Umoja wa dhati ni muhimu

Jumapili iliyopita wafanyakazi kote nchini waliadhimisha Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani, Mei Mosi. Kitaifa ilifanyika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma ambako wananchi na wafanyakazi walikusanyika kuwakumbuka wafanyakazi duniani, waliokataa dhuluma na kukata minyororo ya mateso na kuweka misingi ya kudai haki katika ajira kulingana na kazi zilizopo na muda maalumu wa kufanya kazi.

Wakati wafanyakazi hao wanasherehekea sikukuu hiyo, bado wamo katika mapambano na tabaka la waajiri ambao bado linaendeleza dhuluma, unyanyasaji na kutofuata sheria na kanuni za kazi, zilizowekwa kwa mujibu wa sheria na mamlaka husika chini ya dola inayotawala tabaka mbili hizo na nyinginezo nchini.

Tabaka la wafanyakazi lina historia ndefu ya mgogoro wa maslahi na tabaka la waajiri. Bado waajiri hawajakiri na kuthamini nguvukazi za waajiriwa wao ndizo zinazoendeleza mitaji yao kwenye maofisi, mashambani au viwandani. Aidha, nguvukazi hizo ndizo zinazowezesha na kuboresha hali ya maisha iwe ya upendo na furaha kwa familia zao.

Kwa sababu baadhi ya waajiri hawana huruma, soni wala mahaba kwa wafanyakazi wao na hivyo hujenga kiburi na kuamini kiboko cha kuwacharaza wafanyakazi ni kuwanyima ujira au mshahara. 

Wafanyakazi wanapolalama na kusema ukweli kuhusu jambo fulani, mwajiri huchomwa moyo na kupandwa jazba na kutimua wafanyakazi kazini. Silaha hiyo hutia hofu wafanyakazi na kuwa baridi kama maji ya mtungini, wasiweze kudai haki yao. Ni unyonge.

Waajiri hao wanapenda mno kupurukusha ili waone wafanyakazi watafanya nini. Wanasahau mgomo bayana au wa siri huteteresha au kufilisi mitaji na viwanda kwenda arijojo na pengine kufa. Wafanyakazi hawana cha kupoteza zaidi ya minyororo ya puuza, kebehi na dhuluma. Kupoteza hayo ni ukombozi kwao na kurudisha utu na heshima yao.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (TUCTA ), Nicholas Mgaya, katika sherehe za Mei Mosi mjini Dodoma, alisema kuwa baadhi ya waajiri wanalipa mishahara midogo isiyolingana na kazi zinazofanywa na wafanyakazi. Wafanyakazi hawapewi mikataba ya kazi wala likizo. Posho na marupurupu sitahiki hazitolewi na waajiri kwa wafanyakazi wao.

Baadhi ya waajiri hawajiungi na mifuko ya jamii wala ya Bima ya Afya ya Wafanyakazi ili kuweka akiba ya uzeeni na afya ya watumishi wao. Ni yumkini hunyima haki na uhuru wa wafanyakazi kujiunga na vyama vya wafanyakazi. Ukweli, waajiri hawapendi wafanyakazi kupata haki zao za msingi. Mambo kama hayo yanapatikana hasa katika sekta binafsi kuanzia viwandani, migodini, maofisini na majumbani.

Ni ukweli pia usiopingika sekta binafsi bado changa. Sawa. Katika uchanga wake basi waajiri waoneshe nia ya kuwasikiliza, kuwajali na kuwapa hicho kiduchu kilichopo kihalali badala ya kuwapuuza, kuwatisha au kuwaachisha kazi kwa kuwapachika tabia ya uvivu, uzembe au udokozi na wizi ili mfanyakazi apoteze haki zake. Hayo yanatokea katika ajira za majumbani, mahotelini, kwenye kampuni na kwenye majumba ya vileo na burudani.

