Wagonjwa zaidi ya saba waliokuwa wanadaiwa bili za matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wamesaidiwa kulipa bili hizo na Idara ya Ustawi wa Jamii.

“Jamani ninawaombeni msaada, nisaidieni mimi ni mkulima wa mahindi na muuza mahindi ya kuchoma tu, ninahitaji wahisani wa kunisaidia kuokoa watoto wangu wawili kutoka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kunilipia bili ya Sh milioni 28.”

Ni maneno ya Tumaini Jacob, mkazi wa Tabora, Kijiji cha Kaliua anayeomba msaada wa kuwatoa hospitalini watoto wake; Jennifer Frank 20 na Vailet Alex waliopata ajali ya moto na kulazwa katika hospitali hiyo.

Akielezea mkasa wa watoto hao, amesema Julai 21, mwaka huu walipata ajali ya kuungua moto baada ya jiko la gesi kulipuka na kuwaunguza vibaya watoto hao wakalazwa hospitalini hapo.

Jacob ameeleza kuwa baada ya kufika Muhimbili walipokewa vizuri na madaktari na wakawa wanapatiwa tiba.

Wakiwa hospitalini hapo waliambiwa walipe Sh 100,000 kwa ajili ya kumwongezea Jennifer nyama zilizoungua na kuharibika ili kurekebisha sehemu zilizoungua.

Amesema baada ya siku tatu aliambiwa bili yake inasoma Sh milioni 10 kwa Jennifer na Vailet Sh 1,700,000 ndipo alipoanza kuona ubaya wa kukosa pesa, kwani hakuwa na uwezo wa kulipa pesa hizo. Amesema hadi Septemba 4, 2019 wagonjwa wote waliruhusiwa na bili yao ikiwa inasoma Sh milioni 28 kwa wagonjwa wote wawili.

Kwa upande wake, Maninge Hamisi, mkazi wa Tandahimba amesema kuwa alimleta mgonjwa wake ambaye ni dada yake katika hospitali hiyo na akamtaja kwa jina la Asha Bakari.

Amesema alipewa rufaa kutoka katika Hospitali ya Tandahimba baada ya kufanyiwa operesheni na kuonekana hali yake haijatengamaa, ndipo madaktari walimpatia rufaa hiyo.

Hamisi amesema baada ya kuja Muhimbili walipokewa na kupewa matibabu vizuri na mgonjwa akafanyiwa operesheni ya pili wakalipa Sh 500,000, kisha mgonjwa akaendelea vizuri.

Amesema mgonjwa huyo alifanyiwa tena operesheni ya tatu baada ya kuonekana kidonda chake kinatoa usaha na baada ya kufanyiwa operesheni hiyo anaendelea vizuri na kilichokuwa kimebakia ni ulipaji wa bili ya matibabu ya Sh 3,400,000 ambazo kulingana na uwezo wake kwa kuwa  ni mkulima, alishindwa kulipa bili hiyo na kuamua kuomba msaada.

Levina Jacob, mkazi wa Kijiji cha Masaki, wilayani Kisarawe, mkoani Pwani aliomba msamaha wa kumchangia gharama  za matibabu ya mwanawe, Albinas Sindano, ambaye anasumbuliwa na matatizo ya figo aliyoyapata wakati wa ujauzito.

Levina amesema alipokuwa mjamzito wa mimba ya miezi minane alikuwa anasumbuliwa na kuvimba miguu na alipokwenda katika Hospitali ya Chanika alipewa rufaa ya kwenda Amana na alipofika katika hospitali hiyo aliambiwa hawamuwezi mgonjwa wake, hivyo ni vema akapelekwa Muhimbili, ndipo walipomwandikia kwenda kutibiwa hospitalini hapo.

Amesema tangu Julai 15, 2019 alifika katika hospitali hiyo akawa amepewa kitanda na dawa, lakini matibabu ya ugonjwa wa mtoto wake hayakufanyika kutokana na uwezo wake wa kumudu baadhi ya gharama kuwa mdogo.

Walivyozidi kukaa hospitalini hapo ndipo mgonjwa wake akajifungua salama, lakini uwezo wa kulipia gharama za mtoto na mama hakuwa nao, hivyo akaomba asaidiwe pesa za matibabu kwa ajili ya mwanae.

Mariamu Ali, mkazi wa Mahuta, Mtwara

yeye alikuwa anaomba msaada wa kulipiwa bili ya mgonjwa wake mwenye tatizo la saratani aliyelazwa Muhimbili aweze kulipia gharama za matibabu kutokana na uwezo wake kuwa duni.

Amesema kuwa mgonjwa aliyemleta ni mama yake mzazi na yeye ndiye muuguzaji wa mgonjwa huyo ambaye anasumbuliwa na saratani ya kibofu cha mkojo, ambapo awali mama yake alipelekwa katika Hospitali ya Birigita iliyopo mkoani humo kwa tatizo la kukojoa mkojo wa damu.

Ameongeza kuwa baada ya hapo madaktari walimpatia mgonjwa wake rufaa ya kwenda katika Hospitali ya Ocean Road ambapo baada ya kufika hapo na kufanyiwa matibabu akapewa tena rufaa ya kwenda kulazwa Muhimbili ambapo walilipa Sh 280,000 walizosaidiwa na ndugu na majirani.

Mariamu ameongeza kuwa kikubwa zaidi ilikuwa bili ambayo ilikuwa imefika Sh 2,500,000, na uwezo wa kulipia pesa hizo hakuwa nao, hivyo kuwaomba wasamaria wema kumsaidia pesa aweze kulipia bili hiyo na kumtoa mgonjwa wake katika hospitali hiyo.

Naye Mariamu Ramadhani, mkazi wa Muheza, Tanga aliomba msaada wa kulipia bili ya mtoto wake wa kidato cha nne, Rehema Hassan, anayesoma katika shule ya sekondari, Mtaa wa Goba aliyelazwa hospitalini hapo kwa tatizo la kupigwa tumboni na kitu chenye ncha kali.

Amesema mtoto wake alipatwa na mkasa huo Juni 8, mwaka huu baada ya kurudi nyumbani akitokea shuleni na alipobadilisha nguo tu aligombana na ndugu yake wa kiume na ugomvi ulipokuwa unaendelea kaka yake akamchoma tumboni na kitu chenye ncha kali ndipo wakampeleka Hospitali ya Bombo walipomwangalia wakamwandikia kwenda Hospitali ya Mloganzila.

Baada ya kufika Mloganzila walimpatia vipimo wakalipa Sh 100,000 na madaktari wakampatia rufaa ya kwenda Muhimbili.

Amesema baada ya kuja hapo wakapatiwa matibabu na mgonjwa wake anaendelea vizuri, lakini tatizo lilikuwa bili ya kumtoa hospitalini hapo.

Amesema hakuwa na uwezo wa kulipia bili hiyo kutokana na uwezo wake kuwa mdogo, hivyo kuomba asaidiwe kulipa Sh 1,300,000.

Wagonjwa wamelalamika kutozwa pesa nyingi wakati wao wanatokea mikoani na wengi wao ni wakulima, hawana uwezo wa kulipia pesa za matibabu.

2357 Total Views 15 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!