FrontKwa muda mrefu sasa, zimekuwapo taarifa kwamba familia hiyo ya Rais mstaafu imekuwa ikizibeba kampuni hizo, na moja inayotajwa ni ile ya Home Shopping Centre, iliyojitangaza mufilisi. Home Shopping Centre ilijitangaza kufilisika siku chache kabla ya Rais John Magufuli kuapishwa.

Ridhiwani Kikwete anatajwa kuwa na uhusiano wa karibu mno na kampuni hiyo, ingawa mara kadhaa amekuwa akikanusha. Ridhiwani amewewahi kuhojiwa na JAMHURI na kusema kwamba tuhuma zote zinazoelekezwa kwake ni fitna za kibiashara. 

Rais John Magufuli, akizungumza na wafanyabiashara Ikulu wiki iliyopita, aligusia kampuni inayotumiwa na wafanyabiashara kukwepa kodi. Ingawa hakuitaja kwa jina, wafuatiliaji wa mambo wanasema mlengwa ni Home Shopping Centre na kampuni zake tangu,

Rais Magufuli alisema: “Nafahamu, katika mchezo huo wa kukwepa kodi, baadhi ya wafanyabiashara wadogo hutakiwa kukusanya fedha na kumpatia mtu mmoja fulani ili huyo ndiye akawakombolee mizigo yao bandarini.

“Mchezo wa aina hii kwa mfanyabiashara wa kweli anaweza akaufanya kwa muda tu, lakini hauwezi kuwa wa kudumu kama kweli anaipenda na kuithamini biashara yake. Wanadhani Serikali haifahamu, kumbe tunaujua mchezo wote huu!

“Ndiyo maana natumia muda mwingi kuwaomba tushirikiane. Wale ambao kwa bahati mbaya walikwepa kodi, wakakimbia na makontena yao, natoa muda wa siku saba wawe wamelipa kodi yetu ya Serikali. Wakilipa kodi yetu, hakuna atakayewashitaki kwa sababu tunachohitaji sisi ni fedha zetu, vinginevyo watajipa shida ya bure tu kwa sababu kontena si sindano ya kuficha isionekane.”

Mbali na Ridhiwani, ndugu mwingine wa Rais Kikwete, anayetajwa kuhusika kwenye utoaji makontena bila kuyalipia ushuru, ni aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Madeni Kipande.

Wakati Kipande akiwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA alipitisha waraka uliozaa matatizo yote yanayoshuhudiwa sasa bandarini. Awali Bandari ya Dar es Salaam ilikuwa ikisimamia upakuaji na upakiaji wa makontena, lakini Kipande akahamishia majukumu hayo makao makuu.

Kipande, aliyekuwa na urafiki mkubwa na Waziri wa Uchukuzi wa wakati huo, Dk. Harrison Mwakyembe, Februari 5, 2013 aliiandikia Bandari ya Dar es Salaam kuieleza rasmi kuwa ameunda Kamati Maalum kuwa jukumu la makontena limechukuliwa na makao makuu.

Katiba barua hiyo yenye Kumb. Na DG/3/3/06 (nakala tunayo) Kipande alimtaka Mkurugenzi wa Utumishi, P. D. Gawile kusimamia kitengo cha makontena hasa TICTS, ICDs na CFS.

Katika barua hiyo, Kipande alidai anaipunguzia Bandari ya Dar es Salaam mzigo, anaiepusha na mgongano wa maslahi na uamuzi wake huo ulilenga kuongeza ufuatiliaji, utendaji na mapato. (soma kielelezo)

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa chini ya kipande, makontena 4,200 na magari 919 vilipitishwa katika Bandari ya Dar es Salaam kati ya mwaka jana mwanzoni hadi mapema mwaka huu bila kulipiwa ushuru. JAMHURI ina nyaraka za ripoti ya uchunguzi zinazothibitisha madai hayo.

Kipande aliondolewa kwenye wadhifa huo na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, kutokana na tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka. Siku chache kabla ya Rais Kikwete kung’atuka, alimteua Kipande kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi.

