DAR ES SALAAM
NA CLEMENT MAGEMBE
Wafanyabishara katika Soko Kuu la Kariakoo jijini Dar es Salaam wameiomba Serikali kuweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara wote nchini wapate fursa kubwa ya kuitumia Bandari ya Dar es Salaam, badala ya kuikimbia.
Wafanyabiashara hao wamelieleza JAMHURI kuwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwamba kama mazingira mazuri ya biashara yataandaliwa yatatoa fursa kwa wafanyabiashara wadogo na wakubwa kuagiza kwa wingi bidhaa kutoka nje ya nchi.
Justine Massawe (JB), mmiliki wa duka la nguo lililoko katika Mtaa wa Agrey Kariakoo amesema kwa kuwa hakuna utaratibu maalumu uliowekwa na serikali katika ukusanyaji wa kodi ndio chanzo cha Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kubadilisha kodi bila kuwashirikisha walipaji.
Massawe amesema taratibu mbovu za ukusanyaji wa kodi hasa katika uondoaji wa mizigo bandarini nazo zimechangia kuwakatisha tamaa wafanyabiashara nchini kuingiza mizigo yao kupitia bandari ya Dar es Salaam.
Amesema kikwazo kingine ambacho kimewakatisha tamaa kuendelea kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi ni kucheleweshwa kwa makusudi na maofisa wa TRA ambao wamekuwa wakidai kuwa mfumo (system) unasumbua kwa lengo la kuongeza mapato ya ziada.
“Mimi nilikuwa naingiza mzigo kutoka nje ya nchi kwa kulipia kodi ya sh milioni 60 kwa kontena moja, na nilipoleta mzigo wa aina ile ile na ukubwa kontena unaofanana na ule wa mwanzo nilikadiriwa kodi ya sh milioni 119.
“Ilinilazimu kwenda benki na kukopa kiasi hicho cha fedha ili kulipia kodi hiyo. Hadi sasa sijarudisha fedha ya benki na mzigo nilioingiza sijauza hadi sasa na biashara ya kuingiza bidhaa kutoka nje ya nchi nimeachana nayo,” amesema Massawe.
Mfanyabiashara huyo amesema kutokana na utitiri wa kodi kwa mfanyabiashara wa Tanzania anaweza kufanya biashara hata nchi kama Sudan, hali hiyo imewakatisha tamaa kuendelea kuingiza bidhaa kutoka nje ya nchi na wengi wao wamekijikita katika kazi nyingine.
“Wale niliokuwa nawafahamu kuwa ni waagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi hawaendelei kabisa na shughuli hiyo, wengine wamekuwa wamachinga wanaokwenda kununua bidhaa nchini Uganda na kuzileta hapa,” amesema.
Amesema TRA wanapaswa kujikita kwenye utaratibu unaoeleweka wa ukusanyaji wa kodi kwa uwazi badala ya utaratibu unaotumika sasa wa ukadiriaji na mfanyabiashara asitwishwe mzigo wa kodi kwa uzembe unaofanywa na watumishi wa Mamlaka hiyo.
Pamoja na hayo amesema Serikali na TRA walipaswa kuangalia mfumo wa kodi elekezi sambamba na ule uliofanyiwa utafiti baada ya kuwashirikisha wadau mbalimbali zikiwemo taasisi za serikali na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Tanzania (JWT).
Amesema Serikali kupitia TRA wameshindwa kuleta mkakati mzuri wa ukusanyaji wa kodi kwa wafanyabiashara wakubwa na wadogo na kusababisha kundi kubwa la wafanyabiashara wadogo wanaopanga biashara zao chini kutolipa kodi yoyote na hivyo mapato mengi kupotea.
Kwa upande wa biashara amesema wateja walionao ni wale wale na wanazidi kupungua kila siku kwa sababu ya bughudha wanazokutana nazo baada ya kununua bidhaa mbalimbali katika Soko la Kariakoo.
Amesema askari polisi nao wamegeuka kuwa maofisa wa TRA wakikataa hata risiti wanazoonyeshwa na wanunuzi kwamba hazilingani na kiasi cha mzigo ulionunuliwa.
Amesema kwa nchi za Uganda na Kenya polisi hawana utaratibu wa kuwabughudhi wafanyabiashara au wanunuzi wa bidhaa kwa kuwa wanathamini sana biashara tofauti na hapa nchini.
