sport_sports_Cristiano-Ronaldo-Real-Madrid-2011Mshambuliaji wa kimataifa wa Ureno na Klabu ya Real Madrid ya Hispania, Cristiano Ronaldo, amejinasibu kuwa yeye ni mchezaji bora ulimwenguni.

Ronaldo au CR7 aliyepata kuichezea Manchester United ya England kwa miaka zaidi ya mitano, ana mengi ya kujivunia akiwa ana rekodi ya kuwa mchezaji bora wa dunia mara tatu.

Nyota huyo ambaye ni mfungaji bora wa Real Madrid ya Hispania, anasema: “Sihitaji kujitangaza, ukweli ni kwamba niko katika historia ya mpira, mimi ni legend (gwiji). Namba zinasema kila kitu.”

Ronaldo, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 30, alijiunga na Real akitokea Man U mwaka 2009 kwa kitita cha pauni milioni 80 huku akisema amefikia kiwango cha kushangaza kwa kipindi cha miaka minane iliyopita na anataka kuendelea kucheza kwa misimu mingine mitano au sita.

Rekodi yake inaonesha ana mabao 504 katika mechi 760 hivyo anajinasibu: “Mawazoni mwangu mara zote na mara zote mimi ndiye bora. Sijali watu wanachofikiria, wanachosema. Mawazoni mwangu, siyo mwaka huu pekee lakini mara zote mimi ni bora.”

Ronaldo alikuwa ameulizwa anajilinganishaje na mshambuliaji wa Barcelona na Algentina, Lionel Messi, ambaye ni mchezaji bora wa dunia mara nne akiwa na goli 418 za mechi 492 alizochezea klabu.

“Ni maoni, ninaheshimu maoni. Labda kwa mawazo yako unaona Messi ni bora kuliko mimi, lakini akilini mawazoni mwangu mimi ni bora kuliko yeye. Ni rahisi kujua na inafahamika hivyo,” anasema.

Ronaldo alijiunga Man Utd akitokea Sporting Lisbon mwaka 2003 kwa pauni milioni 12.2 akafunga magoli 118 katika mechi 292. Tangu amehamia Madrid ambako yupo kwa mkataba mpaka 2018 amefunga mabao 326 katika mechi 314.

Kuhusu iwapo kuna siku atarudi kuichezea Man United, Ronaldo amesema: “Hakuna aijuaye kesho lakini hapa nilipo Madrid nina furaha tele japo kwanza ninasikitika kuona ilipo hivi sasa kwa kuwa ningependa iwe Manchester ya kipindi kile cha miaka saba iliyopita.”

Ronaldo pia amemuongelea Jose Mourinho akisema: “Sishangazwi kwa sababu katika soka chochote kinaweza kutokea. Nilifanya naye kazi kwa miaka miwili naujua uwezo wake…

“…Najua siyo yeye tu, lakini pia Chelsea iko katika wakati mgumu. Mimi ni Mreno ninataka kumwona Mreno akiwa juu. Namtaka aondokane na wakati huu mgumu na awape furaha mashabiki wa Chelsea.”

Pamoja na hayo ya kujinasibu: kwa msaada wa mitandao ya kimataifa, tunakuletea mambo matano kuhusu nyota huyo wa dunia katika soka.

1- Ronaldo, maarufu pia kwa jina la CR7, aliwahi kufukuzwa shule baada ya kumrushia kiti mwalimu wake darasani, kitu ambacho Ronaldo anasema alifanya vile kwa sababu mwalimu wake alimvunjia heshima.

 

2- Huenda hili likawa geni kwako, Cristiano Ronaldo, ambaye ni raia wa Ureno, pamoja na wazazi wake, kwa upande wa mama yake ana asili ya Afrika. Bibi wa mama yake Cristiano Ronaldo alikuwa ni mtu mwenye asili ya Visiwa vya Cape Verde.

 

3- Kama ambavyo tumezoea kuishi maisha ya watoto wa kiume na wa kike kulala vyumba tofauti, kwa upande wa Cristiano Ronaldo aliwahi kulazimika kulala chumba kimoja na dada zake kwa sababu ya umaskini wa familia yake, wa kushindwa kumudu kupanga nyumba kubwa.

 

4- Licha ya kuwa Cristiano Ronaldo ni staa wa soka lakini hadi leo hii mwanamke aliyemzaa Cristiano Ronaldo Junior ambaye ni mtoto wa Ronaldo hajulikani, jambo hili linawashangaza wengi kwa mtu maarufu kama Ronaldo watu kushindwa kumjua mzazi mwenzake.

 

5- Baada ya fainali za Kombe la 2006 aliomba kuondoka Manchester United baada ya kugombana na Wayne Rooney katika michuano ya Kombe la Dunia 2006, hivyo Rooney akaoneshwa kadi nyekundu. Tukio ambalo lilivunja uhusiano mzuri ya baina ya wachezaji hao.

4578 Total Views 2 Views Today
||||| 2 I Like It! |||||
Sambaza!