Mwaka jana, Home Shopping Centre ilikuwa miongoni kwa kampuni zilizokuwa kwenye orodha ya ukwepaji kodi kupitia makontena 500. Ingawa hakuna ushahidi wa kinasaba kati ya Home Shopping Centre na familia ya Kikwete, kumekuwapo na matukio kadhaa yanayothibitisha madai hayo.

Miongoni mwa matukio hayo ni kitendo cha wamiliki wa iliyokuwa Home Shopping Centre kuwa karibu zaidi na Rais Kikwete, na hata kupiga picha mbalimbali na katika maeneo tofauti.

Wamiliki wa kampuni hiyo waliweza kuwa mstari wa mbele kutoa misaada yenye thamani ya mamilioni ya shilingi. Miongoni mwa misaada hiyo ni ule waliopewa wakazi wa Mabwepande. Katika msaada huo, Home Shopping Centre ilitoa taa 655, ikaahidi kujenga kituo cha Polisi na ikajenga shule ya msingi kwa watoto wa familia hizo zilizohamishiwa huko kutoka Jangwani, Dar es Salaam. Familia hizo za Jangwani zilihamishiwa Mabwepande kuepushwa na mafuriko yaliyolikumba eneo hilo.

Rais Kikwete amekuwa karibu na familia ya wafanyabiashara hao, na hilo linathibitishwa na uharaka wake wa kwenda kumjulia hali mmoja wa wamiliki wa Home Shopping Centre, Said Mohamed Saad, alipomwagiwa kemikali inayoaminiwa kuwa ni tindikali.

Saad alifikwa na matatizo hayo akiwa anazungumza na mfanyakazi wa duka lake lililopo kwenye Jengo la Msasani City Mall, Dar es Salaam. Wamiliki wa kampuni hiyo walifanya kila wanaloweza kuwa karibu na viongozi wakuu wa kitaifa wa Serikali ya Awamu ya Nne. Baadhi ya picha zinamwonesha Salaah akiwa na Rais Kikwete.

Kadhalika, amepiga picha akiwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu; Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Ambokile Mwakinyule, Waziri wa Uchukuzi wa wakati huo, Dk. Harrison Mwakyembe; Waziri wa Uchukuzi wa mwisho katika Awamu ya Nne, Samuel Sitta; aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uwezeshaji), Dk. Mary Nagu; aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe; Balozi wa Tanzania nchini China, Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo; Balozi wa Tanzania nchini Kenya, John Haule; na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Dar es Salaam.

“Kwanini wawe karibu na Mkuu wa Jeshi la Polisi? Kwanini wawe karibu na Waziri wa Mambo ya Ndani? Kwanini wawe karibu na mawaziri waliokuwa na dhamana na uchukuzi ambao bandari zilikuwa chini yao? Kwanini wawe karibu na Waziri wa Viwanda na Biashara? Huhitaji shahada kutambua nini kilichokuwa kikiendelea hapo.

“Hawa wakubwa inawezekana walijikuta wakipiga picha tu bila kujua maudhui yake, lakini kwa vyovyote huo ulikuwa mpango wa kuwafanya wazoeane ili mambo yao yaweze kunyooka pale walipohitaji msaada,” kimesema chanzo chetu.

Mara kadhaa imeelezwa kuwa makontena ya Home Shopping Centre hayaguswi na wakaguzi bandarini.

Wafanyabiashara wengi wa Kariakoo na mikoani walikuwa wakitumia kampuni za wafanyabiashara hao kusafirisha shehena zao kutoka ughaibuni, hasa China na Dubai.

Vituko vya wamiliki wa kampuni hiyo kwa nyakati tofauti viliripotiwa katika mamlaka za juu za Serikali, lakini mara zote hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa.

Katika kikao ambacho aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, alikutana na wakurugenzi wa kampuni na mawakala wa forodha, miongoni mwa mambo yaliyotawala ni ya wamiliki wa Home Shopping Centre na wamiliki kadhaa wa bandari kavu (ICD). Waliozungumza hawakusita kutamka wazi kuwa wamiliki hao walikuwa wakilindwa na wakubwa serikalini. Mawakala wa Forodha waliituhumu kampuni hiyo kwa ukwepaji kodi.

Walidai kwamba kampuni hiyo imekuwa na utaratibu wa kuingia makubaliano na baadhi ya wafanyabiashara wakubwa na wadogo hasa wa Kariakoo na mikoani.

