Uwekezaji: Fursa ya kuichangamkia – (2)

Kukuza mtaji humpa mwekezaji nafasi ya kuwekeza zaidi katika shughuli nyingine za kiuchumi, kama kilimo

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Wiki iliyopita tulitazama namna ambavyo kampuni ya uwekezaji wa pamoja inayomilikiwa na serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango inavyofanya tathmini na utafiti wa kina kabla ya kuwekeza fedha zilizokusanywa. Endelea…

Tofauti ni nyingi, mwekezaji anaweza kusoma makala zaidi ya hii kwenye tovuti mbalimbali au kutembelea ofisi zetu, dalali wa masoko ya hisa, dhamana mbalimbali hata kwenye weledi mpana wa tasnia kama benki na taasisi nyingine za fedha. 

Meneja lazima awe mwangalifu kufuata kanuni husika, mfano kuhakikisha gharama za uendeshaji hazivuki kiasi kilichokubaliwa, uwekezaji unafanyika ndani ya maeneo yaliyokubaliwa na si vinginevyo.

Mwekezaji anaungana na wawekezaji wengine kuwekeza pamoja, hivyo kwa umoja huo mtaji huwa mkubwa unaowezesha kufanya mambo ambayo peke yake asingeweza kuyafanya.

Pia kuongeza nguvu na ufanisi kwenye majadiliano ambapo huo ni uwekezaji wenye tija. 

Masharti ya mfuko yanamwezesha mwekezaji kuingia na kutoka wakati wowote. Wawekezaji kwenye mfuko mmoja, mara nyingi huwa na lengo moja.

Mfano waliopo kwenye mfuko wa Wekeza Maisha hulenga kupata bima na kukuza mtaji, Mfuko wa Watoto huwa ni elimu na maisha baada ya shule kwa watoto. 

Lengo la mifuko ya Hati Fungani na Jikimu ni kupata gawio la mara kwa mara wakati Mfuko wa Umoja ni kukuza mtaji huku ukitarajia hisa zitakupa faida zaidi.

Pia Mfuko wa Ukwasi walau asilimia 10 hadi 14 au kutokana na rejesho kutoka sehemu kama akaunti za muda maalumu, hati fungani za mda mfupi au mrefu. 

Kipande kinaweza kupanda au kushuka, hili ndilo angalizo kuu. Ili kuanza kuwekeza si lazima uwe na fedha nyingi, kuanzia Sh 10,000 tayari unakuwa mwekezaji.

Siri ni kuendelea kuwekeza kwa mpango maalumu, mpango wako unaweza kuwa wa kila siku, wiki, kila mwezi au mwaka.  

Kwa mfano, asilimia 10 ya kila mapato yako yawe ya siku au mwezi, kwa wale walio na mtaji mkubwa anaweza kuwekeza kwa mkupuo mkubwa.

Si vibaya wakiongeza juu ya huo mkupuo kwa mpango maalumu, kwani haba na haba hujaza kibaba. 

Ulipaji kwa njia za mitandao mfano simu unarahisisha na kuokoa muda wa kwenda benki mara kwa mara, pia mwekezaji ataomba nakala ya uwekezaji wake wakati wowote.

Ni jukumu la meneja kumpa mwekezaji taarifa za uwekezaji wake pale anapohitaji. Mwekezaji anaweza akawa anavuna kutoka kwenye uwekezaji wake kwa mpango maalumu.

Si lazima akitaka fedha zake atoe zote bali atatoa kutokana na mahitaji yake, muda wowote anaweza kuongeza tena uwekezaji. 

Mwekezaji anaweza kujipangia alipwe kiasi fulani cha faida yake kila baada ya muda fulani, meneja atalipa kiasi hicho kwa akaunti ya mteja kwa muda muafaka.

Pia si lazima kuvuna faida, mwekezaji anaweza kuacha faida nayo ikawa sehemu ya uwekezaji, yaani faida ikaendelea kumpa faida.

Akiwa na shida au mahitaji fulani, Waswahili wana usemi unaosema, kimfaacho mtu chake, hivyo anaweza kutoa fedha kutoka kwenye akaunti yake ya uwekezaji vile apendavyo.

Ukifanya upembuzi yakinifu, utakuta uwekezaji wa pamoja ni fursa nzuri kwa maisha ya mbele.

Mwekezaji akiutumia vizuri uwekezaji wake utamsaidia kutatua changamoto mbalimbali na pengine kwenye maisha ya kustaafu.

Wakati wa kustaafu ni kama unaanzaukurasa mpya na wakati huo fedha ndiyo zinahitajika kwa wingi, hivyo uwekezaji wa pamoja unaweza kuwa pensheni mbadala au hata zaidi ya pensheni.

Mwekezaji lazima awe na malengo, mfano ni lini avune, apande mbegu mara kwa mara au mara moja, haya ni malengo ya kawaida kwenye biashara yoyote.

Mwekezaji ni mtu mwerevu, anatakiwa afanye tathmini ya athari zinazotokana na uwekezaji huo na sababu zipi zinafanya kipande kupanda au kushuka. 

