Fukuto kubwa limeanza ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bagamoyo, kutokana na baadhi ya wanachama kuhoji uhalali wa ukoo wa Kikwete kushika nafasi nyeti karibu zote katika Kamati ya Siasa ya wilaya hiyo.

Ukoo huo umehakikisha unashika nafasi zote za juu, ikiwamo ya Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya hiyo iliyokwenda kwa Shaibu Mtawa.


Mtawa alipata kura 811 na kumshinda Mohamed Mrisho Kikwete aliyepata kura 613. Mtawa na Mohamed wote ni ndugu wa damu wa Rais Kikwete.


Habari za uhakika kutoka miongoni mwa wanachama, zinasema majina ya wanandugu hao yalipendekezwa kutoka miongoni mwa wanachama 13. Wengi wao walikatwa kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa na kuhitimishwa kwenye vikao vya kitaifa ambavyo Mwenyekiti wake ni Rais Kikwete.


Katika ngazi hiyo ya Taifa, Mwenyekiti Kikwete alihakikisha majina matatu yanarejeshwa. Mawili – Shaibu na Mohamed –  yakiwa ni ya ndugu zake, na mwingine Omar Mhando.

 

“Mhando hapa aliwekwa kama msindikizaji kwa sababu kwenye raundi ya kwanza aliangushwa. Kwa kuwa hakuna mgombea aliyepata nusu ya kura, ikabidi upigaji kura urudiwe. Ikawa hivyo kwa kupigia majina mawili ya ndugu.

“Kilichofanyika kwenye uenyekiti ni kuhakikisha majina mawili ya wanandugu hawa yanaingia ili mmoja achaguliwe. Hilo limewezekana kwa kuchaguliwa Shaibu,” amesema mmoja wa wanachama.


Habari za uhakika zinasema kwamba kwenye uchaguzi huo kulikuwa na mvutano mkali kati ya wanandugu, hasa kutokana na ukweli kwamba Shaibu ni mdogo wa Katibu Msaidizi wa Rais Kikwete, Alhaji Kassim Mtawa.


“Mvutano ulikuwa mkali kweli kweli bila kujali kuwa waliokuwa wakigombea ni wanandugu, ulikuwa mchuano wa miamba,” kimesema chanzo chetu cha habari.


Baada ya uchaguzi huo, siku iliyofuata wanandugu walikutana katika kikao cha ukoo, kwa ajili ya kuzika tofauti zilizojitokeza miongoni mwao wakati wa uchaguzi.


Mohamed Kikwete anakaririwa kusema kwamba hakuwa na kinyongo kutokana na kushindwa na Mtawa.

 

“Aliyeshinda ni mdogo wangu, sina kinyongo,” alikaririwa akisema.

Baadaye kilifanyika kikao cha Halmashauri Kuu kwa ajili ya kumchagua Katibu Uenezi na Katibu wa Uchumi.


“Kabla ya uchaguzi, wapigakura kadhaa waliwekwa sawa, kuna kina mama walipata khanga, kina baba wakapata misuli na fedha za usafiri. Wajumbe walikuwa kama 140. Sikusikia aliyenung’unika kuwa amekosa kitu,” kimesema chanzo chetu.


Katika nafasi ya Katibu Uenezi, mshindi alikuwa ni ndugu mwingine kutoka ukoo huo huo wa Kikwete, aliyetajwa kwa jina la John Francis (Boli Zozo).


Kana kwamba hiyo haikutosha, nafasi ya Katibu Uchumi Wilaya ya Bagamoyo akachaguliwa Iddi Swala. Huyu ni mjukuu wa Rais Kikwete kwani amezaliwa na mtoto wa dadake Rais.


Ushindi wa Swala umezua gumzo kubwa hasa kutokana na namna alivyokuwa kiongozi ndani ya Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Wilaya ya Bagamoyo. Mgombea aliyetajwa kwa jina moja la Mtiga, aliyeelezwa kuwa na uwezo mkubwa wa uongozi, alishindwa.


Awali, ndugu mwingine wa Rais Kikwete aitwaye Yusuf Mrisho Kikwete, alishinda nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Kata ya Dunda, Bagamoyo.


