*Wazee wataka waruhusiwe watumie ‘nguvu za miujiza’

“Inawezekana shetani kaingia. Huku Tanzania tuna uwezo hata wa kutumia ungo…mimi nimekulia hapa, mpaka ni katikati ya ziwa…Kama ninyi (Serikali) hamna bunduki, wananchi wapo tayari kupigana kwa kutumia fito…Hatutakufa mpaka tuone mwisho wa mgogoro huu, tupo tayari hata kwa kutumia miujiuza yetu,” Haya ni maneno ya  Mzee Anyosisye Mwakenja (80) wa Kijiji cha Matema Beach.

Maneno hayo yanamfanya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, aingilie kati na kuwabembeleza wazee kwa kusema, “Hapana, hapana wazee wangu, msifanye hivyo (kutumia ungo na miujiza). Serikali yenu iko imara na imenuia kumaliza mgogoro huu kwa njia ya mazungumzo. Maombi yangu ni kwamba mtakuwa hai wakati mgogoro huu unamalizwa kwa njia za kidiplomasia ili siku moja tukutane tushangilie. Nina uhakika tutashinda kesi hii.’


Kauli ya Mzee Mwakenja inawakilisha hisia za wazee na wakazi wa Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya, ambao kwa miaka yote maisha yao yamekuwa yakitegemea matumizi ya rasilimali za Ziwa Nyasa, lakini sasa wana shaka endapo urithi huo kutoka kwa Mungu wataendelea kuufaidi. Malawi imejitangazia kuwa Ziwa Nyasa lote ni mali yake.

 

Membe, pamoja na timu za wataalamu zilizoundwa kwa ajili ya kukusanya vielelezo na ushahidi wa wananchi waishio kando ya Ziwa Nyasa upande wa Tanzania, wiki iliyopita alizuru Kyela kwa ajili ya kupata maelezo ya ushahidi kutoka kwa wazee wanaoijua vema historia ya Ziwa hilo.


Wazee wote waliozungumza, hakuna aliyesema kwamba Ziwa Nyasa ni mali ya Malawi. Tena, mzee mmoja wa Kijiji cha Katumbasongwe, Michael Mwang’onda (70), yeye aliishangaa Serikali ya Tanzania kusikia ikisema nusu ya Ziwa ndilo mali yake! Yeye anasema Tanzania ndiyo yenye umiliki wa sehemu kubwa ya ziwa hilo.

 

Mzee Mwang’onda anasema Tanzania inamiliki theluthi mbili ya Ziwa Nyasa, na kwamba Malawi ilichonacho kwenye Ziwa hilo ni theluthi moja tu.

 

“Sisi tunamiliki theluthi mbili, mpaka upo kule Milambo ziwani kabisa, ushahidi upo, kuna barabara ya Waarabu na farasi, inapita kuelekea kule (ananyoosha mkono) ambako kulikuwa na mji, lakini kwa sasa umemezwa na maji, hili ziwa linapanuka,” anasema Mzee huyo na kushangiliwa.


Wazee waliopata wasaa wa kuzungumza katika Kijiji cha Katumbasongwe pamoja na Mzee Michael, ni Mbile Mwakasekele (79), Main Mwakisambwe (83), Jangson Mwakilima (60), Ena Ngomba (62), SWumukaga Kyumba (82), Jestina Kyelu (70), Lauden Mwasulama (74), Edwin Kasilati (75), Elisa Jolam (67), Jonan Kajula (61) na Amos Mwakyusa (75).


Awali, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile, alitoa historia ya Kyela kwa Waziri Membe, kwa kusema, “Eneo hili (Kyela) lilikaliwa na watu wa kabila la Konde. Mwaka 1840,  kulitoke vita kati ya Wanyakyusa na Wakonde, na Wakonde wakashindwa na kukimbilia upande wa pili wa Ziwa wa Malawi ambako wanaishi hadi sasa. Kimsingi sisi ni watu wamoja, kusema kwamba hatuna haki ya ziwa hili kutokana na mkataba wa mwaka 1890 kati ya Wajerumani na Waingereza si kweli.”


