikiria kwanini alimuuza Mata (labda kwa kuwa Mata ni mpole na anahusudu soka la uungwana?).

Waswahili wanasema ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni, na kweli tumestaajabu ya Mourinho tunayaona ya Mbeya City. Baada ya Juma Saidi Nyoso, nahodha wa Mbeya City, kumtendea kitendo kisicho cha kiungwana cha kumshika makalio John Bocco (kepteni wa Azam), timu hiyo inamtetea ikisema beki huyo hakupewa nafasi ya kusikilizwa.

Utetezi huu unatokana na nini? Nyoso ameonewa? Wao wana maslahi na kitendo hicho? Inashangaza sana katika mtandao wa Instagram kuona video iliyowekwa na Mbeya City (kama kweli Mbeya City ndiyo wenye hiyo akaunti), kwa lengo la kuonesha Bocco akianza kumchezea rafu kwa kumkanyaga Juma Nyoso na ndipo akalipa kisasi kwa kitendo hicho cha kihuni (narudia kama kweli akaunti ile ni ya Mbeya City) basi mpira umetushinda.

Ni bora Mussa Mapunda, Mwenyekiti wa Mbeya City, akajua kuwa kuna wakati ili kumsaidia mtu ni vizuri kumwambia ukweli kwamba amekosea na juhudi nyingine za kumsaidia zifanyike. 

Huwezi kumsaidia mtu kama hujamwambia ukweli wa wapi amekosea na katika hili hawamsaidii mchezaji bali wanamuangamiza na kuwanyima chipukizi haki ya kujua nani wajifunze kwake na nani wasijifunze kwake.

Matatizo ya Nyoso yana historia kwani kwa mara ya kwanza akiwa Ashanti United mwaka 2007 alimfanyia hivyo mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Joseph Kaniki, aliyejibu kwa kumpiga ngumi hali iliyomponza kufungiwa na TFF.

Akarudia tena mwaka 2010 alipomfanyia beki wa zamani wa Yanga, Amir Maftah, aliyejibu kwa kumpiga kichwa akatolewa kwa nyekundu, na msimu uliopita akiwa Mbeya City, alipomtomasa aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, Elius Maguri. Kutokana na ushahidi wa picha za magazeti, Nyoso alifungiwa mechi sita na TFF.

Huku wengi wakidhani kwamba adhabu hiyo itakuwa fundisho kwake na hataweza kurudia, lakini Nyoso ameonesha yeye ni ‘nunda’ kwa kurudia baada ya kumdhalilisha Bocco.

Mara zote hizi sina hakika kama uongozi wa timu yake umemwita na kumuonya au kumtafutia hata msaikolojia wala kujua wapi mzizi wa tatizo ili limalizwe na mchezaji aendelee na maisha yake.

TFF imechunguza tukio na hatimaye wamemfungia Nyoso kucheza soka miaka miwili lakini kwa matukio ya mwanzo hasa lile la Maguri, ambako mchezaji alikiri na kuomba msamaha, ulikuwa ni wakati sahihi wa kumsaidia mchezaji huyu. 

Kilichotokea baada ya adhabu ile ya kufungiwa mechi kadhaa ni kama alipokewa kishujaa na kulishambulia gazeti (si hili) lililoripoti habari ile, jambo ambalo halikuwa la kiungwana hata kidogo. 

Huyo ni kepten wa timu anafanya hayo na hakemewi, sasa anawezaje kusimamia nidhamu ya walio chini yake? Usajili wa wachezaji wakati mwingine uwe kama kuajiri wafanyakazi huko maofisini. 

Timu zinaposajili wachezaji lazima zizingatie kupata wachezaji wanaoweza kuwa viongozi na wahamasishaji na siyo bora anajua kupiga mpira.

Wiki mbili zilizopita nilieleza hapa kuwa hakukuwa na haja kwa Simba kumwita Juma Kaseja ‘mzee’ wakati hawakuwa na kijana wa kuiongoza Simba kupata mafanikio aliyoyafikia yeye.

Hakuna haja ya kumshambulia Nadir Haroub ‘Cannavaro’ eti kazeeka wakati ana majukumu makubwa ya kuwalea katika nidhamu iliyotukuka vijana kama Juma Abdul, Haji Mngwali, Simon Msuva na wengine. 

Lengo la makala hii wala si kumsimanga Nyoso maana kama binadamu anahitaji faraja katika kipindi kigumu cha kutengwa na jamii ya soka, ila lengo hapa ni kupinga hizi alitenda na hakutenda maana zinafuga mjadala usio na tija ambao unazidi kumwathiri.

Kupitia hili muundo wetu wa soka lazima uzingatie kuwa na walezi katika timu au wasaikolojia watakaosaidia kuwarudisha mstarini wachezaji wanapokuwa wanahama kwenye mstari. 

Sote tunaelewa wachezaji wetu wengi hawajapita Academy ila huko uswahilini na kwa mantiki hiyo suala la maadili lazima libebwe na timu yenyewe, lakini kwa haya ya Mourinho na ukimya wa Mbeya City nimeshangazwa.

 

Baruapepe: [email protected] 

Simu: 0715 36 60 10

By Jamhuri