Tunapongeza hatua iliyochukuliwa na serikali kwa wakulima wa korosho. Japo matokeo ya uamuzi huo hayajajulikana, lililo la msingi ni kuwa serikali imeonyesha kuwajali wananchi hao.

Historia inaonyesha kuwa kwa miongo mingi wakulima wa mazao ya aina zote wamekuwa wakidhulumiwa licha ya matamko mengi ya kuwatia moyo.

Ufisadi mkubwa umekuwapo kwenye sekta hii kiasi cha kuwafanya wakulima wengi waishi na hatimaye wafariki dunia wakiwa katika lindi la umaskini.

Tunaipongeza serikali tukiamini kuwa hatua ilizoanza kuchukua hazitaishia kwa wakulima wa korosho pekee, bali zitaenea hadi kwa wakulima wa mazao mengine ya biashara na chakula.

Wakulima wa mazao kama ndizi wamekuwa wakinyonywa kwa kiwango cha kutisha na genge la wafanyabiashara wenye mitandao imara kweli kweli.

Wanyonyaji hawa hawatambui wala kuheshimu dhiki kubwa wanazopata wakulima kwa kipindi chote cha kuandaa mashamba, kuyatunza hadi kuvuna.

Wafanyabiashara huenda mashambani kununua mazao, na hata pale ambako wakulima wameshtuka na kwenda wenyewe kwenye masoko wamekutana na vizingiti vingi mno.

Tunatoa mwito kwa serikali kuhakikisha vyama vya ushirika vya wakulima vinafufuliwa na kuachwa kwa wanachama wenyewe ili waweze kuviongoza kwa maana ya kuratibu masoko na mapato.

Wakulima wapewe elimu yenye kuwawezesha kuwa na uthubutu wa kusaka masoko ya ndani na hata nje kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya mawasiliano.

Utetezi wa serikali na wadau wa maendeleo hauna budi kuwapo na kuonekana kwa dhati ili kuwawezesha wakulima kutendewa haki.

Pamoja na hayo, serikali iendelee na utaratibu kama iliouchukua kwenye soko la korosho kwa kuwa mtetezi nambari moja wa wakulima. Dunia ya leo si ya maliwali, bali ni dunia iliyojaa hadaa na dhuluma.

Ni makosa makubwa kuamini kuwa soko huria likiachwa lenyewe linaweza kuwatendea haki wakulima. Duniani kote, serikali zote makini huwa haziachi dhuluma itendeke kwa watu wake kwa kigezo cha soko au biashara huria.

Tunaipongeza serikali kwa hatua iliyochukua kwa kuwakomboa wakulima wa korosho tukiamini kuwa huo ni mwanzo wa safari halali ya kuwatetea wakulima wote nchini.

Tunatoa mwito kwa wafanyabiashara wenye tamaa ya kuwaumiza wakulima kujiepusha na dhuluma hiyo, kwani kufanya hivyo si tu kuwa ni uoenevu, bali ni machukizo hata kwa Mwenyezi Mungu. Wakulima wana haki ya kufaidi jasho lao. Hongera kwa wote walioamua kuwatetea.

1799 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!