MpangoNafanya kazi kwenye sekta ya utalii kwa muda sasa; kwenye utalii unaotambulika kama utalii wa utamaduni na ingawa kuna masuala mengi bado najifunza kuhusu sekta hii kwa ujumla, naamini nimejifunza vya kutosha kuweza kuchangia mawazo yangu juu ya uamuzi wa Serikali wa hivi karibuni wa kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani (nitaiita KOT kwa kifupi) kwa tozo za huduma kwenye sekta hiyo.

Machozi ya wadau wa sekta ya utalii juu ya uamuzi huu wa upande mmoja wa serikali yana ukweli, wala siyo machozi ya uongo. Nayaita maamuzi ya upande mmoja kwa sababu inaelekea kuwa serikali haikutafuta maoni ya wadau husika.

 Athari ipo, lakini labda kwa muda mrefu tutakuwa tunabishana kuhusu ukubwa wa athari hiyo. Kwanza, ni kweli kuwa mawakala wa safari za utalii hupanga safari za wateja wao kwa muda mrefu ujao. Nimekuwa nafanya mazungumzo na wakala wa kuongoza watalii kutoka Ubelgiji ambaye alianza kupanga safari za kuleta wageni Tanzania miaka miwili iliyopita na hatimaye alileta wageni wachache miezi michache iliyopita.

Huyu wakala atakuwa amewatangazia wateja wake gharama za safari iliyojumuisha kutembelea vivutio kadhaa nchini Burundi na Tanzania na bila shaka atakuwa amechapisha matangazo na vipeperushi vikibainisha hizo bei na misafara iliyomo. Na ni hakika kuwa wateja wake wanamlipa pesa mapema sana kabla ya kuanza safari. Mimi mshirika wake wa Tanzania nikimwambia kuwa nadai asilimia 18 ya KOT juu ya gharama ambazo tayari nilishampelekea, hatanielewa. Na ni kweli kuwa niking’ang’ania sana alipe hilo ongezeko anaweza kuamua kuwashauri wageni wake watembelee Kenya badala ya Tanzania. Tembo wa Kenya hatofautiani na tembo wa Tanzania. Na tunafahamu pia watalii wengi wanavutiwa kutembelea Kenya ili kuuona au kuukwea Mlima Kilimanjaro.

Lakini swali moja muhimu ambalo halijaulizwa kwenye malumbano haya ni hili: kama mimi kweli nathamini uhusiano wangu wa biashara ya wageni kutoka Ubelgiji, ni kweli upo ulazima wa kumbebesha ile KOT yule mshirika wangu?

Si kweli kuwa mimi mwenyewe, kwa madhumuni ya kujenga uhusiano mzuri wa biashara ya muda mrefu na mshirika wangu, ningeweza kulipa toka mfukoni mwangu dola 118 kwa kila dola 1,000 ambazo nimepokea?

Nikimbebesha ile asilimia 18 halafu akatafuta mshirika mpya Kenya ambaye ataendelea kufanya naye biashara kwa miaka 20 ijayo, hasara haitakuwa ya Serikali ya Tanzania tu, bali hasara kubwa zaidi itakuwa yangu.

Serikali ya Tanzania ikikosa kodi kwenye utalii itatafuta vyanzo vingine vya kuwakamua raia wake kwenye maeneo mengine na, mimi huyo huyo, ambaye tayari nimekosa mapato kutoka Ubelgiji, naweza kujikuta nimekamuliwa tena kwenye eneo ambalo hata haliniingizii kipato chochote.

Nimejifunza pia kuwa biashara ya utalii inatoa fursa kwa wadau wake kupata faida nzuri tu, na ndiyo maana sikubaliani sana na malalamiko lukuki yaliyotolewa dhidi ya uamuzi huu wa Serikali. Wafanyabiashara siku zote huambiwa kuwa wao ni wadau muhimu sana wa maendeleo, na hilo ni kweli, lakini kusema hivyo sana kunajenga imani kuwa wao ndiyo kila kitu na kila kitu ni wao.

Wamezoeshwa kula keki iliyokolea sukari ya vijiko kumi, na ile sukari inapotolewa ghafla bila samahani, basi wanahisi kama wamevunjiwa heshima.

Lakini kwa mtazamo huo wanajifumba macho na kukinga fursa ya kuangalia njia muafaka ya kugeuza tatizo kuwa fursa.

Kitendo cha kumbebesha tozo mpya mteja ni kitendo chenye mazingira ya mfanyabiashara ambaye anafanya biashara ya papo kwa papo. Lakini biashara ya utalii si ya papo kwa papo, ni biashara ya muda mrefu ya wadau wanaojenga uhusiano wa muda mrefu na wateja wao. Kama mteja ananiletea dola 10,000 kila mwaka, nitakuwa tayari kumlipia dola 1,800 mwaka huu na kumpa taarifa kuwa kuanzia mwakani atalipa dola 11,800. Na kwa faida inayopatikana kwenye huduma za biashara ya utalii, hili linawezekana kabisa.

Pamoja na shutuma hizi dhidi ya wadau wenzangu wa sekta ya utalii, sina maneno mazuri sana ya kusema juu ya uamuzi huu wa Serikali. Kwa kutamka kuwa wafanyabiashara ni wadau wakuu wa maendeleo Serikali inapaswa kufanya uamuzi ambao hauathiri mno shughuli za wafanyabiashara, si tu kwenye utalii, bali hata kwenye sekta nyingine.

Serikali ingeweza kutamka kuwa inakusudia kuongeza KOT kuanzia bajeti ya 2017/2018, na kupunguza visingizio kwa wadau wa sekta ya utalii kufanya shughuli zao kwa ufanisi.

Wafanyabiashara wanayo nguvu kubwa ya kuunga mkono au kuhujumu kazi za Serikali. Haya tumeyaona kwenye suala la sukari kuadimika na kupanda bei hivi karibuni baada ya Serikali kuongeza udhibiti kwenye mchakato wa uagizaji kutoka nje, pamoja na uamuzi wa Bodi ya Sukari kutoa bei elekezi ya sukari.

Mara chache tunaposikia baadhi ya marais wetu kuzungumzia kazi ya kuongoza nchi huwa tunasikia kuwa ni kazi ngumu. Ni kazi ya kumkosesha rais usingizi kila wakati. Kama tumewahi kupata rais ambaye anachapa usingizi Ikulu bila wasiwasi wowote, basi hiyo itakuwa kasoro kubwa sana. Tulimsikia Mwalimu Nyerere akisema kuwa kazi ya urais siyo lelemama. Rais Magufuli naye ametamka kuwa si kazi rahisi. Na ugumu pia umeongezeka kwake baada ya misaada kwa Tanzania kutoka nchi hisani kupunguzwa kutokana na matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar.

Napenda kuamini kuwa Rais Magufuli alitafakari kuwa kati ya kumuudhi mtalii ambaye ana maisha mazuri tu na anaweza kuamua kusafiri kwenda Kenya badala ya kutembelea Tanzania kwa sababu ya kubebeshwa KOT, na kati ya kuhakikisha kuwa mapato ya kodi yanakusanywa kiasi cha kutosha na kuhakikisha kuwa masikini Mtanzania anapata huduma za maji, afya, na nyingine muhimu aliona ni bora amuudhi mgeni.

By Jamhuri