Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,  alituasa kwamba tufanye juhudi kuziba ufa mkubwa uliojitokeza katika Muungano wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, na kuendelea kuainisha nyufa nyingine. Lakini ni kama hatukumsikiliza na kumjali.

Ibara ya 1 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kama ilivyorekebishwa, (Katiba ya Muungano) iliyoanza kutumika Aprili 26, 1977, inatamka; “Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano.” Ibara 2 (1) inaendelea, “Eneo la Jamhuri ya Muungano ni eneo lote la Tanzania Bara na eneo lote la Tanzania Zanzibar, na ni pamoja na sehemu yake ya bahari ambayo Tanzania inapakana nayo.”


Wakati huo huo, unakuta ibara 2 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Toleo la 2010, inatamka kwamba, “Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

 

Ibara hiyo inatokana na kifungu 4 cha Sheria ya Zanzibar, Namba 9/2010, na iliyotungwa kinyume cha utaratibu wa kubadilisha Katiba ya Muungano na baadhi ya sheria uliopo kwenye kifungu 98 cha Katiba ya Muungano, na baada ya kifo cha Mwalimu kilichotokea Oktoba 14, 1999.

 

Kana kwamba uvunjaji huo hautoshi, utakuta ibara 2(2) ya Katiba ya Muungano inafafanua, “Kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano au Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Rais aweza kuigawa Jamhuri ya Muungano katika mikoa, wilaya na maeneo mengineyo, kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge. Isipokuwa kwamba Rais atashauriana kwanza na Rais wa Zanzibar katika kuigawa Tanzania Zanzibar katika mikoa, wilaya au maeneo mengineyo.”


Lakini ibara 2A ya Katiba ya Zanzibar inayotokana na kifungu 5 cha Sheria Namba. 9/2010, inatamka, “Kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za Serikali, Rais aweza kuigawa Zanzibar katika mikoa, wilaya na maeneo mengineyo kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi.” Katika ibara 134 (1) ya Katiba ya Zanzibar, “Rais” maana yake ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

 

Sasa, jiulize, Tanzania ni nchi moja au mbili? Nani ana haki ya kugawa Tanzania Zanzibar katika mikoa, wilaya na maeneo mengineyo – Rais wa Jamhuri ya Muungano au Rais wa Zanzibar? Si uvunjaji wa ibara 98 iliyotajwa hapo juu uliofanywa mchana kweupe, Watanzania wakitizama, kila mtu macho mawili na masikio mawili?


Kwenye udini tukoje? Mwaka 1995, Mwalimu alituonya kuhusu udini kwamba, kwa mujibu wa Katiba ya Muungano, Serikali haifungamani na madhehebu ya dini yoyote. Na kwa kweli, katika miaka 35 ya uhai wa Katiba ya Muungano, tulikuwa hatujasikia kuchomwa, kuvunjwa kwa makanisa na kuporwa kwa vifaa vya ibada, na kukojolewa vitabu vitakatifu kama ilivyotokea Oktoba, 2012.

 

Labda Rais Jakaya Kikwete na serikali yake wahimizwe kujali Tamko la Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF) la Desemba 2012, “Tabia ya kuachia uchochezi wa kidini kuendelea pasipo hatua madhubuti kuchukuliwa na dola, ni udhaifu mkubwa wa uongozi na uwajibikaji.” Pia, katika gazeti la Tanzania Daima la Desemba 27, 2012, mhariri alionya, “Matukio haya Zanzibar hayatatuacha salama.”

 

Mwenye macho na masikio aende hapo kituo cha mabasi cha Mwenge, Dar es Salaam, ambako wanaojiita Wakristo na Waislamu wanajibizana katika mihadhara mchana kweupe. Kituo cha Polisi na kituo cha televisheni cha ITV havipo mbali na mihadhara hiyo. Nchini Marekani utaruhusiwa kuishi hata kama huamini Mungu yupo, ilimradi unafuata sheria za nchi. Si utakufa siku moja upate kujua kama Mungu yupo au hayupo?