Hoja kama hiyo ilitolewa na wazee wote waliozungumza na Waziri Membe. Baadhi yao walitumia lugha ya Kinyakyusa kuzungumza kwa hisia kali

Wazee wa Katumbasongwe

Katumbasongwe ndipo mahali ambako Mto Songwe unapita ukitenganisha Malawi na Tanzania kabla ya maji kuingia ziwani. Mzee Mbile Mwakasekele (79) wa Katumba Songwe, alisema mpaka halisi wa iliyokuwa Ujerumani ya Afrika Mashariki (Dutch East Africa) au Tanganyika ambayo kwa sasa ni Tanzania, ulianzia eneo la Ngara nchini Malawi na kupita Kusini ambako ulikutana na mpaka wa nchi ya Zambia katika eneo la Tunduma.

“Kama Wamalawi wanataka, basi turejee kwenye historia na mipaka ya asili iliyowekwa na Wajerumani kabla ya Waingereza…waikubali hivyo watapoteza sehemu kubwa ya ziwa,” anasema.


Mzee Mwakisambwe anasema mpaka kati ya Malawi na Tanzania upo katikati ya ziwa, na kwamba ukweli huo unathibitishwa na namna meli za Malawi zilivyokuwa zikisafiri ziwani.

“Meli za Malawi zilipita katikati, ilipokuwa Malawi iliweka bendera ya Malawi , ilipofika huku ilipandisha bendera ya Tanzania , mpaka upo katikati,” anasema.


Mzee Amos Mwakyusa, anasema; “Hili kwangu si jambo la kuambiwa, bali nimeona alama za mpaka zikiwa zimewekwa na Wajerumani kwenye mbuyu katika eneo la Ngara, kulikuwa na maelezo yanayosema hapo ndipo mwanzo wa himaya ya Wajerumani katika Afrika Mashariki ( Tanganyika ).”


Anakumbuka kuwa mahali hapo walipatumia kupumzika wakati wakiwa safarini kwenda nchini Afrika Kusini ambako walienda kufanya kazi migodini.


Jonan Kajula alisema Waingereza waliipendekea Malawi katika mkataba wa mwaka 1890, lakini ukweli ni kwamba mpaka halisi unaanzia pale mto Songwe unapoingia ziwani na kwenda hadi Mto Shire ulioko kusini, na hivyo kulifanya ziwa ligawanywe nusu kwa nusu kwa mataifa yote mawili ya Tanzania na Malawi.


Michael Mwang’onda anasema baba yake aliyefariki akiwa na umri wa miaka 116, ndiye aliyekuwa mwasisi wa Kijiji cha Katumbasongwe. Anasema Tanzania inamiliki theluthi mbili ya ziwa, ilhali Malawi wakiwa na theluthi moja tu. Awali, kijiji hicho kilikuwa katika eneo la Milambo, ambalo kwa sasa lipo kilometa mbili ndani ya ziwa.

 

Augustino Mwakasoko, aliyekutwa ziwani na wananchi wengine wakiendelea na shughuli za uvuvi, katika pwani ya Katumbasongwe, alisema, “Kama Malawi wanadai kuwa eneo hili ni lao, basi wawe tayari kujlipa mawimbi haya yanayopiga huku katika ardhi yetu.”

Matema Beach

Baadhi ya wazee ambao Waziri Membe alikutana nao Matema ni Oda Mwasongela, Mzee Ernest (88), Edward Mwaijege, Philip Mwandemele, Obas Mwansasu, Andalwise Mwakyele (70), Anyakwise Mwaifiga (84), na Anyosisye Mwakenja (80).


Mzee Obas Mwansasu (72) wa Matema Beach , alisema, “Wakati tunazaliwa hadi tunakua, wazee wetu hawakupata kutueleza kuwa ziwa hili ni mali ya Malawi. Malawi hawajawahi kupanua himaya yao hadi huku. Hili si jambo la kukusumbua kichwa…Hawa Malawi wanaota ndoto zxa mchana,” alisema Mzee Philip Mwandemele (70).

