Mwaka 1980 Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) , walikuwa na Mkutano wao Mkuu wa Chama katika jeshi. Mkutano ule wa kihistoria ulisimamiwa na Kamisaa Mkuu wa JWTZ na ambaye alikuwa katika Sekretarieti ya Chama – upande wa Oganaizesheni, Hayati Kanali Moses Nnauye, akisaidiwa na kada wa chama, Luteni Jakaya Kikwete Makao Makuu ya Chama.

Katika mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Urafiki, Dar es Salaam, Mwalimu alitamka kitu mimi nakisifia hadi leo.


Katika ufunguzi wa mkutano ule, Amiri Jeshi Mkuu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliungama kwa wanajeshi kwa maneno haya, namnukuu; “Ni kwamba nadhani sasa hivi Tanzania tusichokuwa nacho katika maeneo mengi, na ambacho sasa lazima kabisa tuamue kuwa nacho ni kile ambacho wenzetu wanakiita ‘professionalism’”. Ni kule kutenda kazi yako kiufundi na kuonea fahari sana kazi yako unayoitenda. Kwa sababu heshima yako iko ndani yake. Heshima yako mwenyewe iko ndani ya utendaji ule. Na kazi za ufundi zinazoitwa ‘professional’ zote ni za namna hiyo” (Nyerere: Jeshi Hodari Ufundi na nidhamu uk. 3).


Hapo sasa Mwalimu anakiri utaalamu katika kazi ni muhimu. Basi, katika utawala walikuwapo watu enye ujuzi wa kutawala (administrative officers) katika ngazi sita tofauti. Daraja la VI ndiyo hao tunaowaita maofisa utawala wapya kutoka vyuoni (interns), baada ya uzoefu fulani wanapanda kufikia daraja la V na hivyo hivyo hadi wanakuwa magwiji katika mambo ya utawala wa sheria na wa haki wanapokuwa katika daraja la II na la I.

 

Cheo hiki ndiyo hao waliokiita Makatibu Wakuu, na wasaidizi wao wakiitwa Makatibu Wakuu Wasaidizi (PAS yaani Principal Assistant Secretary daraja la II au la I) walijua “General Orders”, “Financial Regulations” na kanuni zote za utumishi “Establishment Circulars”. Kwa mtu wa aina ile akiwa Katibu Tawala Mkoa au akiwa Katibu Tawala Wilaya, alijua anachokifanya kwa uendeshaji wa Serikali kiutawala bora. Kulikuwa na Chuo cha Mzumbe, Serikali ilikijenga mahsusi kuwafundisha hao maafisa utawala – mabwana shauri.


Baada ya kuacha kufuata mfumo huo wa utawala bora, mtu wa utawala aliweza kurukwa kicheo na mteuliwa kisiasa. Mathalani, ofisa mambo ya ushirikiano wa kimataifa (career diplomat grade I) anarukwa na mwanasiasa anayeteuliwa kuwa balozi na yule mwenye ujuzi wa kimataifa anasota kama mshauri tu. Hapo patakosa manung’uniko?


Vigezo vipi vimetumika kumruka huyu mtaalamu wa ushirikiano wa kimataifa kama si kigezo kile kimoja tu cha siasa? Alikuwa na wadhifa kichama akakosa (ubunge), sasa akale wapi mwenzetu huyu? Katika ile orodha ya “seniority” katika “Staff List” inaonesha tarehe ya kuzaliwa, tarehe ya kuajiriwa, kuthibitishwa kazi, kupandishwa cheo cha sasa, stahiki zake na kadhalika. Kwa mwanasiasa vitu hivyo havioneshwi –  panaachwa wazi. Hapo ndipo chanzo cha tatizo.

 

Kwa vile utaratibu mzima umevurugwa kwa makusudi, basi kelele za utawala mbovu au upendeleo au undugunaizesheni ingawa zinakera na kusikika kila kukicha na hazibadilishi utawala kuwa bora.