 

Tanzania Bara imetelekeza Kiswahili kana kwamba ni mtoto yatima. Au pengine tuseme Kiswahili hicho kimeingiliwa na kirusi cha Kiingereza hadi kimekuwa chotara. Tunashindwa kukumbuka kwamba ni Kiswahili kilichotuunganisha Watanzania, ambao sasa sensa inasema Bara tuko milioni 43,625,434, na Zanzibar milioni 1,303,568; kilichotuwezesha, makabila 126, ya lugha tofauti, kumng’oa mkoloni na Tanzania Bara kutwaa Uhuru tarehe 9 Desemba,1961.


Hata mwaka 1977 Tanzania ikatunga Katiba ya Muungano yote yenye ibara 152 na jedwali mbili katika lugha murua ya Kiswahili kinachozingatia lugha ya kisheria. Mahakama ya Rufani ya Tanzania iliimarisha Kiswahili hicho katika uamuzi ilioutoa katika kesi ya Director of Public Prosecutions Daudi Pete [1993] TLR 22 (Mkurugenzi wa Mashitaka wa Serikali dhidi Daudi Pete, Riporti za Kesi za kisheria Tanzania, ukurasa 22).

 

Katika uamuzi huo Mahakama ilifafanua kwamba kwa kuwa Katiba ya Muungano imeandikwa katika lugha ya Kiswahili, lazima daima tuzingatie kwamba lugha inayotawala katika kutafsiri Katiba ya Muungano ni Kiswahili.

 

Leo hii, mijini, kwa kuona ufahari, Kiswahili kinachanganywa na Kiingereza bila tafsiri, katika mazungumzo ya kawaida, hotuba za kisiasa, na kiuchumi, mahubiri ndani ya nyumba za ibada, Bunge ambamo wanawakilishwa watu wa kawaida, magazeti, vyombo vya habari, vikao vya harusi, misiba, na kadhalika.

 

Pia, vichochoroni mijini, utakuta mahali ambako Mzungu hata mmoja hajawahi kukanyaga tangu tupate Uhuru pameandikwa, “Saloon”, “Butchery”, “Restaurant”, “Cosmetics” na kadhalika. Wakati, mwingine maandishi katika Kiingereza yanakosewa “Stationary” badala ya “Stationery”; “breackfast” badala ya Breakfast”, na kadhalika.


Tanzania Zanzibar imezidi Bara uzalendo

(1) Ibara 87 ya Katiba ya Zanzibar inatukuza Kiswahili kama ifuatavyo: “87. (1) Bila ya kuathiri kifungu hiki, lugha rasmi ya Baraza la Wawakilishi itakuwa ni Kiswahili.


(2) Kila Muswada (pamoja na vijalizo vilivyofuatana na muswada), kila sheria inayotungwa na Baraza, kila Sheria ya msingi au sheria inayopendekezwa chini ya chombo cha sheria na Baraza, maafikiano yote ya kifedha na nyaraka zenye kuhusiana na kila sheria halisi au inayopendekezwa, kusahihishwa au inayoendelea itaandikwa kwa lugha ya Kiswahili na ikihitajika kwa lugha ya Kiingereza.”

 

Vile vile, tulionywa kuhusu athari za ukabila. Leo hii utakuta mtu anazungumza kilugha na mtu wa kabila lake bila kujali watu wa kabila nyingine ambao wako hapo. Fuatilia ndani ya daladala.

 

Hivi kuna mtu aliyechagua kuzaliwa mashariki, magharibi, kaskazini au kusini mwa Tanzania? Mpango wa zamani wa kitaifa wa Mwalimu wa kulazimisha watoto watafute elimu mbali na nyumbani kwao ili wachanganyike na watoto wa makabila mengine haupo tena. Leo, chukua mfano wa Dar es Salaam, wa Ilala wanasoma Ilala, wa Kinondoni wanasoma Kinondoni, wa Temeke wanasoma Temeke – wanafunzi hawafahamiani. Hivi, kwa sababu tu mtu ni wa kabila lako, awe rubani wako wa kukuendesha kwa ndege au daktari wako wa kukupasua kichwa katika mwaka wake wa kwanza wa masomo?


Pia, kuna suala la aina ya elimu. Tumeshaonywa vya kutosha tukae chonjo ubora wa elimu usiparaganyike kiasi cha ajabu kabisa. Onyo la kwanza linaweza kuwa la Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi alipotoa hotuba yake katika Mkutano wa Viongozi na Wataalamu wa Elimu Bara la Afrika kuanzia Oktoba 5-7, 2012.