“Unachofanya ni kununua mzigo wako China, unaenda kwenye kampuni yao au kampuni dada ambazo nyingine zina leseni za kutolea mizigo bandarini.

“Wateja wanaokubali kutumia mpango huu haramu hulipa kwao Sh milioni 17 kwa kontena moja la futi 40 na Sh milioni 12 kwa kontena moja la futi 20.

“Kampuni zinazolindwa na wakubwa zinalipia TRA Sh milioni nane kwa kontena la futi 40 na milioni nne kwa kontena la futi 20 pamoja na gharama za bandarini ambazo si zaidi ya Sh milioni 1.2.

“Inasikitisha Serikali kila siku inahangaika kutafuta vyanzo vipya vya kuongeza mapato wakati hiki kilichoko tena chenye uhakika kikihujumiwa na wachache kwa kushirikiana na wenye mamlaka,” anasema mmoja wa wanufaika wa mpango huo.

Kwa upande wake, mwaka jana TRA walisema kauli kwamba makontena yaliyokamatwa yakiwa na matatizo ni ya Home Shopping Centre, si za kweli.

Aliyekuwa Kamishna wa Forodha, Kabisa Masamaki, ambaye amefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwa sakata ya kuisababishia Serikali hasara, aliliambia JAMHURI kuwa ni upuuzi baadhi ya wafanyabiashara kupotosha ukweli, wakati makontena yaliyokaguliwa ni zaidi ya 2,000 na ni ya wafanyabiashara mbalimbali nchini, kisha kudai kwamba ni ya kampuni moja ya Home Shopping Centre.

Mkurugenzi wa Huduma za Mlipakodi na Elimu wa TRA, Richard Kayombo, akasema kati ya makontena 500 ya wafanyabiashara mbalimbali yaliyokaguliwa kwa wakati huo, 188 yalibainika kuwa na udanganyifu unaolenga kukwepa kodi.

“Tumebaini kuwa nyaraka za takwimu za bidhaa nyingi zinaonesha idadi ndogo kuliko idadi halisi ya bidhaa husika,” alisema Kayombo.

Aliongeza: “Kwa muda mrefu tumekuwa na kawaida ya kukagua mizigo kwa asilimia 30 ili kujiridhisha, lakini kwa sasa tumeanza kukagua kwa asilimia 100 kwa kila mizigo unaoingia bandarini.

“Isipokuwa [hatukagui] malighafi ya kuzalisha bidhaa viwandani, mizigo inayokwenda kwenye miradi iliyofadhiliwa na wahisani, mizigo ya mabalozi na inayokwenda maeneo maalum ya kibiashara.”

Ukaguzi huo ulifanyika baada ya maofisa wa TRA kubaini viashiria vya udanganyifu wa takwimu za baadhi ya bidhaa zikiwamo nguo, vipuri vya magari, vifaa vya ujenzi, televisheni, majokofu na vyandarua.

“Kitu cha msingi ni kwamba tumegundua udanganyifu na tumechukua hatua,” amesema Kayombo bila kutaka kutaja kampuni yoyote kwa jina.

Msemaji wa iliyokuwa Kampuni ya Home Shopping Centre, Joseph Rugakingira, anasema mgogoro uliopo ni fitina za wafanyabiashara wanaoona kampuni ya Home Shopping Centre inachukua nafasi yao kibiashara.

“Ni majungu tu hakuna jambo lolote la ukweli. Kati ya makontena yaliyokaguliwa, ya kwetu wamekagua makontena 463, kati ya hayo ni makontena tisa tu, ndiyo yamekutwa na wrong packing (bidhaa tofauti).

“Yupo mfanyabiashara mmoja simtaji, yeye ya kwake wamekagua makontena 250 tu, wakakuta 231 yana matatizo. Mimi ni tisa tu, na hii imetokana na kuchanganya documents (nyaraka) kutokana na wingi wa mizigo tunayoingiza nchini, lakini hili ndilo wamelishikia bango ajabu.

