Hata hivyo, siku hizi umeletwa utaratibu wa kuwa na “semina elekezi” kwa viongozi wote wakuu wa Serikali. Utaratibu huu unatokea mara kwa mara (periodically) pale hitaji la kuwaelekeza wanaohusika na utawala dhima na wajibu wao kitaifa.

Sijui kama utaratibu huu unafikiria gharama kubwa za kuendesha semina namna hiyo. Basi, wanasiasa wakaona wanapunguziwa uwezo wao au madaraka yao, ndipo wakaivuruga kwa kutupilia mbali ule msahafu wa utawala bora yaani lile likitabu la “General Orders”. Kitabu kile siku hizi ni nadra kabisa kukiona katika ofisi yoyote ya Serikali.

 

Hapo sasa ndipo mparaganyiko wa utawala ulipoanza kutokea. Msimamizi mkuu wa msahafu wa utawala alikuwa Katibu Mkuu wa UTUMISHI – tukiita Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi (PS President’s Office Central Establishment).

 

Kwa kuwa uti wa mgongo wa kanuni za utawala bora umevunjwa kwa makusudi na siasa, basi kila mtu serikalini aliweza kutawala na kutoa uamuzi wake. Kuanzia hapo ma-area commisioner wakawa hawasilikizi utaratibu wa utawala bora kutoka kwa ma-area secretary wao ambao ndiyo waliokuwa kitaaluma mabwana shauri wa wilaya.

 

Ma-RC hawakufuata ushauri wa wale Ma-Regional Administrative Secretaries, wao ambao ndiyo waliokuwa kitaaluma maofisa utawala wa mikoa na walifikia madaraja ya Afisa Utawala Daraja II au I katika utumishi serikalini.

 

Kadhalika, wizarani wale waliokuwa makatibu wakuu – wakiitwa “Permanent Secretaries” wenye daraja la I kiutawala katika nchi hii, wanasiasa (mawaziri) wakawabadili na kuwaita ma-“principal secretaries”; hivyo wakaondolewa ile hadhi ya “wakudumu” yaani “permanent” na sasa wakawa “principal” yaani wakuu.

 

Baada ya mvurugano huo, kukaja kitu kikiitwa “Decentralization”. Utaratibu au mfumo huo ulianza Februari 1972 kwa nia ya kusogeza huduma karibu zaidi kwa wananchi.

 

Kichama kulitolewa SERA, kitu kilichoitwa MWONGOZO (1972) kwa nia na malengo ya kufanikisha lile Azimio la Arusha kujenga Ujamaa, kuimarisha Siasa ya Kujitegemea kama Taifa na kushirikisha wananchi katika uamuzi wote kwa maendeleo yao wenyewe.

 

Hivyo, “decentralization” ilikuwa na maana ya kupeleka madaraka kwa wananchi wilayani na mikoani. Ni nadharia safi sana inavutia. Lakini utekelezaji wake ndiyo ulioleta mmomonyoko hasa wa ule utawala bora uliokwishajengeka katika Jamhuri hii.

 

Mimi katika imani yangu ya Kikristo tunao usemi wa Kiingereza usemao, “THE END NEVER JUSTIFIES THE MEANS” maana yake, “Lengo la jambo halihalalishi njia zinazotumika kulifikia”.

 

Njia zikiwa mbovu, kandamizi au za ki-imla, basi lengo au shabaha iliyolengwa hata ikifikiwa, huwa haina uhalali wowote. Inakuwa batili.

By Jamhuri