Na FX Mbenna
BRIG GEN (MST)

 
Kuna tofauti kubwa kati ya maneno haya mawili – uraia na uzalendo. Hapa nchini Tanzania upo mkanganyiko mkubwa wa utumiaji usio sahihi wa maneno mbalimbali.
 Baadhi yetu tunaona neno uraia ni sawa tu na neno uzalendo, hivyo maneno haya yanaweza kutumika kama vile yote mawili yana maana ile ile, hivyo yako kisawe (synonymous). Hii siyo sahihi, ni mazoea potofu kutumia maneno haya kama vile ni kisawe.


  Nasema hivi kwa sababu sisi Waswahili wa Tanzania tumezoea kuchanganya matumizi ya baadhi ya maneno mathalani maneno sahihi na saini. Inakubalika kuwa maneno yote mawili hayo yana maana ileile yaani yako kisawe, kumbe sivyo.
 Ukweli, Kiswahili fasaha kinatuambia wazi maneno uraia na uzalendo siyo kisawe na yana maana tofauti kabisa. Hali kadhalika maneno SAHIHI na SAINI yako tofauti kabisa. Basi kwa kujichanganya namna hiyo Kiswahili chetu, tunakichafua, inabidi kupambanua tofauti kati ya maneno namna hiyo na hapo tutapaswa kuyatumia vilivyo kwa usahihi wake wa maana ya maneno na siyo kwa mazoea yaliyopo. Tungejua sarufi vizuri kama tulivyojifunza sisi kwa kutumia kitabu kile cha 'Broomfield' cha zamani, leo Kiswahili kisingeborongwa.


  Mathalani neno sahihi linamaanisha urekebisho, usahihisho na kwa hiyo halipaswi kutumika kama mahali pa kucharaza ufupisho wa jina lako.


Ufupisho au mkato huo wa jina la mtu unaitwa SAINI kuonesha alama mtu ameibuni kuwa ni kifupisho. Alama au kifupisho namna hiyo cha jina la mtu wenzetu wanaita “SIGNATURE” ndipo Kiswahili ikakubalika na iliyokuwa East African Territorial Language (SWAHILI) Committee iitwe SAINI.
 

Sasa kwa uamuzi ule basi usahihi wa maneno saini kamwe haiwezi kutumika kama sahihisho au rekebisho, ni maana mbili tofauti. Lakini kwa mazoea yetu hapa nchini hata ofisi za Serikali zinachapisha fomu mbalimbali na kuandika neno SAHIHI yako……………. hapa.
Hii mimi naona siyo sahihi, walipaswa waandike SAINI yako………………Hapa.


  Mazoea hayo sasa yamekuwa kawaida kwa neno sahihi kutumika mahali pa kubandika alama fupi ya jina la mtu. Neno saini limeyeyuka kabisa.
  Tunakuja kwenye mada yangu ya leo maneno URAIA na UZALENDO. Nionavyo mimi yanatumika visivyo katika nchi yetu. Watu wanayachanganya. Neno RAIA linamaanisha mtu aliyezaliwa katika nchi ile au ni kundi zima la watu/wananchi waliozaliwa katika sehemu moja katika ulimwengu huu.
  Mathalani sisi wananchi hapa kwetu, tulipotawaliwa tulijulikana kama raia wa Uingereza. Desemba 9, 1961 usiku wa manane kwa mara moja sote tukawa RAIA wa TANGANYIKA saa 6 usiku. Mwaka 1964 usiku wa kuamkia Aprili 26, wana wa nchi hii kwa mara moja tukageuka na kuwa RAIA wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 

