Tanzania haiwezi kuendeshwa kupata maendeleo mazuri iwapo viongozi wake ni watu wenye unafsi katika kuyaendea maendeleo ya dunia, kama kanuni za sayansi zinavyotaka na imani ya Muumba wetu inavyotaka na inavyoagiza katika kuyakabili mazingira yetu nchini.

Ifahamike kwamba Tanzania ni nchi; ni jumuiya wala si taasisi kama Chama Cha Mapinduzi, Chadema au TLP.  Wala si dini ya Kiislamu, Kikristu au kipagani. Ni umoja wa watu (Watanzania) wenye malengo na madhumuni ya kujenga Taifa bora na lenye watu walio na maisha mazuri kwa njia ya ukweli na haki tu.

Kupata Taifa bora na lenye watu wa sifa nzuri na wanaozingatia misingi ya kufanya kazi, tabia ya kusema ukweli na kutendeana haki, watu wake hawana budi kukemea mtu aliyepo madarakani asipewe mwanya wa kutumia nafasi yake kuleta matatizo katika Taifa la watu wema na wazuri.

Matatizo tunayopata mara kwa mara katika vyombo vya Serikali, mashirika ya umma, vyama vya siasa na madhehebu mbalimbali ya dini zetu nchini, yanatokana na unafsi wa watu katika makundi hayo. Fulani anaamini na kujiona yeye ndiyo mwenye maarifa, uwezo na ujuzi wa jambo.

Nafsi ni roho. Ni mtu mwenyewe na ni kiini au dhati ya jambo au kitu ambacho mtu anaona ni kizuri kutenda. Upo unafsi wa aina nyingi ukiwamo fitina, woga, ukweli, hiyana, haki n.k. Unafsi unapotekelezwa ndani ya jamii huleta matatizo.

Ili nieleweke na Watanzania wenzangu, hasa hasa vijana wetu, nimenakili baadhi ya maandishi kutoka katika kijitabu ‘TUJISAHIHISHE’ cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Kwanza wa nchi hii, kuanzia mwaka 1962 hadi 1985.

Nakili, “Wengine hugawa watu katika mafungu. “Fulani” japo akifanya kosa kubwa sana hasemwi. Lakini ‘Fulani’ wa pili akifanya kosa japo dogo, kosa lile hukuzwa likawa kama Mlima Kilimanjaro. Hawa hutafuta sababu za kumtetea ‘fulani’ wa kwanza, au kumlaumu ‘Fulani’ wa pili, ambazo hazifanani kabisa na ukweli.”

“Fulani wa kwanza akisema katika majadiliano kuwa mbili na mbili ni tano, wao watakubali. Lakini ‘Fulani’ wa pili akisema sivyo, mbili na mbili ni nne, watamwona ni mtu mbaya kabisa ambaye hastahili hata kusikilizwa. Hawa hawajali ukweli hujali nafsi tu, kwao ukweli ni maoni yao na matakwa yao”.

“Makosa yetu mengine hutokana na woga: woga unaotuzuia kumlaumu mkubwa japo tunajua kuwa kakosa, au kumtetea mdogo anayelaumiwa na wakubwa japo tunajua kuwa hana makosa. Na msingi wa woga pia ni unafsi. Pengine huwa tunaogopa sisi wenyewe kulaumiwa au kupata hasara Fulani.”

“Makosa ni makosa na dhuluma ni dhuluma japo watendao makosa hayo au dhuluma ile ni wakubwa au ni wengi. Chama kinachopenda ukweli na haki hakina budi kiwape wanachana wake uhuru na nafsi ya kusahihisha makosa na kuondoa dhuluma”

“Kosa jingine kubwa ni kuwagawa watu katika makundi; kundi “letu” na kundi “lao”. Wakati mwingine “sisi” ni viongozi tunaochaguliwa kwa kura za wanachama. Hili ndilo kundi “letu”. Viongozi wengine ni wale wanaoajiriwa. Baadhi ya viongozi wanaochaguliwa hujiona kuwa ni mabwana, na kwamba viongozi wanaoajiriwa ni watumishi tu ambao hawastahili kuheshimiwa.”

“Wengine humwona mwenzao anafanya kosa. Badala ya kumwambia pale pale kijamaa kwamba atendalo ni kosa, watanyamaza kimya. Lakini hawanyamazi kabisa watakwenda kumteta katika vikundi vya siri siri. Matendo hayo si ya kumsaidia mwenzao, ni ya kumdhuru.”

 

>>ITAENDELEA 

1012 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!