Bila kujali historia sahihi ya Tanzania, aliuambia Mkutano huo kwamba Tanzania iliundwa mwaka 11964 kwa kuunganisha visiwa vya Bahari ya Zimbabwe na Pemba vilivyoungana na nchi ya Zanzibar iliyokuwa ikiitwa Tanganyika!

 

Ukweli ni kwamba mwaka 1964 na si 11964 na kwamba Tanganyika iliungana na Zanzibar. Ibara 1 ya Katiba ya Zanzibar inatamka, “Zanzibar ni nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na visiwa vidogo vilivyoizunguka Zanzibar ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.” Kwa hiyo, suala la Zimbabwe kuwa katika Muungano halipo.

 

Onyo la pili ni la ajuza aliyeripotiwa kwamba ni mwenyeji wa Morogoro mwenye umri wa miaka 105 na ajuza huyo alisema anakaa pamoja na Kikwete Ikulu, amsaidie kupata hati yake ya nyumba aliyotapeliwa. Onyo la tatu lilikuwa katika gazeti la Januari 1, 2013 chini ya kichwa cha maneno, “Wasiojua kusoma wachaguliwa kujaza shule za kata”

 

Elimu nchini imeparaganyika. Kuna shule ambamo watoto wanaketi chini, hawana vyoo, hawana madawati, watoto waliofaulu kwenda sekondari hawajui kusoma na kuandika, walimu hawalipwi mishahara ya kutosha, wazazi wanachangishwa michango mbalimbali. Kuna Shule ambazo zina ubora kweli ambazo zinaitwa “English Medium.” (Mafunzo kwa Kiingereza).

Wengine wamepata shahada nje ya Tanzania. Wakirudi nchini, wanatamba kwamba elimu ya nje ina ubora sana na kubagua wahitimu wa baadhi ya vyuo vya hapa nchini. Matokeo yake ni kwamba wote waliosoma hapa nchini, na wale ambao walisoma nje ni wachache ambao wana nia ya kushughulikia maendeleo ya nchi hii.

 

Nathubutu kusema kwamba, Mwalimu, asingekuwa anatokeatokea na hotuba zake katika vyombo vya habari, ni Watanzania wachache ambao wangejua kwamba aliwahi kuishi. Kama unabisha, taja kwa majina mawaziri wote katika Baraza la Mawaziri la Kwanza katika Serikali ya Tanzania Bara (Tanganyika). Na kama bado unabisha, taja sababu za barabara inayotoka Mnazi Mmoja hadi Ofisi Ndogo ya CCM, Dar es Salaam, kuitwa Barabara ya Lumumba. Watanzania walio wengi tunashabikia habari za nchi za nje – Manchester United, West Ham, Barcelona . n.k.

 

Hatari ya ubinafsi Tanzania

Ubinafsi nao ni hatari kubwa Tanzania – yaani, “mimi kwanza.” Anayetaka kuelewa fika ubinafsi wa Watanzania atembelee miji ya Tanzania ambako kuna shida ya usafiri wa umma, hasa aende Dar es Salaam ajionee. Huko atakuta mabasi mengi ya abiria yana mlango mmoja wa kuingilia na kutokea.

 

Kila mmoja utamwona anataka aingie au atoke akiwa wa kwanza, bila kujali kama wanaotaka kuingia au kutoka pia ni watoto, wajawazito, wazee, wasioona, wasiosikia, walemavu wa viungo vingine na kadhalika.

 

Mtoto atalazimishwa kusimama ndani ya basi, ili mtu mzima akae ingawa mikono ya mtoto haiwezi kufikia vishikizo vya chuma ambavyo vimewekwa kwenye dari la basi na mtoto hawezi kuhimili mikikimikiki ya basi katika kusafiri, kama mtu mzima.

 

Utashangaa kukuta abiria ni wale wale ambao wanahubiriwa kwenye nyumba za ibada, “Mpende mwenzako kama unavyojipenda mwenyewe.” Unashangaa na kujiuliza kama abiria si wale wale wenye kulazimishwa kupanga foleni hospitali na kwenye ATM.