Hapa inaonekana wazi uraia ni kwa kila mzaliwa wa mahali/nchi alipo hapa duniani. Ni hali timilifu na kamilifu anayostahili kila mwananchi kuwa nayo.
  Siku tulipopata Uhuru wetu sisi Watanganyika Desemba 9, 1961 Mwalimu Julius Nyerere alipowahutubia wananchi wa Taifa hili huru, alitamka maneno haya, “…Wakati wote TANU ilipokuwa inapigania Uhuru tumekuwa tukieleza ilivyo muhimu, usawa na utu wa binadamu ipasavyo kuheshimiwa na vile vile tumekuwa tukieleza Hati ya Haki za binadamu. Tumeafikiana kwamba Taifa letu litakuwa Taifa la watu huru na wenye URAIA sawa, kila mtu akiwa na haki sawa na mwingine…. Tumesema kuwa mtu hawezi kunyang'anywa haki ama usawa wa URAIA wake katika Taifa letu kwa ajili ya dini yake, ufundi au kitu chochote….” (gazeti la Uhuru toleo No. 1 la Desemba 09, 1961) ukurasa wa mbele).
 

Si hivyo tu bali hata katika ile KATIBA yetu ya kwanza iliyoandikwa Lancaster House, na ndiyo tuliyotumia wakati tunapata Uhuru ilitamka vizuri kabisa juu ya uraia na raia wa nchi hii. Kwa vile Katiba ile iliandikwa kwa lugha ya watawala yaani Kiingereza, nami sina utaalamu wa kuitafsiri vilivyo kisheria naomba hapa ninukuu vifungu vichache vile vinavyotamka juu ya URAIA.
Ninanukuu CHAPTER: I CITIZENSHIP: Persons who become citizens on 9th December, 1961: 1 – (1) Every person who, having been born in Tanganyika, is on the eighth day of December, 1961 a citizen of the United Kingdom and colonies or a British protected person shall become a CITIZEN OF TANGANYIKA on the ninth day of December, 1961 a citizen of the United Kingdom and colonies or a British protected person shall become a citizen of Tanganyika on the ninth day of December, 1961.
  Aina za uraia zilizotafsiriwa katika vifungu vinginevyo vya Katiba ile vilikuwa 1 – (2); 2 -(1) – (5) mpaka kifungu cha 6 chenye kuelezea uraia wa nchi zaidi ya moja (dual citizenship). Sikutaka kunakili vifungu vile vingine vyote.
 Katika masuala ya uraia, baada ya ule Muungano wa nchi hizi mbili Katiba ilikuwa wazi. Katika Appendix J, Union of Tanganyika and Zanzibar 1964 kuna makubaliano yanayojulikana kama ARTICLES OF UNION kati ya Tanganyika na Zanzibar.


  Basi mle iliandikwa hivi katika vifungu (v) The existing laws of Tanganyika and Zanzibar shall remain in force in their respective territories subject to………… kwa makubaliano hayo uraia tafsiri yake ilibaki kama ilivyoainishwa katika Katiba za nchi hizi mbili.
  Lakini neno hili uraia lina maana nyingine pia na pana kidogo. Uraia pengine linatumika katika somo la elimu kuelezea jumuiya ya watu na nchi yao, Serikali yao, shughuli zao katika jamii husika na mamlaka mbalimbali zinazoshughulikia hiyo jamii na kadhalika.
  Somo hili ni pana, linaelezea mgawanyo wa madaraka kikatiba ya nchi kwa vyombo mbalimbali kama, Utawala (Executive) Bunge (Parliament) na Mahakama (Judiciary).


 Somo linajumuisha kazi na wajibu za wananchi katika Taifa zima. Hivyo neno uraia kamwe haliwezi kutumika badala ya lile neno UZALENDO kwa namna yoyote ile wala hali yoyote ile.
  Sasa UZALENDO basi ni nini? Kwa mara ya kwanza katika nchi yetu wageni (wakoloni) walitumia neno hili uzalendo enzi ya Wajerumani. Wao katika kuhimiza elimu walitamka kama moja ya shabaha zao katika elimu ilikuwa kuamsha moyo wa uzalendo ndipo walitumia maneno haya: Nanukuu “To inculcate…… a sound knowledge of German customs and patriotism”.


