Rais Jakaya Kikwete ameshachoka. Huhitaji kuwa mnajimu kulijua au kuliona hilo.
Mwaka jana akiwa ughaibuni, mbele ya viongozi wengine wa Afrika na dunia, hakusita kuwathibitishia kuwa kachoka. Akasema anasubiri kwa hamu muda wake wa kung’atuka uwadie arejee kijijini kuendelea na maisha ya kawaida.
Alimradi mwenyewe keshatuthibitishia kuwa kachoka, tulichobaki nacho ni kuushuhudia huo uchovu wake.


Mwaka jana watu zaidi ya 40 walifariki dunia katika ajali iliyohusisha mabasi mawili Butiama mkoani Mara. Kama ilivyotarajiwa, si Rais, Makamu wa Rais wala Waziri Mkuu aliyeguswa moja kwa moja na vifo hivyo. Sana sana wakubwa hao wakaona msiba huo ni saizi ya aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe.
Mzimu wa ajali umeendelea kulikumba Taifa letu. Wamekufa watu wengi mno katika ajali mbalimbali za barabarani nchini kote. Funga kazi imekuwa hii ya wiki kadhaa zilizopita ambako watu 52 walifariki dunia mkoani Iringa.


Kama ilivyo ada, Ikulu ikaandika mistari inayohesabika ya maneno tuliyoaminishwa kuwa ni rambirambi kutoka kwa Rais Kikwete mwenyewe. Maneno hayo hayakukosa chachandu ile ile ya siku zote ya: “Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana kufuatia (kutokana na) taarifa za vifo vya watu zaidi ya 40 huku wengine kadhaa wakijeruhiwa katika ajali hii mbaya ambayo imesababisha simanzi na majonzi makubwa kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu.”


Taarifa ya Ikulu ikaongeza hitimisho kwa kusema: “Katika Salamu zake hizo, Rais Kikwete amewahakikishia wafiwa wote kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba wa ndugu na jamaa zao, lakini amesema, pamoja na machungu yote ya kupotelewa na ndugu na jamaa zao, anawaomba wafiwa wawe na moyo wa uvumilivu na subira wakati huu wanapoomboleza vifo vya wapendwa wao.”
Tamko hili ni jepesi mno. Halilingani na uzito wa msiba na mamlaka iliyolitoa. Kama hitimisho la Ikulu kwenye tatizo hili ni la kuwataka ndugu wawe na subira, na mwisho kuwaombea marehemu na majeruhi, basi hatuhitaji ushahidi mwingine wa kutufanya tuamini kuwa miaka 10 imeshamchosha Rais wetu na wasaidizi wake.


Kabla ya kuendelea, nirejee kidogo kwenye ajali zilizotikisa nchi mwaka jana. Aprili 21mkoani Simiyu walikufa watu 11 katika ajali. Julai 30, katika eneo la Pandambili mkoani Dodoma, roho za Watanzania wenzetu 18 zilipotea. Agosti 29 watu 10 walikufa katika ajali iliyotokea Mbalizi mkoani Mbeya. Oktoba 30 watu 12 walifariki dunia katika ajali iliyotokea mkoani Arusha; na Novemba 27 roho za Watanzania 11 zilipotea katika eneo la Mkanyageni, Tanga. Ukijumlisha na ile ya mkoani Mara utaona kuwa ajali nane pekee za mabasi ziliua watu 173!


Ndugu zangu, roho za watu 173 kupotea kwenye ajali nane, katika nchi yenye watu wenye vichwa vinavyounda maswali na kutafuta majawabu, lazima sote kama Taifa tungeshituka. Wananchi hawaonyeshi kushituka pengine kwa sababu hata Ikulu yenyewe imeshaona ajali hizi ni mambo ya kawaida tu.
Hata waandishi wa habari nao wameshakata tamaa. Hili linathibitishwa na baadhi ya magazeti kuzipa habari za vifo vya ajali umuhimu mdogo kuliko zile za mtifuano wa urais au kulishana sumu kunakodaiwa kufanywa na baadhi ya wanasiasa.
Pengine nirejee kwenye msiba huu wa juzi uliochukua roho za Watanzania 52. Pamoja na ukweli kwamba Ikulu haiendeshi wala kukagua magari, linapotokea janga kubwa la kitaifa la aina hii haiwezi kukwepa lawama.


