Kuna wakati nahisi kuwa kama kichaa maana nafikiria vitu ambavyo ni kama mbingu na ardhi, haiwezekani kutokea katika ulimwengu wenye fatiki kali za kisiasa na kiuchumi.


  Haziwezekani kwa sababu kuna mambo ya uanachama na kujulikana, haiwezekani kwa sababu kuna masuala yaliyopitishwa kisheria ili mgombea wa kiti cha urais aweze kupata nafasi hiyo.
  Nafikiria kuchukua fomu ya uanachama wa chama chochote kile iwe kikongwe au hata kipya kitakachoanzishwa muda wowote kwa ajili ya uchaguzi, nafikiria kuchukua fomu ya kugombea urais kupitia chama changu, hivyo kuna shughuli kwanza ya kujulikana ndani ya chama na kisha kwa wapigakura.


  Kila mahali naona kuna tatizo, lakini ya Mungu mengi huko kote naweza nikapita kwa sera zangu, lakini muziki mzito naweza kuupata kutoka kwa wananchi kunipa ridhaa yao ya kuongoza nchi. Hapa si tu kujulikana bali kuna tatizo la wapiga kura kununuliwa kutokana na ugumu wa maisha yanayowakabili, Mungu wasamehe kwa kuwa hawajui walitendalo na hukumu yake ndiyo hii ambayo wengi wao wanajutia huko kwenye vitongoji.


  Mimi nina sera zangu, siyo nyingi lakini kwangu naona zina kipaumbele chake. Awamu iliyopita, moja kati ya sera nyingi ilizokuwa nazo ni ujenzi wa miundombinu ya usafiri, kwa hili tumwogope Mwenyezi Mungu kuliona kama halijafanyika, na hakuna maendeleo yoyote yanayoweza kupatikana bila kuwa na miundombinu bora ya usafirishaji.
  Mimi nataka kugombea urais safari hii, lakini sijui kama nitaweza kupata nafasi iwapo nitashindwa basi mtu anaweza kudesa sera zangu, ninanzo nyingi kubwa na ndogo na ninaziweka hadharani ili mwenye kudesa iwe ni kwa faida ya wote pamoja na mimi.


  Nitaanza kazi na PCCB, ikiwezekana hata kubadili mfumo wa ufanyaji kazi, hawa ndiyo chanzo cha matatizo yote nchini, nitaweka chombo hiki nje ya mfumo wa serikali yangu kiwe ni chombo kinachojitegemea.
  Sitawapa mishahara, lakini nitataka wajitegemee kwa kukamata rushwa na wao wakapata pasenti, hii ni ngumu kueleweka, wapo watakaodhani kwamba sasa nitaruhusu na wao wawe wanavuta kitu kidogo, itakuwapo PCCB ndani ya PCCB.
  Nchi yoyote iliyogubikwa kwa rushwa hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana, nchi hiyo itatawaliwa na nguvu ya wenye nacho, nchi hiyo itakuwa si huru tena bali koloni la mtu mwenye fedha.  


  Nitatumia chombo hicho kurudishia heshima serikali, serikali lazima iogopwe na watu wasitwae  madaraka kutokana na nguvu ya fedha na hasa hasa kama fedha hizo zinatokana na rushwa.
  Nitajikita zaidi katika elimu, nitasimamia uhuru wa watoa elimu nchini, sitageuza kuwa huduma huru kama ilivyo sasa, kwamba kutokana na serikali yangu kushindwa kuhimili idadi ya watoto kuwa shule ndiyo iwe kigezo cha wengine wenye fedha kuanzisha shule na kujipangia ada watakavyo, hilo sitaruhusu kwa kuwa elimu siyo starehe bali ni kitu cha lazima, lakini pia nitasimamia mitaala ili watoto wa Kitanzania wapate elimu ya Kitanzania.


 Nitabadilisha mfumo wa uwajibikaji serikalini na serikali za mitaa, kwani huko kuna miungu watu wanaofikiria kuwa wakiajiriwa serikalini ndiyo kama vile wamepata shamba la kuvuna bila kupanda, nitafuatilia mapato ya kila mtumishi na mali anayomiliki kama vina uhusiano, kinyume na hivyo nitarudisha azimio lile lililotenguliwa na wajanja wachache ili waweze kujinufaisha.


  Nitaimarisha demokrasia ili uwe uwanja wa kupata ndogo ndogo za wahujumu uchumi, mafisadi na wapokea rushwa kubwa na ndogo, nitajenga mazingira ya kila Mtanzania kuwa mzalendo wa kufichua maovu ndani ya jamii yetu iliyoparaganyika kutokana na kukata tamaa ya maisha. Hii itakuwa ni ajenda endelevu ili kujenga utamaduni wa kuheshimiana.  


  Nitakusanya kodi kwa nguvu zote, kodi ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa lolote, kodi itaimarisha huduma za jamii ili Watanzania walionipigia kura waweze kupata huduma ya kisasa katika masuala ya afya na jamii, masuala ya elimu, maji salama na safi kwa kila Mtanzani na huduma za umeme kila mahali, hii ni haki ya msingi kwa kila mwananchi anayelipa kodi. Katika hili sitakuwa na huruma hata kwa mke wangu kama anafanya biashara.


  Yapo mengi ambayo nitayafanya, leo nimeanza na haya na wiki ijayo nitaendelea na sera zangu lakini mwisho wa sera nitataka kundi la kunichukulia fomu ya urais ili niweze kutekeleza sera zangu, suala la kujuana na urafiki hapa ni mbingu na ardhi, cha msingi ni uwajibikaji kama ule wa miaka ile ya Julius.
 
Wasalaam,
Mzee Zuzu,
Kipatimo.

By Jamhuri