* DC atoa tamko kali, awaonya wavamizi

* Ataka wanunuzi wafuate kanuni, sheria

* Ashauri wenyeji wabakize ya kuwasaidia

* Mifugo yailemea wilaya, aipiga marufuku


Serikali katika Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, imewataka wananchi wawe makini katika uuzaji ardhi, kutokana na wimbi la Watanzania na raia wa kigeni wanaojitwalia ardhi kubwa wilayani humo.

 

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Ahmed Kipozi, amesema kasi ya wananchi wakazi wa wilaya hiyo kuuza ardhi imefikia kiwango cha kutisha, na amewataka wawe makini. “Kama mwananchi ana ekari mia moja, basi auze na kubakiza japo ishirini au thelathini kwa ajili yake na kwa kizazi chake.

 


“Suala hili (uuzaji ardhi) limekuwa kubwa sana kwa sababu Watanzania sasa wamejua thamani ya ardhi. Njia pekee ya kuwasaidia, pamoja na sisi upande wetu Serikali Kuu na Halmashauri ya Wilaya, ni kwa taasisi za fedha kuja kutoa elimu kwa wananchi.


“Taasisi za fedha zije, benki zije zitoe semina za kweli kweli ili wananchi wajue namna ya kuitumia ardhi yao, vinginevyo watauza ardhi yote na kuwaacha wao na vizazi vyao wakiwa masikini. Waje watoe elimu ya kukopa ili wananchi wakope, si kutoa elimu za ujanjaujanja na mwisho wa mwaka waseme fedha zimebaki benki kwa kukosa wakopaji,” amesema Kipozi alipozungumza na JAMHURI wiki iliyopita ofisini kwake mjini Bagamoyo, akiwa pamoja na Ofisa Ardhi Wilaya ya Bagamoyo, Josephine Gugu.


Kipozi amesema Wilaya ya Bagamoyo ina changamoto nyingi, na akazitaja baadhi kuwa ni ununuzi mkubwa wa ardhi, uvamizi wa ardhi/maeneo ya watu na maeneo ya Serikali, ujenzi holela, viwanja vya eneo la mradi wa viwanja Ukuni, na migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji.

Ununuzi mkubwa wa ardhi

Wilaya ya Bagamoyo ina ardhi nzuri ambayo ni kivutio kwa watu wengi nje na ndani ya nchi. Hii imesabibisha ununuzi mkubwa kufanywa; na baadhi kufanywa bila kufuata taratibu. Hii inatokana na utayari wa wenyeji kuuza maeneo yao bila kujali hatima ya familia zao kwa wakati uliopo na ujao. Ununuzi wa maeneo usiofuata taratibu katika vijiji na miji ndiyo chanzo kikubwa cha migogoro.

Taratibu za ununuzi wa ardhi vijijini

Kipozi amesema ununuzi wa ardhi unapaswa kufanywa kwa kufuata sheria zilizopo. Amesema kwa sasa kuna watu wengi wanaoingia vijijini na kununua ardhi ambazo zipo kwenye miliki nyingine kisheria. “Lazima kuwe na uwazi katika manunuzi ya ardhi mijini na vijijini. Msimamizi wa ardhi katika ngazi ya kijiji ni Halmashauri ya Kijiji na Afisa Mtendaji ndiye mhusika mkuu.


“Kabla ya kununua kipande cha ardhi ni lazima ufanye utambuzi wa eneo husika kwa kushirikisha majirani na uongozi ngazi ya kitongoji. Hii ni kwa sababu kitongoji si serikali, bali Mwenyekiti wa Kitongoji ndiye anayeunda Serikali ya Kijiji kwa sababu yeye ni Mjumbe Serikali ya Kijiji (Halmashauri ya Kijiji).

 

“Ngazi ya kitongoji si watendaji katika mauziano ya ardhi, bali mashahidi tu. Baada ya utambuzi wa eneo, matangazo yatolewe na kubandikwa katika mbao za matangazo kuanzia ngazi ya kijiji, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya, Idara ya Ardhi na Ofisa Kata na litadumu kwa muda wa siku ishirini na moja.

 

“Baada ya muda huo Afisa Mtendaji wa Kijiji ataridhia mauzo hayo kama hakuna pingamizi lolote lililotolewa. Nasisitiza kwamba kila anayetaka kununua au kumilikishwa ardhi Wilaya ya Bagamoyo afuate taratibu na sheria kama zilivyoainishwa. Aidha, familia kabla ya kuuza ardhi watafakari hali yao na mahitaji yao kwa vizazi vya leo na kesho,” ameasa.

Uvamizi wa ardhi

Kipozi amesema uvamizi wa ardhi katika Wilaya ya Bagamoyo unahusu maeneo ya watu binafsi, taasisi na ya serikali.

 

“Kuna maeneo mengi sana ambayo yameachwa bila kuendelezwa kwa muda wa miaka mingi. Hii imesababisha mashamba haya kuwa mapori na kufuga wanyama hatarishi kwa wanadamu. Maeneo haya yamekuwa vivutio vikubwa kwa wavamizi. Hata hivyo, si sababu ya watu kuingia bila kufuata taratibu.