 

Watu wameishaharibikiwa hata utawaona wasafiri wa Kitanzania kwenye uwanja wa ndege wakilundikana kwenye mlango wawe wa kwanza kuingia. Na hii inatokea ingawa kila msafiri hupewa tiketi ya ndege ambayo inamhakikishia nafasi ya kukaa ndani ya ndege.

 

Tangu Azimio la Arusha, mwaka 1967 lilipopinduliwa kinyemela na Azimio la Zanzibar mwaka 1992, lililoingiza nchini soko huria Tanzania, shabaha ya Tanzania kujitegemea kama ilivyoanishwa katika ibara 9 ya Katiba ya Muungano imebaki kuwa porojo. Tanzania imevamiwa kiuchumi na wawekezaji wa nje (wengine bandia) kwa msingi wa msemo kwamba “wajinga ndiyo waliwao.”

 

Laiti Watanzania tungekuwa bado tunaunganishwa katika kujenga Taifa kwa kutimiza madhumuni ya sheria ya mwaka 1964 ya kujenga Taifa! Imeripotiwa kwamba sheria hiyo ilisitishwa matumizi yake mwaka 1994 na kufufuliwa Januari 2013, kwa nia ya kuita vijana wajiunge na jeshi hilo ambao ni wanafunzi wa kidato cha sita 5,000, Machi 2013.

 

Kabla ya kufutwa kwa sheria hiyo ililiondolea Taifa kero za ukabila, ubinafsi, udini kutotumia Kiswahili, kuondoa kiburi kitokanacho na elimu, kutokuwa mzalendo na kadhalika.


Watu waliishi pamoja kwa mtindo wa abiria ndani ya daladala kukaa asiyeoa na mwanandoa, msichana au mvulana na mtu mzima au mlemavu, na kadhalika; au kwa mtindo wa kuegesha magari kwenye Uwanja wa Taifa, bila ya mwenye Volkswagen, Prado, Toyota, Benz na kadhalika kutafuta kuegesha gari lake pamoja na gari la aina ile ile ya gari lake.


Sheria hiyo, miongoni mwa mambo mengine, ililazimisha wanaume na wanawake, wakiwa raia wa Tanzania kati ya miaka 16 na 35 kuitwa ili wajiunge na jeshi hilo kwa mwaka mmoja au mitatu. Waliolazimika kujiunga waliainishwa kutoka vyuo 13, vyuo vya mafunzo sita, vituo vya mafunzo saba na shule nne wakitokea maeneo tofauti ya Tanzania: Bumbuli, Butimba, Dar es Salaam, Katoke, Kilombero, Korogwe, Kunduchi, Machame, Marangu, Morogoro, Moshi, Mpwapwa, Musoma, Nyegezi, Tabora, Tanga na Ukiruguru.


Miaka hiyo, walikaa chini ya nidhamu ya kijeshi. Madhumuni ya sheria hiyo ni kuwafundisha vijana raia wa Tanzania kutumikia Taifa katika nyanja za maendeleo ya jamii, uchumi na ulinzi wa nchi yao; kuwapa elimu ya kijeshi kwa nia ya kuwawezesha kutafutiwa kazi au kuajiriwa kama askari wa miguu katika vikosi vya JWTZ; na kushiriki katika shughuli za kulinda Taifa. Matumizi ya sheria hii sasa hayavumi na kushabikiwa kwa miaka 18 hadi sasa.


Kama alivyotuasa Mwalimu, tuchunguze nyufa katika “Nyumba inayoitwa Tanzania”, hasa sasa kwa kuwa tuko katika harakati za kuunda Katiba Mpya. Tuachane na porojo za kuwa wamoja, watulivu, wapenda amani na mshikamano.


Mapema kabla ya kusingizia Mtwara na Lindi nia ya kutaka kuvunja nchi vipande vipande, tulipaswa kukemea kwa sauti zetu zote kuvunjwa kwa Katiba ya Muungano. Sote tulikuwapo. Asiyeziba ufa hujenga ukuta!

Mwandishi wa makala haya, Novatus Rweyemamu, ni Wakili Mwandamizi na anapatikana kupitia simu: 0784 312 623


1356 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!