Nimesoma karibu salaam za rambirambi zote ambazo Ikulu imekuwa ikizitoa pindi ajali mbaya zinapotokea kama hizi nilizozitaja hapo juu. Ukizipitia vema salaam hizo utaona kinachofanywa sasa na Ikulu ni ku-copy na ku-paste. Kwa namna rambirambi hizo zinavyoandikwa ni kama vile kuna ukurasa maalumu wa ajali uliokwishaandaliwa na pindi inapotokea, basi kinachoingizwa kwenye ukurasa huo ni mahali ilikotokea ajali, tarehe, idadi ya waliokufa na anayepelekewa hizo salaam za rambirambi.


Nasema hivyo kwa sababu haiwezekani Ikulu ikatoka tamko jepesi kama hili la kufariki dunia kwa watu 52 kana kwamba waliokufa ni mbuzi. Naamini hata wangekuwa ni nyumbu 52 waliouawa, bado tamko lingekuwa zito. Lingekuwa zito kwa sababu nyumbu wanasaidia kuingiza fedha kupitia kwa watalii!
Ikulu yenyewe inaonyesha wazi haiguswi na ajali hizi; na kwa sababu hiyo ndio maana hatuoni lugha ya karipio la kiutawala wala kuwajibika kwa watu wanaopaswa kuwajibika.


Rais wetu amechoka kiasi kwamba hata kufika eneo la tukio ili kuona mahali ambako wapigakura wake wamefia, hana uwezo tena. Lakini ni Rais huyu huyu ambaye mara nyingi tu barabara zimefungwa ili kumpa fursa ya kwenda kuhani na hata kushiriki mazishi ya wasanii. Inapotokea msanii mmoja akawa na maana sana hata msiba wake ukaweza kukwamisha shughuli nyingine, lakini roho za watu 52 zikawa hazina umuhimu; nadhani hapo sitakuwa nje ya mstari wa adabu nikisema Rais haguswi na misiba hii ya mabakwela wasiokuwa na majina makubwa.


Hivi karibuni nchini Ufaransa kumetokea matukio ya kigaidi yaliyogharimu uhai wa watu 15 hivi. Serikali ya nchi hiyo kwa kuthamini uhai wa raia wake, ikatangaza siku kadhaa za maombolezo kitaifa. Ulaya nzima ikazizima. Viongozi wakubwa kutoka mataifa mbalimbali wakaonyesha mshikamano.
Fikiria, watu 15 wanatangaziwa siku maalum za kuwaomboleza! Sisi hapa watu 52 wanakufa katika ajali hakuna siku ya maombolezo wala kushusha bendera nusu mlingoti. Siku ya maombolezo inaweza kutangazwa wakati huo huo wananchi wakiendelea na kazi zao za ofisini, mashambani, biashara na viwandani kama kawaida. Bendera inaweza kupepea nusu mlingoti bila kuathiri kitu chochote.


Kufanya hivyo kuna faida zake kadhaa, lakini kubwa zinaweza kuwa hizi: Mosi, kuwaonyesha ndugu na jamaa wa wafiwa kuwa Watanzania wenzao tu pamoja nao. Pili, ni kuonyesha kuwa tunajali na kuthamini maisha ya kila Mtanzania; na Tatu, ni kuonyesha kuwa sisi kama Taifa, kupitia Serikali yetu, tuna dhamira ya kweli ya kupambana na hatimaye kutokomeza jinamizi hili la ajali za barabarani.


Rais anapotangaza siku ya maomboleo kwa tukio la aina hii anapeleka salaam maridhawa kabisa kwa watu wenye kuhusika na usalama wa abiria kwamba amenuia kuhakikisha ajali zinakomeshwa. Anaonyesha kujali maisha ya wananchi wake. Anakuwa ameonyesha kuguswa na tukio hilo.
Lakini inapotokea Ikulu ikaishia kuwaombea “moyo wa subira” watu waliofiwa na ndugu, jamaa na marafiki zao; na kuwaombea marehemu walale mapali pema peponi; hapo ni kuwaambia kuwa Serikali haina jingine la kufanya, isipokuwa kukubaliana na matokeo ya ajali!
Serikali yenye uchungu na watu wake, eneo ambako roho za watu 52 zimepotea inaweza kuweka mnara wa kumbukumbu ili iwe alama kwa vizazi vinavyo kuwa suala la ajali linapaswa kudhibitiwa.


