Ernest-ManguJeshi la Polisi, kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, linapaswa kujipanga kikamlilifu kukabiliana na matukio ya mauaji yanayolikumba Taifa katika kipindi kifupi sasa.

Leo nimekumbuka uzalendo wa nchi yetu miaka kadhaa iliyopita. Nimekumbuka uzalendo kwa maana ya kila mtu kuwa mlinzi wa mali na amani wa Taifa letu. Nimekumbuka uzalendo wa kujali haki ya kuishi kwa kila Mtanzania, haki ya kutembea na kufurahia maisha ndani ya mipaka ya nchi inayoitwa Tanzania bila ubaguzi bali upendo na amani iliyokuwapo.

Nimekumbuka jinsi tulivyojengewa imani na upendo wa Taifa letu, tulijengewa kuipenda nchi yetu Tanzania kwanza, tulijengewa kuwa na hofu ya Mungu na mambo ya hatari kwa Taifa letu, tulijengewa kuilinda nchi yetu pendwa kwa vile ni mali yetu wenyewe.

Tulifundishwa kutomwonea haya adui, kutomwendekeza adui wa Taifa letu, kutompenda adui wa Tanzania na kumchukulia hatua stahiki adui wa nchi yetu pasi na kupoteza muda. Huu ndiyo uliokuwa uzalendo wa kuipenda nchi yetu Tanzania.

Ninakumbuka jinsi walivyosakwa maadui wa Taifa hili, wavivu na wanyonyaji wa Taifa letu. Majambazi walikuwa na wakati mgumu maana walisakwa mpaka uvunguni bila kupewa upenyo wa kufanya uharamia wa aina yoyote. Walanguzi walikuwa wakiishi kwa muweweseko.

Yote haya yamekuwa ya kukumbukwa tu katika miaka hii, tunaishi maisha ya kukumbuka bila kutekeleza kutokana na kile kinachoitwa utandawazi.

Utandawazi umelikumba Taifa letu na kujikuta tukishindwa kuendelea na misingi ya ulinzi wa nchi yetu, mali zetu na hata uhai wetu.

Utandawazi umetuondolea uzalendo wetu, utu wetu na Utanzania wetu. Tumekuwa watu wa kukurupukana na kudai haki zetu kwa Serikali yetu bila kutimiza wajibu wetu.

Ni wajibu wetu sasa kufungua macho na milango ya fahamu zetu kuiangalia nchi yetu kwa jicho tofauti – jicho la kizalendo.

Tumekuwa mashahidi wa kile kinachoendelea nchini, mashahidi wa jinsi maadui zetu walivyojipanga kutufitinisha sisi kwa sisi, kutaka kuangamiza nchi yetu sasa zinaonekana.

Ndugu zetu wanauawa kwa kuchinjwa kama wanyama. Tunashuhudia yaliyotokea katika sehemu mbalimbali nchini katika kipindi kifupi mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Tanga, Geita, na Arusha.

Watanzania wenzetu wanachinjwa na kuuawa kama wanyama, wanachinjwa na watu wasiofahamika. Sidhani kama kweli wanaofanya unyama huu hawafahamiki kabisa, bali wapo wanaowafahamu na kuwaunga mkono. Hii siyo tabia wala hulka ya Watanzania. Muda umefika sasa wa kuwafichua wale wote wasioitaki mema nchi yetu.

Tanzania ni nchi yetu sote, ni jukumu letu kuhakikisha inakuwa salama ili nasi wote kwa pamoja na vizazi vyetu, tuweze kuishi kwa amani na kufurahia rasilimali za nchi yetu bila kuhofia maisha yetu.

Ni wakati sasa kurudisha uzalendo tulioanza kuupoteza kutokana na umimi ulioibuka katika jamii zetu, uzalendo wa kuwa tayari kwa ajili ya nchi yetu na rasilimali zetu, utayari wa kufichua wale wote wenye nia ovu kwa nchi yetu.

Ni vyema tukafahamu ya kuwa nchi yetu inao maadui wasio tayari kuona tunasonga mbele na kuondokana na adui ujinga, maradhi na umaskini. Maadui hawa wapo tayari kutumia njia mbalimbali kuhakikisha hatusongi mbele. Tuwakatae sasa na kuwafichua ili wote kwa pamoja tuweze kuishi kwa amani na utulivu.

Tanzania ni nchi yetu, tunalo jukumu la kuilinda kwa pamoja.

By Jamhuri