  Hii ilitangazwa na watawala wa Ujerumani mwaka 1903 ndipo neno patriotism yaani uzalendo lilipowafikia Watanganyika. Sasa neno hilo lina maana moja tu katika kamusi ya Kiingereza – Kiswahili “PATRIOTISM” maana yake UZALENDO ni TABIA ya mtu kuipenda sana nchi yake na hata kufia nchi yake hiyo.
  Sasa si kila raia katika nchi au katika Taifa anaweza kuwa mzalendo. Hii ni tabia au moyo wa mapendo makubwa sana kwa nchi yake mtu.


Wajerumani waliposema kufunza wananchi wa koloni lao la Tanganyika mila na desturi za Ujerumani hasa walinuia kuwafunza watoto wa nchi hii kuwa na moyo wa kuipenda nchi yao hao Wajerumani kwa dhati kabisa.   Mzalendo kamwe hathubutu kusaliti nchi bali atajitahidi kuijenga, kuilinda na kuitumikia kwa uaminifu hadi kufa kwa ajili ya nchi yake hiyo.
  Watanzania tangu baada ya Uhuru, Baba wa Taifa alijua mila na desturi za makabila mbalimbali humu nchini. Kila kabila linayo namna ya kufunda watoto wake katika manyata au majando ya kikabila. Humo watoto wa kabila moja wanalelewa kwa pamoja wana maisha ya jamii kwa pamoja na wanarithishwa mapokeo muhimu ya makabila na hasa namna ya kujilinda.


  Sasa Mwalimu akabuni mahali pa kuwafunda watoto wote wa Taifa hili jipya moyo wa kufanya kazi pamoja, moyo wa kulinda Taifa hili pamoja na moyo wa kuzalisha mali pamoja kitaifa. Ndipo pale ulipobuniwa mpango wa HUDUMA KWA TAIFA – tukaita “National Service”.
  Hapo peke yake palikuwa mahali pa kuwafunda watoto wote wa nchi hii UZALENDO. Watoto wa nchi tayari wamezaliwa na kukuwa raia wa Tanganyika lakini hawakuwa WAZALENDO. Makambi yaliandaliwa kuwa majando ya kitaifa kuwafunda watoto wa Taifa zima UZALENDO.
  Katiba ile ya Tanganyika ya 1961 tuliyopatia uhuru, ilikuwa na maneno ya utangulizi kutoka kwa Mwalimu Nyerere yaliyosomeka hivi: namnukuu, “in particular I trust that the young will take particular note of the preamble, where they will find those high ideals by which one country should always seek to direct itself. The concepts of LIBERTY, OF EQUAL RIGHTS FOR ALL, of an INDEPENDENT JUDICIARY, should inculcate into the youth of Tanganyika from the earliest possible stage. It is the duty of all of us to see that these IDEALS become truly a part of our national life, and not mere catchwords and slogans of no significance” (JK Nyerere Prime Minister – 1961).


  Imenilazimu kunukuu utangulizi huo karibu wote kwa vile nimeshindwa kuutafsiri kisheria maana sahihi ya maneno haya. Lakini la msingi hapa ni kwamba katika Katiba iliyotupatia Uhuru Mwalimu alihimiza vijana kuitafakari kwa kina maudhui yake.
  Mle kuna malengo, kuna mahimizo na kuna miito (slogan) na vidahizo (catchwords) vya  kuwasisimua vijana kutafakari hali ya baadaye ya Watanganyika.


  Katiba imesema juu ya haki sawa, imetoa mawazo au dhana (ideals) za Uhuru wa watu, haki na wajibu za watu na Uhuru wa Mahakama.
La msingi vijana watafsiri hayo kwa manufaa ya wote na ndipo akamalizia kuhimiza wajibu wa kila mmoja wetu kuandaa mazingira ya maisha bora ya kitaifa kwa wananchi wote. Vijana wale wa miaka ile ya 61 ndio wazee wa leo hii.
 
Itaendelea

 

4677 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!