Utata balozi wa heshima

Utata umejitokeza kuhusu raia wa Tanzania anayejitambulisha kuwa na hadhi ya kibalozi, akiwa na hati mbili za kusafiria, ikiwamo ya nchi nyingine.

Sambamba na hilo, pia ana majina yanayotofautiana katika hati zote mbili, lakini anasema hana kosa lolote.  

Hati moja ni ya Tanzania, na nyingine imetolewa na Muungano wa Visiwa vya Comoro unaoundwa na visiwa vitatu kati ya vinne vya Moroni, Mohel na Anjouan.

Kisiwa cha Mayotte kipo chini ya himaya ya Ufaransa kuanzia mwaka 1975 kutokana na wananchi wake kupiga kura ya maoni iliyowafanya wasalie kwenye himaya ya mtawala huyo wa kikoloni.

Kwenye hati ya kusafiria ya Tanzania, mtu huyo anatajwa kwa jina la Fouad Mustafa Hamdi Martis; lakini kwenye hati iliyotolewa na Serikali ya Comoro, jina linalosomeka ni la Fouad Mustafa Nagib Ahmed Hamdy. Hata hivyo tarehe ya kuzaliwa kwenye hati zote mbili ni moja, yaani Februari 26, 1974.

Kwa muda sasa amejitanabaisha kuwa ni Balozi wa Heshima na Mwakilishi wa Serikali ya Visiwa vya Comoro nchini Morocco. JAMHURI linasubiri majibu ya Comoro kuhusu madai hayo, japo yeye mwenyewe amesisitiza kuwa bado anatambuliwa kama mwakilishi halali wa Comoro nchini Morocco.

Hadhi hiyo ya kibalozi ndiyo inayowatatiza wengi, wakiwamo baadhi ya watumishi katika vyombo vya usalama; kwani amekuwa akitambuliwa na hivyo kujihusisha na mambo ‘mazito’ yanayogusa masilahi ya kampuni na nchi zenye ukwasi mkubwa.

Kwenye hati ya kusafiria iliyotolewa Comoro, Fouad anatajwa kuwa ni raia wa nchi hiyo, na kuwa Tanzania ni mahali alipozaliwa.

Kwa Sheria za Uhamiaji za Tanzania, uraia wa nchi mbili ni jambo lililopigwa marufuku, isipokuwa kwa watoto wadogo ambao wakishakuwa wakubwa hutakiwa kuukana uraia wa nchi mojawapo.

Amekuwa akitajwa kama mtu ‘muhimu’ na kiungo mahiri kati ya taasisi kadhaa za Tanzania na serikali za mataifa ya Afrika, pia Umoja wa Falme za Kiarabu.

Fouad amezungumza na JAMHURI katika mahojiano maalumu mwishoni mwa wiki na kusema kuwa yeye ni maarufu kutokana na kazi nyingi anazofanya.

Anakana kuwa yeye si tapeli, bali anachofanya kinatokana na weledi na kuheshimika kwake.

Chanzo cha habari kutoka serikalini kinasema: “Huyu mtu si rahisi kumzuia kufanya anachotaka maana ana mtandao mkubwa ndani na nje ya system [mfumo]. Ana marafiki wengi ndani ya karibu kila idara na taasisi.”

Fouad mwenyewe anasema ni Wacomoro wenyewe waliomuomba awe balozi wao wa heshima. “Mke wangu ni Mmorocco, mimi nimesoma huko na nimeishi huko. Mbali na Morocco, ninaishi Dar es Salaam, Dubai na sehemu mbalimbali duniani,” anasema.

Kuhusu kutofautiana kwa majina kwenye hati zake za kusafiria, anasema: “Mimi nimezaliwa Tanzania, lakini wakati ninatakiwa kuanza shule mama alinipeleka Marekani. Kwa hiyo jina unaloona kwenye hati ya Comoro ndilo nililotumia kusoma kule Marekani. Ndilo lipo kwenye certificate zangu nyingi, vitu vyote viko legitimate (kihalali), na Uhamiaji hapa wamepitia na kuona kila kitu kiko sawa.”

Hata hivyo, taarifa za uhakika ambazo JAMHURI limezipata zinaonyesha kuwa suala la kuwa na hati tofauti za kusafiria limekuwa likiibuliwa na kuzimwa kwa namna ambayo haijaeleweka.

“Kuna mtoto mmoja wa mtu mkubwa hapa nchini amekuwa na uhusiano naye, na amekuwa akimsaidia kwa mambo mengi. Huyo amemtafuta siku hizi za karibuni,” kimesema chanzo chetu.

Fouad anatamba kuwa anawajua wote wanaojitahidi kumfuata wakilenga kumchafua, lakini ana hakika hawatafaulu. Katika kuthibitisha hilo, JAMHURI limeonyeshwa ushahidi wa baadhi ya picha za Fouad na mmoja wa viongozi waandamizi wa Jeshi la Polisi mkoani Dar es Salaam katika hoteli moja ya kitalii jijini humo.