Ni muhimu mwekezaji kumfanyia upembuzi meneja, kwani huyu ndiye baada ya makubaliano maalumu na ya kisheria utampa fedha zako awekeze kwa niaba yako, huku ukiendelea na shughuli nyingine. 

Meneja utamjua anaweza au hawezi kwa kuangalia utendaji wake, mfano je, anafikia malengo na vigezo vilivyowekwa na anavizidi kwa kiasi gani? 

Kwa mfano, kigezo kimojawapo ni asilimia ya chini ambayo mwekezaji anatarajia, je, anaifikia na kuizidi kwa kiasi gani, hii ni kila mwaka au?  

Pia vyeti vya meneja na wafanyakazi wake, jinsi walivyojipanga, utendaji wa meneja miaka 5-10 iliyopita.

Kawaida akaunti moja ni ya mtu mmoja, pia mnaweza kufungua akaunti ya kikundi, uwekezaji huu ni wa mtu, watu, taasisi zote, wakiwamo wafanyabiashara wadogo na wakubwa.

Ni rahisi na salama kwa asilimia kubwa ukilinganisha na uwekezaji mwingine wowote. Hii inatokana na muundo wake, pia unatoa nafasi kwa mwekezaji kumwandika mrithi wake kama litatokea la kutokea huko mbele. 

Unaruhusu mlezi au mwangalizi kumwekezea mwenye umri chini ya miaka 18, akifika wakati huo humkabidhi kilichopo na akaamua kuendeleza au kufika ukomo.

Kumbuka kuwekeza na kutoa fedha ni rahisi. Ukishakuwa na akaunti unaweza ukawa unawekeza kwa simu wakati wowote.  

Chukua hatua, jiulize kwa nini niwekeze? Hii itasaidia kufanya tathmini kwa kulinganisha faida na athari kama ungeamua kuwekeza sehemu nyingine mbali na kwenye uwekezaji wa pamoja.  

Tathmini hii iendane na malengo yako, muda, athari na faida tarajiwa. Malengo yatakupa kigezo cha mfuko upi uwekeze kwa kuangalia mfuko husika unawekeza wapi.

Mfano, muda ukiwa mrefu sana mfuko wenye hisa kama sehemu yake ya uwekezaji unaweza kutumika, ila kama ni ya muda mfupi, mfuko wenye kuwekeza zaidi ya asilimia 90 kwenye hati fungani utafaa zaidi.

Hizi ni tathmini chache tu. Mwekezaji anashauriwa kupata elimu ya kutosha kabla ya kufanya uamuzi na elimu kama hii hutolewa bure na UTT AMIS. 

Kwa maneno mengine ni vizuri Watanzania wakajipanua zaidi, kufanya uwekezaji kisasa. Ukiwa hauna pesa nguvu zako ndiyo mtaji.

Kama huwezi kujiajiri lazima uwe mtumwa, yaani uajiriwe, ukiwa na fedha zako zinakufanyia kazi.

Pamoja na uwekezaji wa pamoja, kuna huduma kama usimamizi wa mali/ fedha uwekezaji wa mteja.

Huduma hii ni nzuri, pia ni njia ya kisasa kwa mwekezaji kumpa msimamizi fedha zake awekeze kwa ajili yake, yaani mwekezaji anampa meneja msimamizi mali huku akiratibu huduma mbalimbali kama wapi ziwekezwe, ushauri wa kodi.

Msimamizi hawekezi tu bali anakuwa ndiye bwana ushauri kwa mwekezaji, huku akifanya tathmini ya hali halisi sokoni, mfano kuangalia uwezekano wa kukwepa dhoruba za uwekezaji, kuhakikisha faida zinapatikana. 

Hapa mwekezaji anaweza kupata huduma kama usimamizi wa mali zake huku ukipata ushauri wa kitaalamu jinsi ya kuongeza uwekezaji wake kwa faida.

Katika huduma ya usimamizi wa mali, meneja ataangalia mtawanyo wa mali za mwekezaji, bajeti ya mwekezaji, hesabu zake, kodi, hata bima husika. 

Jukumu la meneja litakuwa kuhakikisha mali zinazoshikika na zisizoshikika zinawekezwa kwa ufanisi wa hali ya juu ili kuleta mapato ya juu kabisa. 

Huduma hii ya usimamizi wa mali mara nyingi inalenga mashirika kama ya pensheni na watu wenye fedha nyingi. 

Kwa wale wenye fedha kidogo wataanza kwenye uwekezaji wa pamoja, wakichanganya na shughuli zao zingine ili kukuza mtaji ambao baadaye utawapa uwezo wa kuingia huko.

Kwa mtu au taasisi wakichagua kuweka meneja, lengo ni kuwa meneja huyo ataleta tija zaidi. 

Kuna mambo makubwa mawili mwekezaji anatakiwa kuyafahamu, kwanza nafasi ya meneja kwenye uwekezaji wake, pili mikakati ya meneja kuongeza rasilimali husika. 

Meneja atawekeza wapi, umuhimu wa hili ni kuwa utapata kubashiri faida au hasara, kwani kama meneja anawekeza kwenye kampuni ambazo hazisimamiwi vizuri na hazina biashara ya kutosha hivyo kuleta hasara. Kumbukumbu na nyaraka zote za uwekezaji lazima ziwekwe vizuri.