Mapema Julai mwaka huu, nilikutana na mzee mstaafu kutoka moja ya wilaya za mkoani Iringa. Mzee huyu ambaye ndiyo kwanza amestaafu  ualimu, nilimfahamu kwa njia ya simu kupitia kwa rafiki yangu. Haja ya mzee huyu ilikuwa tukutane nimsaidie kutafuta gari aina ya Hiace anunue.

Nilimwelekeza kwa simu na hatimaye alifika ninapoishi – mtaa wa Ngome-Kihesa, mjini Iringa. Mzee huyu alikuja na gari aina ya Toyota Cresta GX 100. Alinieleza kuwa gari lile ni lake alilonunua wiki moja iliyopita  kwa Sh milioni 10.

 

 

Vilevile akaniambia amepata mafao yanayofikia Sh milioni 47, ndipo katika hizo akaona aanze kujipongeza kwa kununua gari la kutembelea. Ingawa mazungumzo haya hayakuwa sehemu ya shida iliyomleta kwangu (yaani kusaidiwa kununua Hiace), lakini yalinipa funzo kubwa na nikajikuta nayatumia kama msingi wa uamuzi wangu kwa shida yake hiyo.

 

Kwa kifupi ni kwamba mstaafu huyu alikwishabahatika kujenga nyumba ya kuishi huko kijijini kwao, lakini baada ya kustaafu na kukabidhiwa “mamilioni” akaona kijijini hakumfai. Akaamua kutafuta nyumba ya kuishi maeneo ya mjini na mradi alioona utamsaidia kwa maisha yake baada ya kustaafu ni kufanya biashara za daladala!


Angalia mchanganuo wa mafao aliyopata na matumizi aliyofanya. Alinunua gari kwa Sh milioni 10 na nyumba ya mjini Sh milioni 22. Wakati anakuja nimsaidie kununua Hiace alikuwa amebakiwa na Sh milioni 12. Sh milioni tatu alijigharimia matumizi madogomadogo kama anavyosema mwenyewe.


Nikainama kwa muda, nikatafakari na ghafla moyo wangu ukaingiwa na hofu pamoja na huruma. Harakaharaka nikajua maisha ya mstaafu huyu yatakuwa magumu siku chache zijazo. Nilipotafakari adha ya biashara ya daladala nikaona kama nikimsaidia kununua Hiace anayoitaka nitakuwa nimechangia kummaliza.


Nikamshauri mzee huyu kwamba Sh milioni 12 alizobaki nazo hazitoshi kununua gari zima, sana sana atapata Hiace banzi (Hiace iliyochoka). Ili kumuokoa dhidi ya msiba unaomsubiri, nikatumia muda mwingi kueleza matatizo yaliyopo katika biashara ya daladala huku nikimshauri aachane na wazo hilo mfu.


Nikampa neno hili la mwisho, “Kwa kuwa umeshatumia fedha nyingi kununua nyumba na gari – ambavyo vyote havizalishi fedha, usiingie tena kwenye mradi usiokuwa na uhakika mzuri wa kuzalisha fedha. Nakushauri ufikirie kilimo na ufugaji”. Hata hivyo, pamoja na juhudi zangu hizo za kufafanua hayo lakini aliendelea kusisitiza nimsaidie kutafuta Hiace!

 

Nikaona isiwe tabu, ndipo nikamwambia kwa fedha aliyonayo sitaweza kumtafutia na sitaki kumtafutia gari halafu kesho na keshokutwa likisumbua aje aseme kijana Sanga alinitia umaskini. Tukaachana, akaenda zake. Baada ya wiki moja nikapokea taarifa kuwa mzee yule alifanikiwa kupata na kununua Hiace kwa milioni 8!


Ninapoandika makala haya ni miezi miwili imepita tangu mzee yule anunue Hiace ile, lakini imeshaua injini na imepaki nje ya nyumba aliyonunua. Huhitaji kuwa mtabiri kubaini kuwa maisha ya mstaafu huyu yatakuwa ni magumu na ya tabu hadi kufa kwake.


Yaliyompata mstaafu huyu yanawapata wastaafu wengi, yanawakumbuka Watanzania wengi kuanzia wasomi na wasiosoma, walioajiriwa na wasioajiriwa, wafanyabiashara, wanasiasa na wananchi wa kawaida. Wengi hawana akili ya fedha. Hawajui wapateje fedha, hawajui wakishapata fedha waziongezeje na wala wazitumieje.


