Jamii yoyote ile ni lazima itembee katika ukweli, haki, maadili, mwanga na elimu. Hakuna jamii inayoweza kuendelea pasipo watu wake kuwa wakweli na wenye maadili na akili tafakari na akili bainifu. Hatuwezi kuendelea kutambua kwamba sisi ni wajinga na bado tukaendelea kuishi maisha ya kijinga. Lazima tukubali kubadilika. Tunahitaji kufahamu lipi linaweza kubadilishwa na lipi haliwezekani na zaidi kufahamu tofauti zake. Kwa hali ilivyo sasa, Watanzania wanahitaji kupikwa na kupikika kifikra.

Duniani kote hakuna mabadiliko ya kweli na ya kudumu nje ya uhuru wa kifikra. Kwa usemi mwingine, tunaweza kusema kwamba akili iliyo huru ni nyenzo muhimu sana katika mapinduzi yoyote yale. Kabla sijaendelea na mjadala ninaomba kutoa fikra zangu. Binafsi siamini uwepo wa uchawi. Siamini uwepo wa majini. Hata kwa chembe kidogo siamini. Ukinuliza: Je, wachawi wapo au hawapo? Nitakujibu: Hawapo, isipokuwa katika mawazo ya mtu anayesadiki na anayeogopa kwamba wachawi wapo. Kama wachawi wapo wanapatikana wapi? Mimi nawatafuta. Ningefurahi sana kama mwenye tafiti za kina za uwepo wa uchawi angejitokeza hapa gazetini na kuthibitisha hoja yake ya uwepo wa uchawi. Binafsi nimefanya tafiti ya uwepo wa uchawi kwa baadhi ya makabila ya hapa Tanzania. Nilichobaini ni hofu tu. Hakuna uchawi. Hadithi na simulizi za mababu zetu bado zimetufunga. Bado ile hofu iliyopandikizwa na vizazi vilivyopita bado inafanya kazi ndani yenu. Watoto wetu wanakua huku wakisikia habari za uchawi na ushirikina, na sisi wazazi na walezi tunaendelea kuwaogopesha na kuwafundisha kwamba kuna uchawi. Tunaendelea kuwapandikiza hofu. Hofu hii wanakua nayo.

Siku moja mwanafalsafa Socrates aliwasha taa mchana [kweupe] na akaenda nayo kwenye soko la Athenes [Ugiriki ya sasa]. Pale sokoni wananchi wengi walimshangaa sana Socrates wakamuuliza: “Kwa nini wewe umewasha taa hapa sokoni wakati ni mchana na mwanga wa taa yako wala hauonekani kutokana na mwanga wa jua uliopo?” Socrates aliwajibu: “Pamoja na nuru hii ya jua lakini akili za watu wengi ziko kwenye giza nene.” Ukweli huu aliousema Socrates unawagusa watu wanaoishi kwa kuamini nguvu za ushirikina katika maisha yao. Huwezi ukafanikiwa kwa kuamini nguvu za ushirikina.

Askofu Renatus Nkwande wa JimboKuu Katoliki la Mwanza anasema: “Kuamini uwepo wa uchawi ni ushamba wa elimu na kutokuamini nguvu za Mungu.’’ Kuendelea kuamini nguvu za kishirikina katika maisha yetu ni kuonyesha kwamba bado sisi ni watoto ambao bado tunanyonya dole gumba. Mwanahabari Jenerali Ulimwengu anasema: “Jamii ikishindwa kuonyesha dalili za kukomaa na ikabakia kuwa jamii ya “kitoto” ambayo bado inahitaji baba mkali wa kuicharaza bakora, jamii hiyo inakuwa imevia, imedumaa, imekwama mahali fulani katika mchakato wa kukua. Inakuwa jamii ya kunyonya dolegumba daima.”

Msinitake kucheka. Eti mchawi ni mtu ambaye anaweza kuingia mlango ukiwa umefungwa. Anaweza kupaa bila kifaa chochote. Anaweza kumdhuru mtu yeyote. Anaweza kumgeuza panya akawa mbwa. Anaweza kuwasiliana na mapepo, shetani, majini n.k. Binafsi siamini sifa hizo. Ninazisikia tu. Hizo ni sifa ambazo kimaumbile binadamu hawezi kuwa nazo. Lakini naamini hazipo kwa binadamu ninayemfahamu. Uchawi haupo ila shetani yupo. Hakuna binadamu mchawi, ila yupo binadamu mjanja mjanja anayekuzidi ujuzi fulani. Kama wachawi wapo mbona hawaibi fedha benki? Kama wachawi wapo mbona watoto wao hawaongozi kimasomo darasani? Nisikilize; Ni kwamba dhana hii ya uwepo wa uchawi au ushirikina ilipandikizwa na mababu zetu. Kwa wakati wao walipandikiza dhana hii kulingana na mazingira yao yalivyokuwa. Kwetu sisi hatupaswi kuishi nadharia za mababu zetu.

Hata Ulaya hii dhana ya uchawi au ushirikina ilikuwepo. Barani Asia ilikuwepo, kwa bahati nzuri wenzetu wa mabara mengine waliondokana na dhana hii. Bahati mbaya ni kwetu sisi Waafrika ambao bado tumeikumbatia dhana hii potofu. Wenzetu wanatushangaa. Sisi ni binadamu tunaokua kiumri lakini tusiokua kifikra. Waafrika hatujaonyesha dhamira ya dhati ya kuondokana na dhana hii ya uchawi. Tatizo liko wapi? Kwa bahati mbaya sana, wale ambao wangekuwa mstari wa mbele kuporomosha dhana hii ya uchawi au ushirikina kutoka kwenye bongo za wanajamii wetu nao wanaamini uwepo wa uchawi. Kwa tafsiri nyingine uwepo wa hofu ya uchawi/ushirikina kwa wanajamii wetu ni mtaji kwa baadhi ya watu na taasisi za kidini. Ni mtaji makanisani. Katika jamii yetu kuna wimbi la makanisa yanayoota kama uyoga. Wachungaji wa haya makanisa wengi wao wanaamini uwepo wa uchawi/ushirikina. Ni hao hao wanaopandikiza hofu ya uwepo wa uchawi kwa waumini wao kwa kuwatungia vitabu na sala kadha wa kadha za kupambana na wachawi. Wanaaminisha kwamba uchawi upo, hivyo wapambane nao kwa nguvu za maombi.

972 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!