Usajili wachezaji wa kigeni uzingatie vigezo

NA MICHAEL SARUNGI
Usajili wa wachezaji wa kigeni usiozingatia vigezo vinavyotakiwa umesababisha
klabu nyingi zinazocheza Ligi ya Vodacom Tanzania Bara kujikuta zikisajili
wachezaji wasiokuwa na viwango na kusababisha kukosa nafasi za kucheza na
kuishia kukaa benchi.
Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti, wapenzi wa michezo nchini
wamesema ni aibu kwa mchezaji wa kigeni kusajiliwa kutoka nchi ya mbali na
kujikuta akimaliza msimu mzima huku akishindwa kuingia katika timu ya kwanza.
Ibrahim Hassan, mkazi wa Shinyanga, amesema wengi wa wachezaji
wanaosajiliwa katika baadhi ya klabu nchini ni wale wanaosajiliwa bila ya
kuzingatia vigezo vya kimataifa vinavyotakiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu
Duniani (FIFA).
Amesema mojawapo ya masharti yanayopaswa kuangaliwa wakati wa usajili wa
wachezaji wa kigeni ni pamoja na ushiriki wake katika timu ya taifa lake kule
anakotoka, na kuongeza kuwa hilo linaweza kupunguza usajili wa wachezaji
wabovu.
Amesema wingi wa wachezaji wa kigeni ndani ya klabu wasiopata nafasi ya
kucheza kunaziba nafasi ambazo zingechukuliwa na wachezaji vijana ambao
wangekuja kuwa na faida kwa klabu husika na timu ya Taifa siku zijazo.
Amesema mamlaka husika zinapaswa kuweka sheria kwa klabu ili kumsajili
mchezaji wa kigeni kutoka nje ya nchi na kuhakikisha mchezaji anayesajiliwa
kuwa anakalia benchi bila.
“Kama zitakuweko sheria za kudhibiti klabu kutakuwa na umakini wakati wa
kusajili wachezaji wa kigeni na kupunguza idadi ya wachezaji wasiokuwa na
viwango kuja kuziba nafasi za wachezaji wazawa,” amesema Hassan.
Mwenyekiti wa Chama cha Waamuzi wa Soka, Mkoa wa Mwanza (MZFA),
Emmanuel Mataba, amesema ni aibu kwa klabu kuwa na wachezaji wa kigeni
saba halafu wanaocheza katika timu ya kwanza ni watatu au wanne huku wengine
wakiwa benchi.
Amesema klabu zinaweza kuwa na wachezaji wachache wa kigeni lakini wenye
mchango mkubwa ndani ya klabu kuliko kuwa nao saba wasiokuwa na mchango
unaotakiwa ndani ya klabu, na kujikuta klabu zikijibebesha mzigo mzito.
Kocha wa zamani wa Simba, Mwadui FC na sasa Dodoma, Jamhuri Kihwelu
‘Julio’, amesema anaamini wapo wachezaji wazawa wenye uwezo unaolingana
na wachezaji waliosajiliwa kutoka nje ya nchi na kulipwa mamilioni.

Amesema kusajili wachezaji wa kigeni wasiokuwa na uwezo ni kuendelea kuua
vipaji vya vijana wachanga ndani ya klabu husika, hali ambayo haina afya kwa
mustakabali wa Timu ya Taifa (Taifa stars) na mchezo wa mpira kwa ujumla.
Amesema hakuna haja ya klabu kuwa na mlundikano wa wachezaji wa kigeni
ambao hawapati nafasi ndani ya klabu zao, badala yake kilabu ziwekeze nguvu
na fedha nyingi katika timu za watoto kwa manufaa ya siku zijazo.
Kaimu Katibu Mkuu wa (TFF), Wilfred Kidao, amesema kimsingi ni jukumu la
klabu husika kuwa makini na wachezaji wanaotaka kuwasajili kuja kuzitumikia
katika mashindano mbalimbali ya ndani na ya kimataifa.
Amesema tatizo la klabu nyingi nchini ni kukosa mawakala makini hasa wakati wa
kutafuta wachezaji wa kigeni wa kuja kuzitumikia katika mashindano mbalimbali;
vinginevyo zitaendelea kupata shida za kujitakia kila mara.
“Kwetu kama TFF tunachoweza kuzisisitiza klabu ni kuwa na mipango endelevu
kwa timu za vijana wa rika zote kwa manufaa ya klabu zenyewe na kwa mpira wa
Tanzania kwa ujumla kwa siku za usoni,” amesema Kidao.