Huu uwezo wa kutafuta, kuongeza na kutumia fedha ndio ninaouita ‘Financial IQ.’ Huko nyuma kupitia gazeti hili nimewahi kuandika makala iliyokuwa na maudhui kuwa wafanyakazi (hasa walimu na madaktari) hawahitaji kuongezewa mishahara. Licha ya kwamba maudhui yale yalipokelewa kwa hisia tofauti lakini maana yangu ilikuwa na picha kubwa.


Hata kama ukiongezewa mshahara ukawa mkubwa kiasi gani, lakini kama huna akili ya kuutumia vema hutafika popote kimaendeleo. Watu wawili wanaweza kuwa katika kazi moja, wakawa wanalipwa mshahara mmoja na wakawa na majukumu sawa, lakini mmoja akawa na maendeleo makubwa kuliko mwingine. Mara nyingi mtu asipojipa muda wa kufanya ulinganisho huo, ni rahisi kuhamishia uduni wa maisha yake kwa wengine, hasa Serikali!


Kiwango cha ‘Financial IQ’ kinapimwa kwa kuangalia unatumiaje unachokipata kuzalisha vingi. Katika hili kila fedha inayopita katika mikono yako inatakiwa kuchukuliwa kama mbegu. Kama ninalipwa shilingi laki tano kwa mwezi halafu nikatumia laki tano yote katika matumizi yasiyozalisha (kama vile pango, chakula na mavazi) basi ‘Financial IQ’ yangu inahesabika kuwa ni sifuri!


Lakini pengine kuna mfanyakazi mwenzangu anayelipwa hiyo hiyo, laki tano halafu kila mwezi akawa anatenga shilingi elfu hamsini, unapoisha mwaka atakuwa na shilingi laki sita. Tuchukulie imepatikana fursa sehemu kuwa kuna kiwanja kinauzwa laki sita; moja kwa moja mfanyakazi mwenzangu atakuwa na nafasi ya kukinunua.


Kwa kuwa ardhi inapanda thamani, kila siku kiwanja alichonunua kitakuwa kinapanda thamani, hivyo utajiri wake utakuwa unapanda wakati mimi nitakuwa pale pele ama nitakuwa ninashuka kwa sababu sina uwezo wa kutumia fedha ninayopata kuzalisha fedha nyingine.

 

Unaweza kujiuliza: ‘Nitajuaje ikiwa nina ‘Financial IQ’, na kwa kiwango gani?’ Jibu ni rahisi. Kiwango cha maisha yako ya uchumi kinapima ‘Financial IQ’ uliyonayo. Kama unaishi maisha ya uhaba na ‘kuungaunga’ katika eneo la fedha basi ujue una ‘Financial IQ’ ndogo. Kama unaishi maisha yenye viwango vya juu kiuchumi basi ujue una ‘Financial IQ’ kubwa.


Ni vema nieleweke kuwa hapa sizungumzii kiwango cha fedha ama mali unazomiliki, la hasha! Ninazungumzia mfumo wa fikra zako katika kupata, kuongeza na kutumia fedha. Kwa lugha rahisi ni kuwa kuna watu wa aina mbili. Kundi la kwanza ni wale wanaopata fedha na kuzitumia ‘zooote.’ Kundi la pili ni wale ambao kila wapatapo fedha hufikiria namna bora ya kuzizalisha ziongezeke. Kundi la pili wana ‘Financial IQ’ kubwa wakati kundi la kwanza wana ‘Financial IQ’ ndogo.


Ili ukuze ‘Financial IQ’ yako kuna mambo unahitaji kujifunza na kuyazoea. La kwanza ni imani yako kuhusu fedha. Kila mtu anamiliki kiwango cha fedha sawa sawa na imani yake kuhusu fedha. Kuna watu wanaamini kuwa mtu mwenye fedha nyingi (tajiri) hawezi kumpendeza Mungu na wala hawezi kuingia mbinguni.


