Msimu uliopita, Dar es Salaam Young Africans (Yanga) yenye makao yake mitaa ya Twiga na Jangwani jijini iliyokuwa ikitetea ubingwa wake, ilifundishwa na makocha watatu kwa nyakati tofauti.

Kwanza ilianza ligi hiyo, Agosti mwaka jana ikiwa na Sam Timbe, Mganda ambaye hata hivyo alifukuzwa miezi michache baadaye na nafasi yake kuchukuliwa na Kostadin Papic, raia wa Serbia, lakini pia akawa nayo kwa kiasi cha miezi minne tu na kutimuliwa.

Alifukuzwa kwa kigezo cha kumaliza mkataba wake wa kazi mwishoni mwa Aprili, mwaka huu, na timu hiyo kubaki mikononi mwa kocha msaidizi na beki mahiri wa zamani wa kimataifa wa timu hiyo, Fred Felix Minziro.

Mbali ya Timbe, Papic na Minziro, makocha wengine walioifundisha Yanga kuanzia mwaka 2000 hadi Aprili 2012, ni Raul Shungu (marehemu), Charles Boniface Mkwasa, Polycarp Bonganya, Syllersaid Mziray (marehemu), Kennedy Mwaisabula, Jack Chamangwana, Sredojevic Milutin Micho na Dusan Kondic.

Tayari tena imepata kocha mpya, Thomas Saintfiet (au Uncle Tom) aliyeingia mkataba wa kuinoa kwa miaka miwili, kazi aliyoianza siku 12 zilizopita katika Uwanja wa Kaunda, Dar es Salaam unaomilikiwa na Yanga yenyewe.

Jambo la kusisimua siku zote timu hiyo inapoleta kocha mpya ni mapokezi. Anapokewa kwa shamrashamra kubwa anapowasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini, mapokezi yanayofanywa kwa mbwembwe nyingi na mashabiki wake kutokana na hamasa ambayo inaongozwa na viongozi.

Ndivyo walifanyiwa Sam Timbe na Papic kila mmoja alipowasili. Lakini wanavyokuja kwa kishindo ndivyo pia wanaondoka, wengine wakiachana na timu hiyo kwa kutupiana maneno na kuhangaishwa kupata haki zao.

Mbali na hilo, makocha hao kuna wakati huletwa kwa siri bila ya aliyepo kufahamu nini kinaendelea dhidi yake, kisha anapata taarifa hizo kupitia katika vyombo vya habari hasa anapokwenda kwao likizo au kuitembelea familia yake.

Ndicho kilimkuta Sam Timbe aliyekuwa hajui lolote kuhusiana na ujio wa Papic, wakati huo akiwa mapumzikoni kwao Kampala, Uganda wakati Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ikiwa imemalizika mzunguko wa kwanza.

“Mimi sina taarifa yoyote. Najua nipo kazini na kama wakinifukuza inabidi wanilipe fidia kwa mujibu wa mkataba niliosaini nao. Hata wakitaka kunipa kazi nyingine tulipane kwanza ndipo tuanze majadiliano,” alisema kocha huyo alipopigiwa simu kufahamishwa na vyombo vya habari kuwa ametimuliwa na Yanga.

Papic naye alipomaliza muda wake wa takribani miezi sita tu aliondoka kwa mvutano wa mshahara na haki nyingine, suala ambalo hata hivyo lilianza mapema zaidi wakati timu hiyo ikijiwinda kwa michuano ya Klabu Bingwa Afrika alipodai kutotimiziwa makubaliano kati yake na timu hiyo.

Alilalamikia usafiri wa kumpeleka mazoezini na kumrudisha akisema alikuwa hapewi hata mafuta ya gari, na kwamba alipangishiwa kuishi hoteli ya kiwango cha chini ikilinganishwa na hadhi aliyonayo.

