Waliokuwa vigogo wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), wanaoshitakiwa kwa makosa 15 ya uhujumu uchumi na utakatishaji wa fedha, wamemwandikia Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) wakiomba kukiri makosa yao na kutaka kurejesha mabilioni ya fedha wanayodaiwa kuyachotaka wakiwa watumishi wa umma.

Vigogo hao ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha, Astery Bitegeko, aliyekuwa Mhasibu wa bodi hiyo, Goodluck Moshi, Emmaculate Bitegeko ambaye ni mke wa Astery Bitegeko aliyeunganishwa katika kesi hiyo kutokana na kuwa mmoja wa wakurugenzi wa Kampuni ya AKIK and Family wanayomiliki yeye na mumewe.

Hata hivyo, hadi wiki iliyopita bado walikuwa hawajapokea taarifa yoyote kutoka kwa DPP kutokana na maombi yao hayo.

Hayo yalibainika wiki iliyopita baada ya vigogo hao kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kilimanjaro kwa ajili ya kesi yao kutajwa, chini ya Hakimu Mkazi Julieth Mawolle.

Katika mashitaka yanayowakabili, mawakili wa serikali, Ignas Mwinuka na Lilian Kowero walidai kuwa kati ya Julai 2016 na Julai 2018 watuhumiwa hao walianzisha na kusimamia kikundi cha uhalifu kwa ajili ya kutekeleza wizi na utakatishaji wa fedha haramu.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, shitaka la kwanza hadi la nne linawahusu Bitegeko, Moshi na Mrema waliokuwa watumishi wa Bodi ya Kahawa ambao wanadaiwa kumwibia mwajiri wao fedha.

Wanadaiwa kati ya Julai Mosi 2016 na Februari 2018 wakiwa watumishi wa Bodi ya Kahawa waliiba jumla ya dola milioni 1.2 za Marekani na zaidi ya Sh bilioni 2.9.

Wengine ni mfanyabiashara Doglas Malamsha, Katibu wa Kampuni ya Gee General Ltd, ambaye aliunganishwa katika kesi hiyo Desemba 10 mwaka jana na kusomewa mashitaka yake mbele ya Hakimu Pamela Mazengo.

Wamo pia wafanyabiashara Charles Mwashilindi, Elvis Umbella na Englbert Shayo ambao ni miongoni mwa wakurugenzi wa Kampuni inayojihusisha na biashara ya kahawa ya Gee General Ltd.

Wote hao wamemwandikia barua DPP kuomba kukiri makosa yao huku washitakiwa wawili, Isaya Mrema aliyekuwa mkaguzi wa ndani wa Bodi ya Kahawa na mfanyabiashara Said Banda wakiamua kutoandika barua.

Walipofikishwa mahakamani hapo wiki iliyopita, washitakiwa hao kupitia Wakili wao Emmanuel Anthony waliomba kujua hatima ya barua yao waliyoiandika kwa DPP kukiri makosa yao na kutaka warejeshe fedha wanazodaiwa kuzichota. Walitoa ombi hilo baada ya upande wa mashitaka kudai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.

Malamsha alisomewa mashitaka mawili; moja la uhujumu uchumi na kutakatisha fedha ambalo linawakabili pia washitakiwa wengine sita wanaodaiwa kutenda kosa hilo kati ya Julai Mosi 2016 na Februari 28, mwaka huu.

Malamsha pia ameshitakiwa katika shitaka la kuanzisha na kusimamia kikundi cha uhalifu kwa ajili ya wizi na utakatishaji wa fedha haramu.

Wakili Ignas Mwinuka na mwenzake Lilian Kowero walidai kuwa Malamsha na wenzake walifanya muamala wa dola 157,032.27 za Marekani kwa kuingiza fedha hizo katika akaunti za fedha za kigeni kupitia akaunti za Kampuni ya Gee General Ltd na kuidhinisha zitolewe Benki ya CRDB na NBC.

Katika kipindi hicho pia wanadaiwa kufanya mualama wa dola 424,820.12 za Marekani kwa kuingiza na kutoa fedha hizo kupitia akaunti za Lawaita Amcos na AKIKI and Family Enterprises inayomilikiwa na Bitegeko na mkewe Emmaculate. 

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyosomwa katika mahakama hiyo, washitakiwa hao pia wanadaiwa kuwa Februari 13, mwaka 2017 walijihusisha na muamala wa dola 30,000 za Marekani kwa kuziingiza na kuzitoa kupitia akaunti ya fedha za kigeni ya mshitakiwa wa pili, Goodluck Moshi.

Pia wanadaiwa siku hiyo hiyo ya Februari 13, mwaka 2017 washitakiwa hao walifanya muamala wa dola 22,010 za Marekani kwa kuziingiza na kuzitoa kupitia Kampuni ya Unyiha Associates na AKIKI and Family Enterprises.

459 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!