Wafuasi wa Uhuru Kenyatta walijitokeza mwishoni mwa wiki kusherehekea ushindi wake wa kiti cha urais wa Kenya. Uhuru amepata ushindi kwa asilimia 50.03 dhidi ya mpinzani wake wa karibu, Raila Odinga.

Matokeo yaliyotolewa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya yanaonesha kuwa Uhuru amepata kura 6,173,433 dhidi ya Odinga aliyepata kura 5,340,546.


Hata hivyo, Odinga amepinga matokeo hayo kwa madai kwamba yalikuwa yamehujumiwa, hasa baada ya kutokea hitilafu katika mitambo ya kielektroniki iliyokuwa inatumiwa katika shughuli hiyo. Amesema kwamba muungano wao unakwenda mahakamani kupinga matokeo hayo.

 

Amesema kuwa baada ya kutokea hitilafu, kura alizokuwa amepata katika maeneo ambayo ni ngome zake, ziliongezwa kwa hesabu ya kura za muungano pinzani wa Jubilee.

Mapema wiki iliyopita, wakati shughuli ya kuhesabu kura za urais ikifanyika, CORD walilalamika bila mafanikio kuhusu shughuli nzima, hasa baada ya kura kuanza kuhesabiwa kwa mikono badala ya mashine.


Ofisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Uchaguzi ya Kenya, James Oswago, amesema kuwa uchaguzi huo ulikuwa mgumu zaidi kuwahi kufanyika na ulikuwa na changamoto nyingi.

Mjini Eldoret, moja ya vitovu vya ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2007, ulikuwa ni uwanja wa sherehe za ushindi wa Kenyatta. Kisumu, ambayo ndiyo ngome kuu ya Odinga, wafuasi wake walionekana kununa kutokana na kushindwa kwa mgombea wao.

Hotuba ya Uhuru

Kenyatta amesema anawakaribisha katika serikali yake wapinzani wake na ushindi uliopatikana si Muungano wa Jublee bali ni wa Wakenya wote.


“Uchaguzi umekwisha na uchaguzi si uadui, tukishinda baada ya uchaguzi walioshindwa na aliyeshinda mnashikana mikono na kutembea pamoja.


“Tushirikiane kwa pamoja tujenge nchi yatu, ndugu yangu Raila Odinga aje tushirikine kujenga Kenya yetu. Uko tayari Bwana Odinga tushirikiane kujenga taifa letu la Kenya?” alisema Kenyatta.


By Jamhuri