Upo usemi kuwa kelele za mpita njia hazimkoseshi mwenye nyumba kupata usingizi au kelele za chura kisimani hazimzuii ng’ombe kunywa maji kisimani. Wanasiasa ndiyo wenye nyumba wanaoendelea tu kuendesha nchi hii kwa mazoea yaliyopo. Huku nchi ikiwa haina utawala bora. Maofisa utawala wazoefu au wanadiplomasia wazoefu wanagandishwa wakati wanasiasa, ndugu na marafiki wanapeta tu!


Wazee wengi kama mimi tuliozoea enzi zile za utawala bora na wa sheria kumalizia barua zetu kwa maneno kama “your faithful servant” au “I am, your obedient servant”- tunabaki kutazama tu haya yanayotokea katika utawala wa siku hizi.


Barua zinamaliziwa kwa maneno “wako ndugu katika utumishi au chama!” Lakini kuvunjika kwa koleo si mwisho wa uhunzi.


Hivyo tunapaswa kuirehemu ile koleo iliyovunjika au mpini uliokatika na tuendelee na kazi yetu ya uhunzi jamani. Sivyo?   Tunafanyaje basi? Kwanza kabisa nadhani Serikali ikishajitafiti na kuona pengo kubwa lililopo la ukosefu wa maofisa utawala, ijiridhishe hivyo na ianze kufunza maofisa utawala.

 

Ni muhimu sana kila wilaya, mkoa, idara, kuwa na aina hii ya watawala kuendesha Serikali ya haki na ya sheria. Bila kuwa na kada namna hiyo wale ma-DAS na ma-RAS wenye ujuzi na uzoefu wa kanuni za utawala bora hapatakuwa na utawala bora. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema, namnukuu tena; “Na kinachotuwezesha kufanya kazi pamoja ni utaratibu: kuna utaratibu unaotusaidia kufanya kazi…” (Nyerere akiongea na wanajeshi Ukumbi wa Urafiki Septemba 16, 1980 uk 7 ibara ile ya kwanza). Sasa huo utaratibu ndiyo ule niliosema huko nyuma ulikuwapo katika msahafu wa utumishi serikalini – yaani General Orders.


Kazi bila utaratibu maalumu ni fujo! Turejee kwenye utaratibu wa utumishi serikalini. Watumishi wote wafuate utaratibu namna moja. Chukua mfano mdogo tu wa mafao kwa wastaafu. Agizo la Serikali linawaweka watumishi katika makundi mawili tofauti. Watumishi wa kawaida “civil servants” na watumishi wa kisiasa “political officers” wenye kushikilia madaraka ya kisiasa mfano mawaziri, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, wanatendewa tofauti na watumishi wa Serikali – makatibu wakuu, ma-RAS, ma-DAS, ma-DAPO na kadhalika.


Mifano hai Sheria ya Mafao ya Uzeeni inaonesha mafungu tofauti. Enzi za ukoloni ilikuwapo sheria inayojulikana kwa watumishi wote ikiitwa “The Pensions Ordinance of 1954”. Kila mtumishi wa Serikali aliyestaafu alilipwa mafao yake kwa mujibu wa sheria ile. Na waliostahili kulipwa walikuwa ni watumishi wale tu walioajiriwa kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa kudumu “Permanent and Pensionable Terms” ambao masharti yao yaliwekwa bayana katika “General Orders” na pia rekodi zao zilikuwa katika “Seniority list” ya watumishi.

 

Sasa kumekuja sheria ya mafao inayoitwa The Public Service Retirement Benefits Act, No. 2 of 1999. Humo kuna utaratibu wake kwa watumishi wa umma (serikalini na mashirika ya umma).

 

Halafu kuna mafao maalumu kwa wanasiasa (wabunge, mawaziri, ma- RC, ma-DC, viongozi wa siasa) wamejiwekea stahiki zao. Ipo sheria yao inayojulikana kama “The Political Pension Benefits Act No. 3 ya mwaka 1999”. Sheria hii ina marupurupu kama haya; (i) mafao ya uzeeni (Pension) (ii) kiinua mgongo (gratuities) (iii) kifunga ofisi (Winding up allowances) na (iv) mengineyo (Contingencies). Hapo viongozi wa siasa wanajipangia asante zao za kuridhisha.