Lakini madai yake hayo yalikanushwa na Katibu Mkuu wa Yanga, Celestine Mwesiga aliyemtaka ausome vizuri mkataba wake huku naye akimshutumu kupenda sana makuu, kwamba alipotakiwa kuileta nchini familia yake badala ya kuendelea kuiacha kwao Serbia hakutekeleza.

Akamshutumu pia kuwa alipenda sana kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu mambo ya Yanga wakati haikuwa kazi yake, na kwamba hata hoteli aliyokuwa akitaka apangishiwe ni ya gharama kubwa mno kutokana na kupenda kwake anasa.

Ndiyo maana mkataba wake mfupi ulipomalizika tu hakuongezewa mwingine, lakini kama adhabu akakumbana na mvutano mkubwa na uongozi wa Yanga. Alijikuta akihangaikia malimbikizo ya mishahara, madai ambayo nayo yalikanushwa na viongozi wa timu hiyo.

Hata hivyo, madai ya kulimbikiziwa mishahara na posho nyinginezo hayakuishia kwa Papic pekee. Kocha msaidizi wa timu hiyo, Fred Minziro pia naye aliibuka nayo. Alisema anaidai Yanga fedha nyingi na kutangaza kuwa asingeendelea kuinoa timu yake endapo isingemlipa haki zake hizo.

Alichukua uamuzi huo wakati ikihitaji kocha wa kumfundishia kikosi chake, kikubwa zaidi ikiwa maandalizi ya kutetea ubingwa wake wa michuano ya Kombe la Kagame iliyoanza mwishoni mwa wiki, kazi aliyokuja kuifanya baada ya madai yake kutekelezwa.

Tayari Uncle Tom, raia wa Ubelgiji, ameianza kazi hiyo akiwa na uzoefu wa kufundisha soka barani Afrika na kutimuliwa. Alikumbana na hali hiyo huko Nigeria, Namibia, Zimbabwe na Ethiopia alikodumu kwa miezi mitano tu, kule ambako alifikia hadi hatua ya kunyimwa mshahara wake.

Alipokuwa kocha wa timu ya taifa ya Namibia, Uncle Tom alipigwa vita na makocha wazalendo wakihoji kwa nini wasipewe kazi hiyo wao, hatua iliyomfanya akimbilie Zimbabwe mwishoni mwa mwaka 2010. Huko alipewa mkataba wa kuinoa timu ya nchi hiyo kwa miaka minne, lakini akanyimwa kibali cha kufanya kazi nchini humo!

Kama ilivyotokea Namibia, makocha wazalendo pia hawakumuunga mkono alipokuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa timu ya taifa ya Nigeria (Green Eagles) mapema mwaka huu, walianzisha malumbano makubwa baina yao na Chama cha Soka cha nchi hiyo (NFF) naye kuamua kuondoka.

Ingawa bado ni mapema kujua endapo ataiweza Yanga na kudumu nayo kwa miaka hiyo miwili aliyotia saini, lakini anasema amekubaliana na hali aliyoikuta ndani ya klabu hiyo akisema haina tofauti yoyote na sehemu nyingine alizopitia Afrika.

“Mimi naielewa Afrika kuliko mnavyodhani. Niko tayari kushirikiana na wadau wa Yanga ili kuiendeleza timu yao itishe katika bara hili,” alisema kocha huyo muda mfupi baada ya kutia saini mkataba wa kuianza kazi hiyo takriban wiki mbili zilizopita.

Pamoja na malengo mengine, Uncle Tom anataka kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara inayoanza mwezi ujao, kisha timu hiyo ifike mbali katika Ligi ya Mabingwa Afrika tofauti na miaka yote iliposhiriki michuano hiyo katika historia yake.

Lakini kama ilivyotokea mara nyingi kwa makocha wa timu hiyo kupokewa kwa nderemo, vifijo na hoihoi na kuja kutupiwa virago vyao, yeye atadumu hadi lini ama naye atafukuzwa kama wenzake wakiwamo wawili wa karibuni zaidi akina Sam Timbe na Kostadin Papic?

1071 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!