Juzi pale Dodoma, Mwenyekiti wa Chama Cha Waajiri, Mheshimiwa Almasi Maige (MB), amekiri kwamba waajiri wanategemea sana nguvukazi yenye hali nzuri hususani afya, elimu na ujuzi kutoka kwa wafanyakazi. Alisema kuwa waajiri wanataka wafanyakazi kutekeleza kwa uadilifu na ustadi mkubwa kuepuka uvivu, wizi na ufisadi.

Ukweli hiyo ni kauli ya ukombozi kutoka kwa waajiri kwenda kwa wafanyakazi iwapo imetoka ndani ya nafsi ya waajiri siyo kinywani. Ameipigilia mshindo aliposema kuwa wanahitaji ‘uadilifu na ustadi mkubwa.’  Mambo mawili hayo hayatokei kama upepo uvumao kutoka pwani kwenda nchi kavu. Maandalizi na mwendelezo wake ni ushirikiano wa dhati kati ya mwenye mali (mwajiri) na mtunzaji mali (mfanyakazi). Je, hilo waajiri wanalo kwa dhati?

Mwenyekiti huyo amelalama kuwa sekta binafsi inabanwa na sheria kali pale wanapotaka kuwaadhibu wafanyakazi wavivu. Sekta binafsi wanalipa kodi nyingi ni bughudha kwao. Tena upo urasimu katika utekelezaji sheria. Mwenyekiti huyo ameomba sheria ziwe na ukomo kwa utoaji haki kwa wafanyakazi wao kama vile mfanyakazi wa kike anaponyonyesha mtoto mchanga, baada ya kumaliza likizo ya uzazi.

Ndugu yangu Mheshimiwa Almasi ameeleza mazonge hayo yako kwenye sekta binafsi lakini kwenye sekta ya umma hayapo. Inawezekana ikawa hivyo kutokana na taratibu za ajira ni zipi kati ya sekta hizo. Niseme tu kwamba, ukweli huwezi kupata ufanisi na tija mwanana iwapo sifa, weledi, uwezo hauzingatiwi.

Vipi tusiwe na wafanyakazi wazembe, wavivu na wezi badala ya kuwa na wafanyakazi waadilifu na wazalendo kwenye sekta binafsi iwapo taratibu za ajira zinalala kwenye malipo duni na kutolipa ujira? Sifa na uwezo wa mfanyakazi ni vigezo halali vya mtu kupata kazi. Uadilifu na nidhamu mahali pa kazi ndiyo tegemeo kubwa kwa mwajiri. Mwajiri hana budi kujikomboa kifikra ili afanikishe mambo yake.

Ni matarajio ya kila mfanyakazi kuona anathaminiwa, anaenziwa na anasikilizwa wakati wa amani na wakati wa matatizo. Nadhani ni wajibu wa waajiri wa sekta binafsi kujitazama kwa ukweli na undani. Kukiri kosa si kosa, kurudia kosa ni kosa kwa sababu umedhamiria kuwanyanyasa wafanyakazi wao.

Kuundwa kwa utatu yaani Serikali, waajiri na wafanyakazi naupongeza. Kukaa meza moja na kubuni mbinu mpya na bora za kufanya kazi kwa ufanisi na kupatikana tija ni hatua kubwa ya kuleta maendeleo ya kiuchumi ya nchi yetu inayokusudia kuwa ya viwanda.

Ikumbukwe na kuzingatiwa vyombo hivyo vitatu vina wajibu mkubwa kwa wananchi katika mustakabali wa kujenga uchumi imara kutokana na viwanda. Kupanga ni kuchagua na Serikali imeshaonesha dira yake ya maendeleo na mafanikio ifikapo mwaka 2025.

Penye uhai na majaaliwa yake Mola katika Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani mwaka 2017, tunatarajia kusikia na kuona mnyororo wa dhuluma na uonevu umekatwa. Mrija wa unyonyaji kati ya mwajiri na mwajiriwa umechomwa moto. Uwiano wa hali ya maisha kati ya mwajiri na mfanyakazi angalau unalingana. Uvivu, uzembe, wizi na rushwa vinazikwa. Uzalendo, uadilifu na hapa kazi tu vinatawala anga zote kazi. Uhuru ni Kazi