“Kutokana na sheria na taratibu za ardhi, Serikali inaweza kuyafuta au kuyachukua mashamba haya kwa sababu zifuatazo: Kwa manufaa ya umma (public or good cause), kuvunja masharti ya uendelezaji, kutokulipa kodi ya pango la ardhi kwa muda mrefu, kutokuendeleza eneo kwa muda mrefu, na kutelekeza (abandonment).

 

“Wananchi wanatahadharishwa kwamba wasivamie mashamba hayo kwani wanapofanya hivyo watakuwa wanavunja sheria. Aidha, itakuwa vigumu kuyachukua au kuyafuta. Serikali haitasita kufuta umiliki ambao umeshindwa kufuata taratibu,” amesema Kipozi.

Uvamizi maeneo ya Serikali

Mkuu huyo wa Wilaya ya Bagamoyo amesema kuna uvamizi wa maeneo ya Serikali unaofanywa na watu ambao, ama wanafanya hivyo makusudi au kwa kutojua kwa vile hawataki kufuata taratibu na sheria za ununuzi wa ardhi.

 

“Kwanza kabisa napenda ieleweke kwamba maeneo ya Serikali hayana ukomo wa muda. Aidha, Serikali haina hatimiliki kwa sababu yenyewe ni mmiliki na maeneo yake yanafahamika. Maeneo ya Serikali ni maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya miradi ya Serikali, shule, hospitali na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji na hifadhi (reserve land).

 

“Wilaya ya Bagamoyo ina maeneo matatu makubwa ambayo yametengwa kwa ajili ya uwekezaji. Eneo la EPZA ambalo linajumuisha vijiji vya Pande, Kondo, Mlingotini na sehemu za vijiji vya Kiromo na Zinga. Eneo hili limekwishatangazwa rasmi kuwa eneo la ukanda maalumu kwa ajili ya uwekezaji. Ukubwa wa eneo hilo ni ekari 10,000 na tayari fidia imelipwa kwa ekari 2,000.  Maeneo yaliyobakia yatalipwa kwa awamu kutokana jinsi fedha zitakavyopatikana.

 

“Eneo la pili ni eneo la RAZABA. Kirefu cha RAZABA ni ‘Ranch of Zanzibar in Bagamoyo’. Shamba la RAZABA limeanza kutumiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuanzia mwaka 1976 baada ya waliokuwapo katika eneo hilo kulipwa fidia. Kuna wachache ambao walikataa kupokea fidia zao, lakini hiyo haina maana kwamba eneo halikutwaliwa. Eneo lina ukubwa wa hekta 28,094 na limepimwa na limetengwa kwa ajili ya uwekezaji.

 

“Hivi karibuni kumekuwa na wimbi la kununua vipande vya ardhi katika eneo hilo. Inabidi ieleweke kwamba eneo la RAZABA ni la Serikali. Kwa yeyote anayedai umiliki wa kipande cha ardhi ndani ya shamba hili itabidi atoe ushahidi wa kutosha wa jinsi alivyolipata kutoka serikalini.


“Naomba wananchi wasiendelee kununua ardhi katika eneo hili, hususan Bigo na Makaani. Ukikiuka ushauri huu utakuwa umepoteza fdha zako bure.


“Hifadhi ya Taifa ya Saadani. Ardhi ni mali ya umma na mdhamini wake ni Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na anayo mamlaka kisheria kutwaa eneo lolote kwa manufaa ya umma. Eneo la Hifadhi ya Saadani lilitwaliwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo Novemba 5, 2004 kwa Tangazo la Serikali Na 281.

 

“Kutokana na sheria za hifadhi hakuna makazi yanayoruhusiwa ndani ya hifadhi. Serikali imekwishafanya tathmini ya mali zote zilizomo ndani ya hifadhi ya Saadani na kuandaa fidia stahiki. Baadhi ya wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi hii Kitongoji cha Uvinje wamekataa kutoa ushirikiano katika uthamini.

 

“Nawatahadharisha kwamba kukataa kuthaminiwa au kufidiwa hakuizuii Serikali kutwaa eneo lolote. Kwa taarifa hii wananchi wote walioko katika Kitongoji cha Uvinje waondoke mara moja kabla ya hatua za kisheria hazijachukuliwa,” ameonya Kipozi.

Viwanja vya Mradi wa Ukuni

Kipozi amesema Mradi wa Viwanja 3,000 Ukuni na Chalinze ulibuniwa na Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo mwaka 2005, baada ya kutokea kwa upungufu mkubwa wa viwanja vya makazi na matumizi mengine, uliosababishwa na kuongezeka kwa idadi ya watu wanaofanya shughuli mbalimbali mjini Bagamoyo na mikoa jirani, hasa Jiji la Dar es Salaam.

 

“Ili kukidhi mahitaji ya wananchi wa Bagamoyo na mikoa ya jirani, mradi huu ulibuniwa kuwa na idadi ya viwanja 2,500 Bagamoyo mjini na viwanja 500 Chalinze vyenye ukubwa tofauti na matumizi mbalimbali.