Kuchaguliwa kwa wanaukoo hao, pamoja na kupita bila kupingwa kwa Ridhiwani Kikwete ambaye ni mtoto wa Rais Kikwete, kunaifanya Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Bagamoyo iwe na viongozi wakuu wanne ambao ni ndugu wa damu, pamoja na wajumbe wengine wa kawaida. Nafasi hizo ni Mwenyekiti, Mjumbe wa NEC Taifa, Katibu wa Uchumi na Katibu Uenezi.


Hata hivyo, kuwapo kwa wanandugu hao kungeweza kupanuka zaidi endapo nafasi ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake (UWT) Wilaya ya Bagamoyo, ingeshikwa na mwanaukoo mwingine wa Kikwete, Magreth Halfan Kikwete. Magreth kaolewa na mtoto wa Mzee Seleman Kikwete.


“Huyu wanachama wakasema haiwezekani, wakaamua kumbwaga maana ilishaonekana sasa chama kinakuwa cha ukoo tu. Tukaamua kumpa Hapsa Kilingo,” amesema mwanachama mwingine.


Kadhalika, ndugu mwingine wa Rais Kikwete, Mwanaisha Halfani Kikwete, alipitishwa kugombea Ujumbe Baraza Kuu/Halmashauri Kuu ya UWT Mkoa wa Pwani.

 

Wakati hali ikiwa hivyo kwenye uchaguzi huu unaoelekea ukingoni, mtoto mwingine wa Rais Kikwete, Khalfan Kikwete ni Mjumbe wa Baraza Kuu Idara ya Chipukizi ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM). Mwenyekiti wa Idara hiyo ni Gabriel Makalla – mtoto wa Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla.

Ushindi wa Ridhiwani, Mama Salma

Kitendo cha Ridhiwani kupita bila kupingwa kumeacha maswali mengi. Kuna habari kutoka kwa baadhi ya wanachama kwamba wale waliothubutu kujitokeza kuwania nafasi hiyo walitishwa, na wao wakatishika.


Wapo wanaosema kwamba kupita kwake kwa mbinu hiyo kulitokana na hofu ya wajumbe kutokana na ukaribu alionao na mzazi wake, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Taifa.

 

Ni woga kama huo uliowaingia pia wanachama na wapenzi wa CCM katika Wilaya ya Lindi Mjini, walioamua kusalimu amri na kushuhudia mke wa Rais Kikwete, Mama Salma, akipita bila kupingwa.

Ridhiwani na ubunge 2015

Watu walio karibu na kijana huyo wanasema kwamba anajiandaa kugombea ubunge Jimbo la Bagamoyo mwaka 2015.


Wanaotoa madai hayo wanatetea hoja yao kwa kigezo cha namna Kamati ya Wilaya ilivyosukwa kwa kuwa na viongozi wakuu ambao karibu wote ni ukoo mmoja. Wachunguzi wa mambo wanasema matumaini ya Mbunge wa sasa wa Bagamoyo, Dk. Shukuru Kawambwa, kuwania nafasi hiyo mwaka 2015 yamefutwa kutokana na kundi lake kushindwa vibaya katika ngazi karibu zote.


Kwa sasa Dk. Kawambwa ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

 

Jambo jingine ambalo JAMHURI haijalithibitisha ni kwamba suala la ukabila nalo limekuwa likitawala kwenye uchaguzi wilayani Bagamoyo, kama ilivyo kwenye uchaguzi wa CCM katika maeneo mbalimbali nchini.


Dhambi hiyo ndiyo inayomfanya Dk. Kawambwa sasa aonekane kuwa ‘wa kuja” asiyetakiwa na “wazawa”.

Mbona hata Nyerere alipendelea?

Kuna hoja zinazojadiliwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, naye alipendelea ndugu zake wakati akiwa katika uongozi.

 

Anatajwa Joseph Warioba Butiku, aliyekuwa Katibu Myeka wa kiongozi huyo, kama kielelezo cha Mwalimu kuwabeba ndugu.


Pia anatajwa Joseph Nyerere, ambaye ni tumbo moja na Mwalimu, aliyepata kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa muda usiozidi miaka miwili; na pia Katibu wa Umoja wa Vijana wa TANU.


Baadaye, kuanzia miaka ya 1970 hadi kifo chake miaka ya 1990, Joseph alikuwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Butiama.


Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali David Musuguri, naye anatajwa kama mmoja wa waliopendelewa na Mwalimu, ingawa kumbukumbu zinaonesha kuwa Janerali huyo alijiunga katika Jeshi la Kikoloni la KAR kabla ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia (1939-1945).


By Jamhuri