*Maofisa wahusika wawakingia kifua

Hifadhi ya Msitu wa Mtae wenye ukubwa wa hekta 3,182 katika Tarafa ya Maramba, wilayani Mkinga, Tanga, iko hatarini kutoweka kutokana na uvamizi unaofanywa na raia wa Kenya, kwa baraka za baadhi ya viongozi na wananchi wa Tanzania.

Watumishi wa Idara ya Misitu wasio waaminifu, wamekuwa wakiwapokea Wakenya na kuwaingiza msituni humo kukata miti, na hivyo kuhatarisha uhai wa viumbe na binadamu ambao maisha yao yanategemea msitu huo.

 

Miti asilia ambayo ni adimu hapa nchini, imeanza kupotea kwa kasi. Miongoni mwa miti hiyo ni mivule, minyasa, mibarika, milombelombe, mishai na mikarambati. Pamoja na ukataji miti, uharibifu mwingine unaofanywa ni wa uchimbaji madini msituni humo.

 

Uharibifu huo umesababisha kuanza kupotea kwa ndege adimu katika Mto Msambiazi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mazingira ya Kijiji cha Maramba A, Thadeo Hiza, anasema hali si nzuri kabisa msituni humo, na kwamba mazingira ya Mto Msambiazi yameharibiwa mno na hivyo kusababisha upungufu wa maji.

 

Anasema licha ya jitihada za kamati za mazingira kuimarisha ulinzi, hali bado ni mbaya kwa kuwa kuna wavamizi wengi kutoka Kenya wanaoshirikiana na wenyeji kufanya hujuma kwenye msitu huo.

 

Anasema wameuarifu Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) wanaoshirikiana na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili (TFCG), ili kujionea hali halisi na kutoa taarifa mamlaka husika kupitia vyombo vya habari. Analalamika kwamba urasimu uliopo utasababisha kumalizwa kwa msitu huo.

 

Diwani wa Maramba, Said Almas, anasikitishwa na mazingira ya urasimu yanayooneshwa na watumishi wa Idara ya Misitu, kwani wamekuwa wakiuzuia mtandao wa MJUMITA, waandishi wa habari na kamati za mazingira kuingia msituni kuonea hali halisi.

 

“Kwa kweli hata sielewi ni kwa nini hawa watu wamewazuia ndugu zetu wa MJUMITA kufanya kazi iliyowaleta, mimi naamini kwamba hawa wana nia njema na wamekuja kushirikiana na wao watu wa misitu na wananchi ili kuhakikisha rasimali zetu hazihujumiwi,” anasema Almas.

 

Msitu wa Mtae uangalizi wake upo chini ya vijiji vinane (wananchi) na Serikali Kuu kwa utaratibu unaofahamika kama Joint Forest Management iliyopo kwa mujibu wa Sheria ya Misitu Namba 14 ya mwaka 2002 na Sera ya Misitu ya mwaka 1998.

 

Kuzuiwa kwa MJUMITA na waandishi wa habari kuingia msituni kumezua maswali mengi, hasa yenye hatima ya kujua kinachoendelea humo ndani.

 

Mratibu wa MJUMITA Kanda ya Kaskazini, Shabani Hamisi, anasema jitihada mbalimbali zilifanywa na mtaalamu wa misitu kutoka wilayani Mkinga, Frank Chambo.

 

Hamisi anasema anashangazwa kuwekewa zuio la kuingia msituni akielezwa na Chambo kwamba amepokea maelekezo kutoka kwa mkuu wake wa kazi,  Cathbert Mafupa, aliyepo Same mkoani Kilimanjaro.

 

Kitendo cha Chambo ambaye ni Kaimu Meneja Misitu Wilaya ya Mkinga kuwazuia MJUMITA, kimezua maswali miongoni mwa wajumbe wa kamati za mazingira na wananchi wengine.

 

“MJUMITA wapo kisheria na huu ni msitu shirikishi wa pamoja ambapo sisi wananchi ndiyo tuliowaita MJUMITA kuja, kwa hiyo tuna haki. Mazingira ya kukatazwa kuingia msituni yanaashiria kuna maafisa wanahusika kufanya hujuma,” anasema mmoja wa wanakamati.

 

Wanasema juhudi za kuhakikisha msitu huo unalindwa zimegonga mwamba kutokana na kuwapo mtandao mkubwa unaowahusisha wananchi kadhaa, viongozi na wasimamizi wa misitu pamoja na wageni kutoka Kenya.

 

Viongozi wa kamati za mazingira kwa vijiji vinavyozunguka msitu huo, wanasema watu kutoka nchi jirani ya Kenya wenye asili ya kabila la Waduruma, wanashirikiana na wenyeji na Mabwana Miti kuvuna miti kwa wingi. Miti inayoandamwa zaidi ni mkarambati ambao hutumika kutengenezea samani za mapambo.

 

Akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari, Chambo anasema amelazimika kutowaruhusu MJUMITA kuingia eneo la msitu wa Mtae, baada ya kupokea maagizo ya mkuu wake anayetaka mratibu wa mtandao huo kwenda huko ili kuweza kufanyika kwa makubaliano ambayo yatawezesha kutolewa kwa ruhusa.

Diwani Almas anapendekeza kutumiwa kwa askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) walio jirani ili waunusuru msitu huo.

 

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Mboni Mgaza, anakiri kushamiri kwa uharibifu wa msitu wa Mtae. Ameahidi kufuatulia msuguano kati ya MJUMITA na viongozi wanaowazuia wasiingie msituni.

 

Anataja hatua ambazo zimeshachukuliwa kudhibiti uharibifu wa mazingira msituni humo kuwa ni pamoja na kuwakamata na kuwafikisha mahakamani  wenyeviti wawili, akiwamo Mwenyekiti wa Kijiji cha Kwengema, na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kwengema. Anatoa wito kwa wananchi kutokata tamaa, badala yake waendelee kuwafichua watu wote wanaouhujumu msitu huo.

 

Mtendaji Misitu Kanda ya Kaskazini, Cathbert Mafupa, anasema kuwa shutuma zinazoelekezwa kwake juu ya kuwanyima ruksa MJUMITA kuingia eneo la hifadhi hazina mashiko.

 

Anasema amefanya hivyo kwa nia njema akiwataka wadau hao wa misitu kuwasiliana naye kwa kufika ofisini kwake kuzuia mwanya wa kutoa fursa hiyo kwa watu ambao si waadilifu.

 

Anasema kuna wakati hutokea watu wanaojitangaza kuwa wadau, lakini matokeo yake wamekuwa wakiuhujumu msitu.

 

Mwenyekiti wa MJUMITA, Revocatus Njau, anawatuhumu watumishi wa Misitu kwamba wamekuwa kikwazo kikubwa katika suala zima la ulinzi wa rasilimali misitu, akisema hawawatakii mema Watanzania.

 

Anapendekeza ufike wakati Idara za Misitu kupitia Tanzania Forest Service (TFS) kuangalia uwezekano wa kuachana kabisa na mambo ya misitu kwa kile alichoelezwa kuwa ni dhaifu.

 

Anasema upo ushahidi wa kutosha wa watumishi wa Misitu wanaohujumu hifadhi za misitu, na kwamba yuko tayari kuwaweka wazi iwapo atatakiwa kufanya hivyo.

 

Ameahidi kuwataja kwenye kikao cha wadau kitakachofanyika mkoani Tanga chini ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Galawa, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.

 

0755 28 24 57

By Jamhuri