 

Mtazamo wangu ni kuwa kwa nini nchi kama yetu raia wote ambamo tunaitana ndugu, tunawekewa mafao kimatabaka? Jambo namna hii halioneshi nia ya utawala wa haki na wa sheria kwa watumishi wote.   Matabaka ni alama ya utawala wa kibepari.


Tukiweza kujitambua kitaifa upungufu wetu hapo ufumbuzi wa kweli wa utawala wa nchi hii unaweza kupatikana. Haki sawa kwa wote ni kaulimbiu ya chama kimoja cha siasa hapa nchini. Na nguvu ya umma ni kaulimbiu ya chama kingine cha siasa hapa hapa nchini. Uhuru na umoja ni kaulimbiu pia ya chama cha siasa hapa nchini. Kaulimbiu zote kwa umoja wao zinalenga kuwapo kwa utaifa wa nchi yetu.

 

Ili utaifa huo ujengeke lazima pawe na haki, pawe na mshikamano na pawe na umoja – Taifa litasonga mbele. Turejeshe haraka iwezekanavyo imani kwa wananchi ya Serikali yenye kujali wananchi wake na hivyo kuwa na utawala bora na wa sheria. Waandaliwe maofisa utawala kuendesha ofisi za Serikali. Utaratibu wa kufuata msahafu wa “General Orders na Financial Regulations” urejeshwe serikalini.

 

Serikali kupitia chama kinachotawala ijishughulishe na sera (policy), lakini isimamie utekelezaji wa hizo sera zake kwa mujibu wa sheria za haki na kanuni za utawala bora.


Utumishi (Civil service) usivunjwe ubaki na utaratibu wake ule ule wa kutoa huduma bora kwa raia (The civil service should remain intact) kama utaratibu ulivyo katika msahafu wa Serikali (General Orders) kutoingilia kanuni za utumishi, kuwapa maofisa utawala nafasi ya kutumia ujuzi wao (Professionalism) kujenga utawala ulio bora na wa haki na wa kufuata sheria, nchi ya Tanzania itarudisha heshima yake ile ile kama ya miaka ya zamani pale mataifa mengine yalipotuheshimu, yalipotujali, yalituogopa na hata yalikuja kujifunza utawala bora wa nchi hii.


Mahali hadi sasa mataifa mbalimbali bado wanatukiri kwa ubora na utaalamu ni katika majeshi yetu na katika mahakama. Kwa nini? Ni vile katika majeshi na mahakama taratibu zingali zinafuatwa na nidhamu ya utendaji iko juu, hasa jeshini.


Mwalimu kwa kuamini Watanzania wake aliwahi kutamka,” inawezekana, timiza wajibu wako” (Nyerere: Bungeni tarehe 12 Mei 1964).  Ndipo ningali najiuliza, je, Watanzania tuliteleza wapi? Kukosea ni tabia ya kila binadamu, lakini kurejea kosa lile lile mara kwa mara ni upumbavu.

 

Warumi wa kale wakisema na nukuu Kilatini hicho, “errare humanum est, sed perseverare in errore stultitia est”. Hivyo kuendeleza makosa kulikuwa kunalaumiwa tangu kale. Tanzania sasa tujirekebishe kupata utawala bora, wa haki na wa kufuata sheria – Hii itatuimarishia amani na umoja wetu kitaifa. Tujisahihishe!


Brigedia Jenerali mstaafu Francis Mbenna anapatikana katika simu 0715 806758. Alikuwa mwalimu wa sekondari na Afisa wa JWTZ. Ni mwanahistoria na ameandika kitabu cha HISTORIA YA ELIMU TANZANIA toka 1892 hadi sasa (Dar es Salaam University Bookshop).


 

By Jamhuri