 

Akizungumza kwa Kinyakyusa, Anyakwise Mwaifiga (84) alisema eneo lote la Malawi lilikuwa likikaliwa na Wanyakyusa, na kwamba utawala wa Wajerumani ulijitanua hadi eneo la Ngara, ambalo ni kama kilometa nne kutoka Karonga nchini Malawi, lakini likaongezwa hadi kilometa 20.


Mzee Philip Mwandenele (73) alimkabidhi Waziri Membe kitabu kinachothibitisha kuwa sehemu ya Ziwa Nyasa ni mali ya Tanzania. Kitabu hicho kiliandikwa na raia wa Kijerumani, Theodor Meyer, aliyezaliwa mwaka 1864. Alifika Ukyakyusa mwaka 1891 kama kiongozi wa kikundi cha kwanza cha Wamisionari wa Kanisa la Morovian.

 

Aliendelea na kazi hadi mwaka 1916 Wajerumani walipoondolewa na Waingereza. Alifariki dunia mwaka 1933 nchini Ujerumani. Utafiti wake juu ya mila na desturi za Wanyakyusa ambao aliufanya kati ya mwaka 1891 na 1916, aliendelea kuusahihisha akiwa Ujerumani. Nakala moja aliipeleka katika Makumbusho ya Habari za Mataifa mjini Hamburg, Ujerumani. Baada ya muda mrefu, andiko lake lilishughulikiwa na kupigwa chapa mwaka 1989, na baadaye kutafsiriwa kwa Kiswahili.

Msimamo wa Tanzania

Kwa upande wake, Waziri Membe anasema  Ziwa Nyasa ni urithi halali wa Watanzania.

“Nashukuru sana wazee wangu, kuanzia kule Katumbasongwe hadi hapa Matema Beach wote mnasema sehemu ya ziwa hili ni yetu. “Mimi nawashukuru sana, kesi hii lazima tushinde. Mapambano ya aina hii na mengine nisiyoyasema huwa hatushindwi,” amesema Membe kwa kujiamini.


Membe ameendelea kusema; “Ziwa hili ni triple heritage ya nchi tatu, lengo letu ni kuhakikisha kuwa hadi Desemba, mwaka huu tumemaliza documentation. Najua wanakwepakwepa, lakini hii ni kudhihirisha kuwa tuna hoja kubwa sana. Hata kama wakiendelea kukwepakwepa sisi hatutarudi nyuma. Sheria ziko wazi kwamba maji yanapotenganisha nchi na nchi mpaka unakuwa katikati ya maji. Mkataba wa mwaka 1890 ulivurunda sana, ni jambo la kipuuzi. Kote ambako kulivurundwa, wamerekebisha, kwanini isiwe kwetu?


“Kuwapo au kutokuwapo mazungumzo hakutaifanya Tanzania itulie, sisi tunaendelea na kazi. Tutaenda kwenye leadership forum ya SADC…hii inahusisha marais wastaafu, tutakwenda AU (Umoja wa Afrika), tutakwenda ICJ (Mahakama ya Kimataifa).


“Nawapongeza sana Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Mbeya…sisi ni watu wakubwa, big power…tunaogopwa, hata ukipenga tu. Tuna nguvu za kila aina. Wananchi wasiwe na wasiwasi, waendelee na shughuli zao, wasiwe na shaka juu ya amani yao, tuna kazi kubwa ya kuumaliza mgogoro huu kwa amani. Endeleeni na doria sehemu ya ziwa letu, hii si “no man’s land”, tuna dhamana ya kulinda. Suala hili tumenuia kulimaliza katika uongozi (awamu) wetu.”


Membe ameshafanya ziara kama hiyo katika Mkoa wa Ruvuma ambako pia kuna sehemu ya Ziwa Nyasa. Akiwa Ruvuma, pia alizungumza na wazee. Akiwa Kyela, alizuru pia mpaka wa Kasumulu ambako alikutana na Chifu wa Karongo, Clement Mwakasungura.

 

Katika hotuba zake zote, Membe amekuwa akisisitiza kwamba ni ya Serikali ya Tanzania ni kuhakikisha mgogoro kati yake na Malawi unamalizwa kwa njia za kidiplomasia, hasa kwa kuzingatia kuwa Watanzania na Wamalawi ni ndugu wa damu.


1366 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!