Kwanini kusijengwe mnara? Hakujengwi mnara kwa sababu Ikulu inajua ikiruhusu hilo, kila mita ya barabara itakuwa na mnara! Itakuwa na mnara kwa sababu ajali ni nyingi na yenyewe (Serikali) haina mpango au imeshinfwa kuzidhibiti. Ilivyo sasa ni kama inasema haitakuwa na bajeti ya kutosheleza ujenzi wa minara maana ajali ni nyingi!
Rais Yoweri Museveni wa Uganda alipoona madereva wa daladala nchini mwake hawataki kutii sheria za usalama barabarani, akaamuru wacharazwe bakora hadharani. Uamuzi huo ukaonekana ni udikteta, lakini ukweli ni kwamba umesaidia kuwanyoosha madereva nchini humo.
Hapa kwetu sipendekezi utaratibu huo, lakini kama upunguzaji ajali kwa njia nyingine umeshindikana, kwanini hilo lisifanyike kwetu pia?


Zipo sababu nyingi zinazotajwa kwamba ndiyo chanzo cha ajali nyingi. Mathalani, ulevi, uzembe wa madereva na watumiaji wengine wa barabara, uchakavu wa magari na hata barabara zenyewe; wingi wa malori na kadhalika. Matatizo yote haya mzizi wake unatajwa kuwa ni rushwa.
Kwa mfano, upo ushahidi usiotiliwa shaka kuwa baadhi ya madereva wa mabasi, malori na magari madogo wanapata leseni wakiwa hawajui kuendesha vyombo hivyo. Wanajifunza wakiwa tayari wameshakabidhiwa vyombo na leseni. Hapo trafiki hawakwepi lawama.


Wingi wa malori barabarani ni sababu nyingine kubwa. Ukweli ni kwamba malori yamezidi. Njia pakee ya kukabiliana na hali hii ni kuimarisha reli na usafiri wa majini. Kuna athari za kiusalama na kiuchumi kuona nondo, saruji na mizigo mingine mizito ikisafirishwa kwa kutumia barabara. Rais ajaye aiweke reli kwenye vipaumbele vyake.
Pia sheria za usalama barabarani zibadilishwe. Ziongewe makali.


Lakini kubwa kuliko mengine, nadhani ni kuhakikisha kuna uwajibikaji. Wengi tunaamini kuwa ajali kama hii iliyoua watu 52 ikitumika kumfanya waziri mwenye dhamana au Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani wajiuzulu, watakaoziba nafasi zao watahakikisha wanafanya kila linalowezekana kukomesha maafa haya.
Ajali za barabarani si matukio ya asili kama ilivyo mvua, kimbuga au matetemeko ya ardhi. Ajali hizi ni matukio ya kibinadamu ambayo wahusika wanaopaswa kuyadhibiti wanaposhindwa kutekeleza wajibu wao, sharti wang’oke.


Sijui afe nani ili kuifanya Ikulu itambue kuwa ajali hizi ni janga la kitaifa ambalo linapaswa kupatiwa ufumbuzi wa kudumu. Afe nani mwingine maana tayari ajali ilishatuulia Waziri Mkuu wetu kipenzi, Edward Moringe Sokoine.


Mawaziri wenye dhamana, mapolisi na wengine wenye dhamana na usafiri huu wamebaini kuwa Rais wetu kachoka, na kwa sababu hiyo wanajua hawezi kuchukua hatua zozote dhidi yao zaidi ya kutoa ‘mkwara’ unaoishia kwenye salaam za rambirambi.
Ukisoma salaam za rambirambi za Ikulu unatambua kuwa kweli Rais Kikwete amechoka. Kama mwenye Ikulu kachoka, huyo Kamanda Mpinga atafaa nini? Hapo ndipo Watanzania tulipofikishwa.

2175 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!