Kwa kuwa wanaipenda mbingu na kwa kuwa kwao umaskini ndiyo utakatifu, basi hubaki kuwa na uhaba wa kifedha. Kuna watu wameunganisha fedha na imani za ushirikina. Hawa wanaamini kuwa matajiri wengi (kama si wote) wanatumia ushirikina katika biashara zao. Mtu wa hivi hawezi kuwa na fedha za kutosha kwa sababu katika fikra zake ameunganisha fedha na ushirikina, na kwa kuwa hapendi kuwa mshirikina basi anabaki kuwa maskini!


Wafanyakazi wengi (pengine kutokana na mishahara isiyotosha) huamini kuwa mfanyakazi hawezi kujenga nyumba ama kununua gari isipokuwa awe amefanya ufisadi kazini kwake. Ukiunganisha maendeleo na wizi katika fikra zako hutaendelea na wala hutakuwa tayari kujifunza kutoka kwa walioendelea.


Kwa wale wanaofuatilia makala zangu nimewahi kuchambua imani hizi kwa kina huko nyuma katika makala iliyokuwa na kichwa cha habari: “Huhitaji fedha kuzalisha fedha.”

 

Jambo jingine litakalokuongezea ‘Financial IQ’ ni nidhamu yako ya kujiwekea akiba. Kabila la Wakinga tuna mila moja imara sana kuhusu uwekaji akiba. Mkinga huweka akiba ambayo hawezi kuitumia hata kama anakufa na njaa. Akiba hii iitwayo ‘Ekhefumbato’ hutakiwa kutumika pale tu inapopatikana akiba nyingine ya kubadilisha na ni lazima itumike kwa kusudi la msingi.

 

Bahati mbaya Watanzania wengi hatuna utamaduni wa kujiwekea na kuheshimu akiba zetu. Ukiweka akiba benki ambayo labda umepanga ni kwa ajili ya kusomeshea watoto, halafu unakutana na tatizo la kufiwa na unaenda kuichukua ujue bado nidhamu yako ya kujiwekea akiba ni ndogo na ‘Financial IQ’ yako iko chini.


Nigusie jambo la mwisho litakalokusaidia kuongeza ‘Financial IQ.’ Hili ni nidhamu ya matumizi. Unapopata fedha, ni vipaumbele gani unaviweka katika maisha yako? Je, vipaumbele vyako vina tija gani katika kuboresha uchumi wako sasa na baadae? Je, vitu unavyonunua vina umuhimu sawa na umuhimu unaovipa?


Huenda umeamua kuchukua mkopo benki kwa dhamana ya mshahara wako na ukaamua kununua gari la kutembelea. Je, gari la kutembelea lina umuhimu ‘halisi’ kwako? Au umeamua kununua ili na wewe uonekane kuwa umo kati ya wanaomiliki magari?


Hata kama umenunua hilo gari, hamna shida! Lakini, je, una kipato kinachokidhi gharama za uendeshaji wa gari ikiwamo mafuta na vipuri? Kuna kitu tunatakiwa kuwa nacho makini hapa kwa sababu wapo watu ambao licha ya kuwa na mishahara ya kawaida, bado wanakopa mikopo na kununua magari yanayotumia mafuta mengi kwa ufahari tu.


Ni kawaida kuona mtu ana gari la kutembelea la kifahari lakini anahangaika hata hela ya mafuta. Tabu yote ya nini? Kwa mtu mwenye ‘Financial IQ’ kubwa ataanza kutengeneza vitegauchumi kwa kutumia mshahara ama mkopo kabla ya kufikiria kununua vitu vya starehe kama gari la kutembelea.

 

Nihitimishe kuhusu kisa cha yule mzee mstaafu. Kama mstaafu yule angalinifuata akiwa na milioni 47 zote pengine ningemshauri tofauti. Nisingemwambia kununua nyumba mjini badala yake ningemwambia aishi kule kule kijijini alikojenga afuge na kulima.

 

Kama anatamani gari la kutembelea ningemsaidia kutafuta ‘Pick-up’ ambayo akitaka kwenda harusini anaenda itamfaa na akitaka kufanyia shughuli za shamba itamfaa. Bahati nzuri ‘Financial IQ’ mtu huzaliwi nayo isipokuwa unajifunza kwa kuwa na mtazamo na maamuzi sahihi kuhusu fedha.


Watanzania tunahitaji ushindi wa kiuchumi. Wasalaam!

[email protected] 0719 127 901


By Jamhuri