Juma lililopita Rais John Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza katika Bandari ya Dar es Salaam iliyoibua masuala kadhaa. Madhumuni ya ziara yalikuwa kuhakiki iwapo mafuta yaliyohifadhiwa kwenye matangi hapo bandarini yalikuwa ghafi au la, ili kubaini ushuru sahihi wa kulipia mafuta hayo.

Zipo sababu nyingi kwanini rais analazimika kwenda bandarini kukagua shehena ya mafuta, lakini ni moja ambayo ndiyo ya msingi zaidi: wale ambao wanapaswa kukagua hiyo shehena, ama hawajafanya kazi yao, au hawajaifanya kwa ukamilifu.

Kutokufanya kazi au kutoifanya kikamilifu kunaweza kusababishwa na mengi: kuzembea kazini, kutofahamu kazi, au kuleta janjajanja kazini.

Sababu nyingine ya kumpeleka rais bandarini inaweza kuwa anafanya kazi na watu ambao hawaamini, ambao analazimika kuwafuatilia kwa karibu. Siamini kama hii ndiyo sababu kwa kuwa ana uwezo mkubwa wa kuteua watendaji katika nafasi mbalimbali na tumeona mifano mingi ya kutengua uteuzi wa watendaji katika nafasi mbalimbali.

Sababu nyingine nitaiita sababu ya kisiasa, na natumia neno hili kwa maana yake halisi, siyo kwa maana ya kejeli. Siku atakapoapishwa rais wa awamu ya sita, mimi na wewe tutakaa kutoa alama za kufaulu au kufeli kwa rais wa awamu ya tano. Hatutawapima wale jamaa ambao hawajui au walishindwa kutimiza wajibu wao na kusababisha ziara za rais bandarini.

Na ni sababu hii ya kisiasa inayofanya yule ambaye “siyo kazi yake” kulazimisha kuwa yake. Kila mtu ana kazi na wajibu wake, lakini hatimaye kazi za Watanzania wote na mafanikio au kutofanikiwa kwa kazi hizo ni tatizo la rais. Ni suala ambalo linapaswa kumkosesha usingizi, na iwapo halimkoseshi usingizi tuna haki ya kuwa na wasiwasi na uwajibikaji wake.

Wote, pamoja na wale tuliopewa kazi na hatukutimiza wajibu wetu, tutakaa kumjadili na kumkosoa rais mstaafu ambaye alishindwa kusimamia kwa ufanisi utekelezaji wa shughuli za serikali yake. Ni mtu mmoja tu atasimamishwa kizimbani ndani ya mahakama ya jamii kujibu matatizo ya maelfu na maelfu ya watendaji wake.

Kwa hali kama hii ni rahisi kukubali umuhimu wa hatua anazochukua rais kukabiliana na usimamiaji hafifu wa shughuli mbalimbali za uongozi, lakini wakati huo huo, si rahisi kupuuzia athari za kufanya hivyo.

Hoja ya msingi kabisa kwanini rais hapaswi kufanya kazi hizi ni kuwa wapo watu wanalipwa mishahara kwa kazi ambayo hawaifanyi. Ingeleta maana zaidi waondolewe kwenye nafasi zao za kazi halafu huo mshahara tumuongezee rais, lakini hili litakuwa suluhisho la kinadharia zaidi kwa sababu rais hawezi kufanya kazi za kila mtu ambaye hawajibiki, na bado akapata muda wa kufanya kazi zake mwenyewe.

Naamini kila awamu, kwa viwango tofauti, imekuwa na hali hii ya viongozi kulazimika kuingilia kazi ambazo siyo zao. Lakini naamini pia kama kiwango kile kinazidi kuongezeka.

Hili suala kwamba wale wanaopewa majukumu yao hawayakamilishi kwa ukamilifu ni suala ambalo lipo sehemu kubwa ya nchi yetu na halimhusu rais pekee. Tumeliona kwa viongozi katika ngazi mbalimbali siyo tu serikalini na kwenye sekta ya umma, lakini lipo hata kwenye sekta binafsi.

Ukichunguza kwa undani, ni tatizo ambalo limeenea katika nyanja zote za maisha yetu, hata kwenye familia zetu. Ni janga la kijamii. Anachofanya rais ni kutukumbusha tu juu ya tatizo ambalo limeshamiri miongoni mwetu.

Suluhisho la muda mrefu litakuwa kujenga msingi wa kielimu kwa wale tunaowalea kuona umuhimu wa uwajibikaji na uadilifu katika kila jambo la maisha. Maana yake ni kuwa anayeaminiwa kutekeleza jukumu fulani, alitekeleze kwa uwezo wako wote, na kwa bidii kubwa.

Lakini hatuwezi kusubiri watoto wetu waje kurekebisha tatizo lililopo. Kuna wajibu wa kuchukua hatua sasa. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wanaweza kutusaidia kuleta suluhisho. Nimesoma maandiko yanayojenga hoja kwamba hakuna mfano bora wa raia asiyekubali uwajibikaji hafifu kuzidi yule anayelipa kodi.

Mlipa kodi ana mkataba na wote wanaokula kodi yake kuwa anakubali kukatwa kodi ili wale wanaonufaika na kodi ile kwa njia ya mshahara watekeleze majukumu yao kazini na kwa jamii. Wanaposhindwa kuetekeleza majukumu yale mlipa kodi anapaswa kuwa mtu wa kwanza kumtumbua asiyewajibika.

Katika mazingira kama hayo itakuwa kila mara rais anapopanga safari ya kushtukiza bandarini, kabla hajafika kwenye lango kuu la Ikulu safari yake inakatishwa kwa taarifa kuwa kajitokeza mlipa kodi mmoja ambaye ameibua tatizo na ambalo mamlaka husika zimechukua hatua kulimaliza.

Katika mazingira ya sasa wengi tunaamini kuwa uongozi ni wajibu wa wale wanaoitwa waheshimiwa peke yao, au wale wanaoteuliwa na rais. Uongozi ni wa kila mmoja wetu. Rais pamoja na viongozi wengine wateule serikalini na kwenye sekta ya umma hawawezi kuongoza peke yao.

Muhimu zaidi, na ndiyo maana napendekeza msaada wa Mamlaka ya Mapato, ni kuwa ile pesa ya kuendesha Serikali ni pesa ya walipa kodi. Tukianza kuiona kama ni pesa yetu, tutaanza kupaza sauti dhidi ya vitendo vya kutokuwajibika. Tatizo la sasa ni kuwa kwa sababu tunaiona kama ni pesa ya Serikali tunaamini kuwa si kazi yetu kuhakikisha kuwa tunaowapa kazi wanafanya kazi.

Kwenye programu yao ya elimu kwa walipa kodi, Mamlaka ya Mapato Tanzania wanapaswa kujenga hoja siyo tu ya umuhimu wa kulipa kodi, lakini muhimu kabisa kuliko yote, ni kujenga hoja kuwa mlipa kodi anapaswa kuwa mkali sana na anapaswa kuchukua hatua dhidi ya udhaifu wa uwajibikaji na matumizi mabaya ya kodi.

Hatua hizi zitagawa kazi ya ufuatiliaji wa uwajibikaji wa majukumu ya uongozi kwa raia wengi zaidi na kuwapunguzia viongozi kazi ambayo hawapaswi kufanya peke yao, au hawapaswi kuifanya kabisa.

1763 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!