“Na mimi najua tatizo limelala wapi. Hawa wanafanya fitina. Wapo wafanyabiashara wakubwa ambao wamekuwa wakileta mzigo na kuuza kwa bei za juu ajabu au wanasafirisha mizigo kwa bei kubwa na kuwaumiza wafanyabiashara wadogo hapa nchini.

“Sasa hivi mfanyabiashara mwenye shilingi milioni 10 na kuendelea anakwenda China, ananunua mzigo analeta kwetu tunamsafirishia kwa bei rahisi, anakuja hapa nchini anauza na kupata faida.

“Kinachotokea ni kwamba wale waliokuwa wanawanyonya wafanyabiashara wadogo hapa Kariakoo wameanza kukimbiwa na wafanyabiashara. Wafanyabiashara wadogo wanaona bora waje kwetu tuwasafirishie na kuwatolea mzigo kwa bei nafuu, wapate faida.

“Sasa hawa wanaokimbiwa na wafanyabiashara wadogo waliokuwa wakiwanyonya, wanaokuja kwetu tuwasaidie kukua, inawakera [wafanyabiashara wakubwa] wanaamua kutupiga fitina.

“Hili la Ridhiwani tumelisikia, lakini tunasema si kweli. Tumekuwa na biashara miaka mingi tu, Ridhiwani kuwa na urafiki au mawasiliano naye ya hapa na pale, si kwamba amekuwa mbia katika kampuni zetu.

“Tunasema mwenye wasiwasi na kampuni zetu, basi na aje hata leo akague documents au bidhaa zetu. Tuko huru na wazi. Hatuna wasiwasi. Hebu tusaidiane kukua hapa nchini,” alisema Rugakingira.

Rugakingira pia aliiomba TRA kujenga utamaduni wa kusafiri hadi katika nchi kama China na kwingineko kuona bei halisi za bidhaa badala ya kuweka kodi kubwa zenye kukatisha tamaa walipakodi.

Alisema bidhaa zinauzwa kwa bei ndogo China ila zinaongezeka bei kutokana na ukubwa wa kodi hapa nchini, na kwamba hilo linawafanya wafanyabiashara wasio waaminifu kufikiria kukwepa kodi.

 

Kampuni zilizokwepa kodi

Kampuni 43 zimeshabainika kukwepa kodi katika makontena 349 kupitia Bandari Kavu (ICD) ya Said Salum Bakhresa.

Kampuni hizo na idadi ya makontena kwenye mabano ni:

1: Lotai Steel Tanzania (100)

2: Tuff Tyres Centre Company (58)

3: Binslum Tyres Company Ltd (33)

4: Tifo Global Mart (Tanzania) Company Limited (30)

5: IPS Roofing Company Limited (20)

6: Rushywheel Tyre Centre Co. Ltd (12)

7: Kiungani Trading Company Limited (10)

8: Homing International Limited (9)

9: Red East Building Materials Company Ltd (7)

10: Tybat Trading Co. Ltd (5)

11: Zing Ent Ltd (4)

12: Juma Kassem Abdul (3)

13: Salum Link Tyres (3)

14: Ally Masoud Dama (2)

15: Cla Tokyo Limited (2)

16: Farid Abdullah Salem (2)

17: Salum Continental Co. (2)

18: Zuleha Abbas Ali (2)

19: Issa Ali Salim (2)

20: Snow Leopard Building (2)

 

Wenye kontena moja moja wamebainika kuwa ni:

21: Abdulaziz Mohamed Ally

22: Ahmed Saleh Tawred

23: Ali Amer

24: Ally Awes Alhamdany

25: Awadhi Salim Saleh

26: Fared Abdallah Said

27: Hani Said

28: Hassan Hussein Suleyman

29: Humud Suleiman Humud

30: Kamil Hussein Ali

31: Libas Fashion

32: Nassir Salehe Mazrui

33: Ngiloi Ulomi Enterprises Co. Ltd

34: Omar Hussein Badawy

35: Said Ahmad Hamdan

36: Said Ahmed Said

37: Salumu Peculier Tyres

38: Sapato N. Kyando

39: Simbo Yonah Kimaro

40: Straus International Co. Ltd

41: Swaleh Mohamed Swaleh. 

4995 Total Views 1 Views Today
||||| 7 I Like It! |||||
Sambaza!