Wiki iliyopita, Dk. Khamis Zephania katika mada hii ya vidonda vya tumbo na hatari zake, alizungumzia kazi na ulinzi wa kunyanzi za tumbo na utumbo mdogo, utemaji wa asidi ndani ya tumbo na sababu za vidonda vya tumbo. Sasa endelea na sehemu hii ya tano…

Tafiti zinafichua zaidi kwamba bakteria huyu ndiye anayewajibika sana kusababisha uvimbetumbo sugu, vidonda vya duodeni na huchangia kutokeza kwa baadhi ya saratani za tumbo. Asilimia 75-90 ya vidonda vya tumbo huhusishwa na bakteria huyu mwenye umbo la mviringo.

 

H. Pylori huishi ndani ya tumbo la binadamu na ni kiumbe pekee anayeweza kuishi katika mazingira yenye asidi nyingi. Ana umbo la helical ndiyo maana akapewa jina la Helicobacter na anaweza kujinyonga ndani ya kunyanzi za tumbo na kulitawala.

 

Tumbo huzalisha vitu viwili — Hydrochloric acid na pepsin. Hivi ni vitu vyenye kuchoma na vimewekwa mbali kutoka kwenye ukuta wa tumbo, vitenganishwe na ute telezi (mucus). Hivyo, ute telezi ndiyo KINGA ya tumbo dhidi ya asidi kali ya tumbo.

 

Bakteria huyu hudhoofisha hiyo kinga ya tumbo kwa kudhuru kunyanzi zake. Mfuniko wa tumbo na mfuniko wa duodeni hudhoofika na hali hiyo huruhusu maji ya usagaji chakula, kula kunyanzi za tumbo au duodeni.

 

Kama tulivyoona kunyanzi za tumbo hulindwa kutokana na kudhuriwa na asidi ya tumbo. Pindi ulinzi unaposhindwa, kidonda hujiunda. Unaweza kuwa tayari una bakteria anaishi tumboni mwako, na usitambue. Karibu watu milioni tatu duniani kote wana maambukizo ya H. pylori.

 

Watu wengi hupatwa na H. pylori wakati wa utotoni, lakini dalili kwa kawaida hutokea ukubwani. Watoto wanaoishi katika mkusanyiko mkubwa wa watu na ambao wana hali za chini kimaisha, ni rahisi sana kuambukizwa.

 

Wataalamu kwa hakika hawafahamu jinsi anavyoenea, ingawa inaonekana zaidi ni kupitia chakula, maji machafu na pia inasemekana yuko katika mate ya binadamu; hivyo anaweza kusambaa kupitia kugusana mdomo kwa mdomo, kama vile busu, magonjwa yanayoathiri njia ya chakula (hasa wakati wa kutapika), pia kupitia kinyesi.

 

Kama ambavyo tumekwishaona, kukaa na H.pylori mwilini hakusababishi vidonda vya tumbo, lakini ni kipengele kikuu.

 

Pia, hata kama vidonda havitatokea, bakteria huyu anafikiriwa kuwa ndiye sababu kubwa ya uvimbetumbo sugu (chronic gastritis) na uvimbe wa duodeni (duodenitis). Baadhi ya watafiti wanaamini H. pylori vilevile anaweza kurithiwa.

 

Kama tulivyokwishaeleza, bakteria huyu hukaa ndani ya ute telezi (mucus) ambao hufunika kunyanzi za tumbo na duodenum na huzalisha kimeng’enya (urease), ambacho huzimua (neutralize) asidi ya tumbo na kuifanya isiwe kali sana. Ili kufidia hali hii, tumbo hutengeneza asidi zaidi, ambayo huchoma kunyanzi za tumbo.

 

Kama tulivyoona , mara nyingi bakteria yoyote hawezi kuhimili kukaa katikati ya asidi ya tumbo, lakini Helicobacter pylori anaweza, kwa sababu ya kutoa kwake kimeng’enya ambacho kinaiwezesha kukaa ndani ya juisi ya tumbo kwa kuzimua juisi hiyo.

 

Kimeng’enya hiki hubadilisha kemikali iitwayo urea kuwa ammonia. Uzalishaji wa ammonia ndiyo unaowezesha asidi ya tumbo kuzimuliwa, na kuifanya kuwa pole na kuipokea bakteria kwa ukarimu zaidi.

 

Hivyo, hapo sasa bakteria huyu hutengeneza makazi yake ndani ya tumbo au duodeni akitoa kimeng’enya hicho ambacho humlinda dhidi ya shambulio la asidi ya tumbo, na kisha huchimba shimo ndani ya kunyanzi za ute.

 

Ingawa seli za kinga ambazo mara nyingi hutambua na kwenda kuwashambulia bakteria hawa, hujikusanya karibu na eneo la H.pylori lililoathiriwa, lakini seli hizi za kinga, hazina uwezo wa kuzifikia kunyanzi za tumbo. Yaani bakteria hawa wametengeneza mbinu za kuingilia muitikio wa kinga za mwili, na kuzifanya zisiweze kufanya kazi katika kuwang’oa. Pia, virutubisho vinavyopelekwa kusaidia chembehai nyeupe; kwa hakika navyo huishia kumlisha na kumrutubisha huyu bakteria.

 

Hali kadhalika, umbo lake la kujinyonga humsaidia kuchimba utando telezi ambao asidi yake si kali sana kuliko sehemu ya ndani. H.pylori anaweza pia kujishikiza katika seli ambazo zinaongeza ujazo sehemu ya ndani ya tumbo.

 

Hivyo, baada ya kuingia na kukaa ndani ya asidi ya tumbo, H. pylori sasa  hufanya kazi yake kwa namna mbili: kwanza huongeza utemaji wa maji tumbo (gastric juices) na pili hudhoofisha ute wa duodeni. Ukuta wa tumbo au duodeni ambao hauna kinga hushambuliwa na majitumbo.

 

Itaendelea

1287 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!