“Suala hili tumeliripoti TRA lakini bado linaendelea hadi sasa na hicho ndio chanzo cha wateja wetu kutoka nje ya nchi kuacha kuja katika soko hili kununua bidhaa… Hali ni mbaya sana, watu wamepungua sana katika soko hili. Miaka michache iliyopita mizigo ilikuwa inajaa katika mitaa yote ya soko, lakini kwa sasa yanashushwa mabelo matatu ya nguo.
“Wengi wameacha kuingiza mizigo yao nchini na inayopita kwa wingi ni ile inayosafirishwa kuelekea nchini Uganda, hivyo wateja wamehamia Msumbiji, Kenya na Afrika Kusini,” amesema.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Sylvester Kiondo amesema matatizo yanayowakabili wafanyabiashara nchini likiwemo suala la kodi yanaeleweka, lakini wataanza kuyashughulikia baada ya kuundwa na kuitambulisha Bodi ya Jumuiya hiyo.
Mwenyekiti JWT aliyemaliza muda wake, Johnson Minja amelieleza JAMHURI kuwa serikali iweke utaratibu mzuri wa kukusanya kodi kupitia taasisi yake ya TRA badala ya utaratibu unaotumika sasa kwa kila taasisi kujiingiza katika kazi ya ukusanyaji wa kodi.
Minja amesema kinachowatesa wafanyabiashara wengi nchini ni wingi wa kodi ambazo ni zaidi ya 38 ikiwemo kodi ya huduma (service levy) ambayo bado inatozwa na halmashauri wakati huo huo ikiendelea kutoza ushuru wa taka, kodi za mabango na usafi.
“Tunatozwa kodi hii ya huduma wakati tunaendelea kulipa kodi nyingine pamoja zile zinazotozwa na taasisi karibu zote za serikali, hali hii hailengi kumthamini mfanyabiashara wa hapa nchini.
“Wakati biashara zinakufa, TRA wanasema mapato yameongezeka, hapa tunajiuliza haya mapato wanayapata wapi? Na kwa biashara gani wakati zinakufa kila kukicha?” amesema.
Amesema kwa nchi za Kenya na Uganda mtu akilipa kodi mara moja kwenye mamlaka ya serikali halipi tena sehemu nyingine wala mnunuzi wa bidhaa kubughiwa na polisi kama ilivyo hapa nchini.
Amesema kwa sasa polisi wanakusanya kodi, madalali wanatumika kukusanya kodi, TRA, halmashauri, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na taasisi nyingine za umma na utaratibu huu umekuwa mzigo mkubwa sana kwa mlipa kodi wa nchi hii.
Amesema Rais John Magufuli aliahidi wakati wa kampeni kwamba akiingia madarakani atapunguza utitiri wa kodi wafanyabiashara nchini, lakini bado suala hilo halijafanyika ingawa ana nia njema na Watanzania.
“Rais Magufuli ni kiongozi mzalendo kwa nchi. Anapenda wafanyabiashara na Watanzania kwa ujumla tuwe na maendeleo kwa kukuza uchumi wa nchi, na kinachoonekana wasidizi wake hawampi ushauri unaotakiwa.
“Kwa sasa bandarini wizi wa kutorosha mizigo umekomeshwa, reli inajengwa ambayo itakuwa kichocheo kikubwa cha uchumi wa nchi yetu na hizo zote ni jitihada nzuri za Serikali,” amesema.
Amesema kabla ya uhuru uchumi wa nchi ulikuwa unashikiliwa na wageni na baada ya uhuru Serikali ilikuwa imejiingiza moja kwa moja kwenye biashara huku tukipambana na maadui watatu ujinga, maradhi na umaskini.
Pamoja na kufanya biashara, Serikali ilijitahidi kujenga shule na hospitali za umma na Awamu ya Pili nchi iliingia kwenye uchumi wa soko ambao si soko huru.
Minja ambaye kwa sasa ni mshauri JWT, amesema baadaye nchi iliingia katika uchumi uliolenga ujasiriamali huku mapato makubwa ya serikali yakiwa yanategemea makusanyo ya kodi na hivyo mwaka 1998 ikaundwa TRA, lakini tatizo kubwa ni elimu kwa wafanyabiashara.
Hata hivyo, amesema kuweka utaratibu mzuri wa kukusanya kodi serikali ihusike moja kwa moja na ukusanyaji badala ya kuziachia baadhi ya taasisi zake kuendelea kuleta kero kwa wananchi wanaotakiwa kulipa kodi kwa uaminifu kukuza uchumi wa nchi.
8610 Total Views 8 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!