“Nawajua wanaonichafua, siwezi kuchafuka, I am a hardworking people, ndiyo maana najulikana kwa wakubwa wengi, hilo siwezi kuficha, hadhi yangu ya ubalozi ipo, na kuwa na hati ya kusafiria ya Comoro siyo tatizo,” anasema.

Kwa maelezo yake, hivi karibuni ameteuliwa na chombo cha Umoja wa Mataifa (UN) kwa miaka miwili kuwa mwakilishi wake katika masuala ya uchumi, amani na utoaji misaada katika maeneo mbalimbali.

Anamtaja mmoja wa watu (JAMHURI halimjui) anayedai kuwa anamfuatafuata. “Najua (anamtaja) ndiye anayenifuata. Sijui ana (neno haliandikiki) gani ambazo zinasumbua, namuomba Mungu amsaidie.”

Akizungumza kwa mbwembwe, anasema yeye ni mwakilishi wa mfalme (hataki kumtaja) na mshauri wa Serikali ya Dubai. Na-keep low profile, lakini mimi ni mtu mzito kupita kiasi. Niko legitimate, na sibabaiki. Mawaziri wengi wananijua, mawaziri wa mambo ya nje waliopita na wa sasa wananijua, mawaziri wote wananijua kutokana na kazi zangu, hata Serikali hii wananitambua kuwa ni mtu ninayefanya kazi za uwakilishi.

“Hapa mimi ni mwakilishi wa vitega uchumi vya Hyatt Tanzania,” anasema.

Miongoni mwa vitega uchumi vya Hyatt Tanzania ni hoteli kadhaa, ikiwamo Hyatt Kilimanjaro Hotel iliyopo jijini Dar es Salaam.

“Najua sina shida, Uhamiaji wamefuatilia faili langu liko vizuri, siyo kwamba nimehonga. Mimi ni Mtanzania – mama yangu ni Mhehe na baba ni Mjerumani, hii rangi (weupe) siyo shida. Babu yangu Charles Mzena amehudumia nchi hii kwa miaka 45, amemhudumia hadi Mwalimu Nyerere. Babu yangu Martis alioa Mhehe na kumzaa mama yangu Mary Martis. Ukitaka stori ya kunisifu sawa, nitakupa ili ujue kwanini ninaheshimiwa na kwanini nimepewa hiyo hadhi,” anasema.

Fouad akizungumza kwa mbwembwe nyingi anasema: “Nina digrii ya masters, najua lugha nyingi. Najua lugha sita za kimataifa – Kiswahili sikihesabu maana ni lugha yangu. Nazungumza Kiingereza, Kiarabu, Kifaransa, Kispaniola, Kireno na nyingine. Haiwezekani Watanzania wote tuwe mabwege, na kwa kweli kunigusa mtu kama mimi ambaye nina hadhi ya balozi ni aibu.”

Foaud anatajwa kuwa ni mtu mwenye fursa za kuingia mahali popote, na ni mwenye ushawishi wa kufanikisha alicholenga.

“Hapa kuna mashauri mengi ya kampuni mbalimbali za kitaifa na kimataifa. Kuna shauri moja nisingependa kulitaja lakini yeye amekuwa akilichelewesha kwamba anao uwezo wa kulimaliza kwa kiwango kidogo cha fedha ilhali ukweli ukiwa kwamba hawezi na serikali haiwezi kukubali. Anachofanya ni kama udalali,” kimesema chanzo chetu, lakini kwa upande wake Fouad anasema hafanyi udalali, na anajua wanaomwandama wanafanya hivyo kwanini.

JAMHURI limeonyeshwa baadhi ya picha alizopiga na viongozi mbalimbali wa kisiasa na wa vyombo vya ulinzi na usalama, hali hiyo ikitajwa kuwa ni kushawishi anaoshirikiana nao kuamini ukaribu alionao kwa wakubwa hao.

Msemaji wa Idara ya Uhamiaji nchini, Ally Mtanda, ameulizwa na JAMHURI kuhusu Fouad kuwa na hati ya kusafiria zaidi ya moja, na kusema kisheria suala hilo haliruhusiwi, lakini atatoa majibu baada ya kuwasiliana na idara husika.

“Najua wapo mabalozi wa heshima na mara nyingi wanapatikana katika nchi husika. Sina utaalamu zaidi upande huo, lakini lililo wazi ni kuwa sheria zetu haziruhusu kuwa na uraia wa nchi mbili ingawa kwa watoto wanakubaliwa, lakini wakifikisha umri wa miaka 18 inabidi wakane uraia wa upande mmoja,” anasema Mtanda.