 

“Kutokana na Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kukosa rasilimali fedha, watu na vifaa vya upangaji, uthamini na upimaji wa viwanja ilifanya mradi huu kuwa mradi shirikishi ambako gharama za upangaji na upimaji wa viwanja hivyo zilichangishwa kutoka kwa wananchi na taasisi mbalimbali kulingana na mahitaji yao. Michango hii haikujumuisha thamani/fidia ya ardhi, majengo, mazao na maendelezo juu ya ardhi.


“Malengo ya mradi yalikuwa: Kupunguza ukuaji wa makazi holela kwa kuupanga Mji wa Bagamoyo na Chalinze kwa kupima na kugawa viwanja 2,500 Bagamoyo mjini na viwanja 500 Chalinze.


“Kuongeza thamani ya ardhi kwa kugawa ardhi iliyopimwa kisheria.


“Kuweka miundombinu kama barabara, umeme, maji na huduma nyingine za kijamii.


“Kupunguza/kuondoa urasimu katika upatikanaji wa viwanja, na kupanua wigo wa kodi kwa Serikali kukusanya maduhuli ya ardhi.


“Mradi huu bado ni endelevu ili kukidhi mahitaji ya viwanja kwa ajili ya wananchi waliolipia mwaka 2000/2005 na kwa waombaji wapya,” amesema.

 

Onyo kwa wanaojenga holela

Kipozi amesema ili kupunguza kasi ya ujenzi holela, Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo imeamua kushirikisha wadau katika kuongeza idadi ya viwanja vilivyopimwa.


“Kwa wakati huu Serikali inaandaa mpango mkakati kwa ajili ya maeneo ya Kerege na Mapinga ambayo yameiva kwa ajili ya shughuli za kimipango miji na maeneo ya Kingani na Kaole kwa upande wa Bagamoyo mjini. Aidha, kupanua eneo la kimipango miji katika Kata ya Chalinze na maeneo mengine ambayo yataainishwa hapo baadaye.

 

“Serikali inatoa onyo kwa wale wote ambao wana viwanja ndani ya maeneo ya mipango miji kama vile Bagamoyo mjini na Chalinze ambao wanajenga bila kufuata taratibu za ujenzi. Kwa lugha nyingine wamejenga bila vibali vya ujenzi, hivyo kujenga majengo ambayo hayakubaliani na uendelezaji mji. Serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi yao ikiwa ni pamoja na kubomoa maendelezo hayo.


“Hivi karibuni kumetokea mpango wa kujenga vijumba vingi ndani ya maeneo ya ujazo mkubwa yasiyo maeneo ya makazi makubwa (housing estates) kwa nia ya kupangisha. Maeneo ya ujazo mkubwa maana yake ni watu wachache. Taratibu hizi ambazo zinaonekana kushamiri ni vizuri zikakoma. Kama mtu anahitaji kujenga nyumba nyingi za kupangisha ni vizuri akajitafutia eneo lilotengwa kwa ajili hiyo au akaainisha nia yake mapema ili atengewe eneo stahili,” amesema Kipozi.

Migogoro ya ardhi

Mkuu huyo wa Wilaya anasema kwa kiasi kikubwa migogoro ya ardhi katika Wilaya ya Bagamoyo imepungua; na kwamba migogoro mingi iliyopo ni kati ya wakulima na wafugaji.


“Wafugaji wengi wanaotoka nje ya Wilaya ya Bagamoyo hawafuati taratibu na sheria za maeneo walikofikia. Wanakuwa na mifugo mingi ambayo inavamia mashamba ya wananchi waliowakuta. Kutokana na wingi wa mifugo, ardhi haitoshi kwa malisho na shughuli nyingine kama kilimo, hivyo mifugo huishia kuharibu mashamba ya watu na maeneo ya hifadhi. Tatizo hili ni kubwa, lakini Serikali inalitafutia suluhisho la kudumu,” amesema.


Wilaya ya Bagamoyo hadi Julai mwaka huu, ilikuwa na ng’ombe 235,814, mbuzi 84,998, kondoo 38,694, nguruwe 3,832, mbwa 7,966 na punda 315.  Amewahamasisha vijana kujitokeza kwa wingi kumiliki ardhi kwa njia halali na kuendesha shughuli za kilimo na ufugaji.


Amesema ufugaji wa kienyeji wa kuzurura na mifugo haufai kwa kuwa unaibua migogoro kati ya wafugaji na wakulima. Ameshauri ufugaji ufanywe kwa njia za kisasa au zinazoelekea kwenye ukisasa.

 

“Kwa wakati huu mifugo iliyopo Wilaya ya Bagamoyo imezidi sana, tunatahadharisha wafugaji wasiingize tena mifugo.

Natoa wito kwa yeyote anayetaka kuishi au kuwekeza wilayani  Bagamoyo asisite kufanya hivyo, lakini afuate taratibu, kanuni na sheria.


Karibu Bagamoyo, karibu uwekeze. Milango iko wazi,” amesema Kipozi.

 

2943 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!