ijmc

Miili yetu hutegemea vyanzo viwili vya nguvu ambavyo ni oksijeni na vyakula. Oksijeni huingizwa ndani ya miili yetu kupitia pumzi na kuingia moja kwa moja katika utendaji, wakati chakula hutakiwa kupitia mchakato mrefu kuweza kutumiwa na mwili.

Muundo na mchakato huu huitwa mfumo wa usagaji chakula ambao ni tumbo (mfuko wa chakula), utumbo mdogo (utumbo mwembamba), utumbo mpana (utumbo mkubwa), kibofu nyongo, ini na kongosho. Tatizo lolote katika viungo hivi huweza kusababisha mwili wote kuugua.

 

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), watu zaidi ya milioni sita duniani hufa kwa matatizo mbalimbali yanayotokana na mfumo wa viungo vya usagaji chakula. Vidonda vya tumbo ikiwa ni mojawapo, ni mmomonyoko katika kunyanzi za tumbo, sehemu ya mwanzo ya utumbo mdogo (duodeni), au umio (koromeo). Ugonjwa huu huua asilimia nne ya watu duniani.

 

Kwa hakika, vidonda vya tumbo ni ugonjwa ambao sasa unawasumbua watu wengi kote duniani, hasa katika nchi zinazoendelea, huku nchi ya Ufilipino ikiongoza kwa maradhi hayo.

 

Katika miaka ya nyuma, vidonda vya tumbo lilikuwa ni tatizo la watu wachache sana, hususan watu wenye umri mkubwa wa kuanzia miaka 50 kuendelea, na wafanyabiashara wakubwa kutokana na misongo mikali ya kibiashara na ulaji mwingi wa vyakula vya kusisimua.

 

Lakini kulingana na mtindo wa maisha siku hizi, vidonda vya tumbo limegeuka kuwa tatizo la wote; vijana kwa wazee. Inakadiriwa kuwa kati ya 10% hadi 20% ya watu duniani, hupata vidonda vya tumbo walau mara moja katika maisha yao.

 

Tatizo ni kwamba watu wengi hujikuta ugonjwa umekuwa mkubwa kutokana na kudharau dalili za awali kwa kuziona ni za kawaida, hivyo kutotafuta matibabu ipasavyo. Wengi wanafahamu kuwa vidonda vya tumbo vinaleta maumivu katika tumbo lakini hawafahamu kama ugonjwa huu unaweza kuwa tishio la maisha.

 

Mgonjwa mmoja wa vidonda vya tumbo vinavyotokea katika mfuko wa chakula (gastric ulcers) kati ya kila wagonjwa 20 huweza kupata saratani ya tumbo.

Hata hivyo, vidonda vya tumbo vinaweza kutibiwa kabla havijazaa magonjwa mapya.

 

MFUMO WA USAGAJI CHAKULA

Tunatupia vyakuala mdomoni, lakini hatujui kinachoendelea ndani yake. Hakika ni kwamba walau kwa sekunde moja tungeweza kuona utendaji wa ajabu unaofanyika miilini mwetu, hakika tungestaajabu sana!

 

Hizi harakati za ‘ubadilishaji chakula kuwa chembe ndogo ndogo’ ndizo zinazoitwa, ‘usagaji wa chakula’ au ‘mmeng’enyo wa chakula’  (digestion).

Kwa kuwa vidonda vya tumbo vina uhusiano na viungo vinavyohusika na usagaji wa chakula, kwanza kabisa ni muhimu kuufahamu mfumo wa usogaji chakula.

 

Viungo vinavyohusika na harakati za usagaji chakula ni mdomo, umio, tumbo, utumbo mdogo, utumbo mkubwa, ini, kibofu nyongo na kongosho.

 

Mdomo: Harakati za usagaji chakula huanzia mdomoni. Mdomo una meno, ulimi na matezi ya mate (salivary glands). Meno husaidia kuvunja chakula kuwa vipande vidogo vidogo zaidi. Matezi ya mate hutoa mate ambayo husaidia katika usagaji wa chakula cha wanga. Pia, hukitia chakula unyevunyevu kinakuwa rahisi kumezwa. Kisha ulimi hukichanganya chakula kwa mate, na kukiviringisha chakula na kuwa matonge madogo madogo na kuyasukumizia kwenye koo.

 

Umio: Hili ni bomba la chakula. Kutoka mdomoni chakula huchukuliwa hadi kwenye tumbo kupitia kitu kinachofanana na tyubu nyembamba. Hiki huitwa umio au koromeo (Oesophagus). Chakula hutembea pole pole sana kupitia umio.

 

Tumbo: Huu ni mfuko wa misuli. Tumbo la binadamu lina umbo kama herufi J, na liko sehemu ya juu ya kushoto ya fumbatio (abdomen).

 

Itaendelea

By Jamhuri