Moscow, Russia

Na Mwandishi wetu

Vita ya maneno inazidi kupamba moto baina ya mataifa tajiri duniani yakigombea mipaka ya taifa la Ukraine.

Hali hiyo imezuka baada ya Urusi kuzidisha vikosi vyake vya kijeshi kwenye mipaka ya taifa hilo, jambo ambalo limewaibua Marekani na Umoja wa Ulaya wakilaani kitendo hicho.

Wakati ikilalamikiwa kwa hatua hiyo, yenyewe inajitetea kwa kueleza kwamba kuanzisha kambi za vikosi vya kijeshi karibu na mipaka ya taifa hilo ni kujihami dhidi ya vitisho vya Marekani, Umoja wa Ulaya na vikosi vya majeshi ya NATO.

Msemaji wa taifa hilo, Dmitry Peskov, amekanusha taarifa za uvamizi akisema kwamba zinakuzwa na vyombo vya habari vya mataifa ya Magharibi na kwamba wao hawana mpango wa kuivamia kijeshi Ukraine.

‘‘Huu ni mpango wa kuogopesha na jaribio la kututisha. Urusi haimtishi mtu yeyote, harakati za vikosi vyetu kwenye mipaka yetu haipaswi kuwa mjadala kwa watu wengine,” amesema Peskov.

Taifa la Ukraine limekuwa likilalamika kuwa Urusi imezidi kuweka maelfu ya wanajeshi karibu na mipaka yake na kwamba hatua hiyo inalenga kuongeza mashinikizo kwake kama ambavyo imekuwa ikifanya kwa mataifa yaliyowahi kuwa mshirika wa umoja wao, nchi za Kisovieti.

Aidha, hatua hiyo inafananishwa na kile kilichotokea mwaka 2014 baada ya kuzuka kwa machafuko baina ya vikosi vya upande wa mashariki vilivyojitenga na Serikali ya Ukraine, Urusi ikaamua kushiriki machafuko hayo kwa kuvipa nguvu vikafanikiwa kuichukua rasi ya Crimea ya taifa hilo.

Waziri wa Ulinzi wa Ukraine amekaririwa akisema kuwa takriban vikosi 90,000 vya kijeshi vya Urusi vimewekwa karibu na mipaka ya taifa hilo, hasa kwenye eneo la mashariki mwa nchi hiyo ambalo limekaliwa na vikundi vyilivyojitenga dhidi ya serikali.

Mkuu wa majeshi wa taifa hilo, Luteni Jenerali Valeriy Zaluzhny, anasema Urusi imeingiza maofisa wa kijeshi takriban 2,100 katika vikosi vya waasi na kwamba maofisa hao ndio wanaoviongoza katika kuendeleza uasi nchini humo.

Kitendo hicho kinadaiwa kusababisha watu 14, 000 kupoteza maisha mashariki mwa taifa la Ukraine lakini Serikali ya Urusi imekuwa ikikanusha taarifa hizo.

Katibu Mkuu wa Serikali ya Marekani, Antony Blinken, amemhakikishia Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Dmytro Kuleba, kwamba suala la ulinzi wa mipaka ya taifa la Ukraine limo mikononi mwa Marekani.

Blinken ameinyooshea kidole Urusi dhidi ya matumizi ya nguvu za kijeshi katika mipaka ya Ukraine na kuahidi kwamba endapo itaendeleza ubabe huo Marekani haitasita kuingilia kati mgogoro huo.

‘‘Hatujui makusudi ya Urusi lakini tunayo historia ya kilichotokea siku za nyuma, Urusi iliweka majeshi yake kwenye mipaka ya Ukraine na kuanzisha migogoro. 

‘‘Hicho ndicho inalenga hata sasa na ndicho kilifanyika mwaka 2014,” amesema Blinken huku akiahidi kwamba wamo kwenye mazungumzo na washirika wao wa mataifa ya Ulaya kuhusu hatua za kuchukua dhidi ya ubabe wa Urusi.

Balozi wa Urusi katika Baraza la Umoja wa Mataifa, Dmitry Polyansky, ameulizwa kama Urusi inajiandaa kuivamia Ukraine, ambapo amejibu kuwa taifa hilo halijawahi, halina mpango, na halitatekeleza mpango huo.

Taarifa hizo amesema zinazushwa na taifa la Ukraine kwa lengo la vitisho na manyanyaso yanayochochewa na Marekani, ambayo kwa sasa imeweka meli zake za kivita katika Bahari Nyeusi iliyopo karibu na mataifa hayo mawili.

Kwa upande wake Peskov, amesisitiza kuwa Urusi inahitaji kuilinda mipaka yake kutokana na Marekani pamoja na washirika wake kuweka vikosi vya wanamaji katika bahari hiyo.

Kwa upande mwingine anasema Urusi inalenga kukomesha matukio ya kiintelijensia yanayoongozwa na NATO  karibu na mipaka yake.

‘‘Tunachukua hatua madhubuti kujihakikishia ulinzi wetu pale tunapoona mpinzani wetu anajiimarisha karibu na mipaka yetu. Hatuwezi kuwa tofauti katika hilo. Ni lazima tujilinde,” anasema Peskov.

Naye Waziri wa Ulinzi wa Urusi anasema kitendo cha Marekani kuruhusu meli zake za kivita kuingia  Bahari Nyeusi  kinasababisha vitisho vya kiusalama katika maeneo yao.

Nao Umoja wa  Ulaya kupitia Rais wake, Ursula Von der Leyen, wakati akizungumza na Rais wa Marekani, Joe Biden, kuhusu mgogoro huo anasema umoja huo unaiunga mkono Ukraine katika kupinga mipaka yake kuvamiwa.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ufaransa, Jean- Yves Drian, na Waziri wa Ulinzi, Florence Parly wote kwa pamoja wameionya Urusi kwamba vitendo vyake vitazua machafuko na kuiharibu mipaka ya Ukraine.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, ameahidi kuzungumza na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, siku zijazo kuhusu hali ya usalama ya Ukraine na Belarus.

Chanzo: ABC News

By Jamhuri