Vigogo Sumbawanga wakusanya vitabu ‘feki’

Vigogo wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa, wanaodaiwa kutengeneza vitabu bandia vya kukusanyia mapato ya ushuru na leseni za  uvuvi wa samaki katika ziwa Rukwa wameanza kuviondoa katika mzunguko.

Wiki iliyopita gazeti la JAMHURI liliripoti habari ya uchunguzi kuhusu baadhi ya maofisa wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga na Manispaa ya Sumbawanga kuchapisha vitabu bandia ambavyo vimekuwa vikitumika kuiibia serikali mapato kwa muda mrefu kwa kisingizio cha kuchanganywa vitabu hivyo bila kukusudia.

Baada ya kuripotiwa kwa habari hiyo, vyanzo vyetu vya habari vimelieleza gazeti hili kuwa baadhi ya wakuu wa idara wanaomiliki vitabu hivyo na kuiibia halmashauri mapato yatokanayo na shughuli za uvuvi wilayani humo walikutana na kuanza kuviondoa vitabu hivyo ‘feki’ katika kambi za wavuvi.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari kutoka katika kambi za wavuvi zilizoko pembezoni mwa ziwa hilo, wakuu wa idara akiwemo mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi wa Wilaya hiyo waliagiza vitabu hivyo vikusanywe na kurudishwa halmashauri kwa ajili ya uchunguzi na vilevile kuwachukulia hatua wahusika.

Imedaiwa kuwa baadhi ya watumishi wanaohusika na ukusanyaji wa mapato yatokanayo na sekta ya mifugo na uvuvi walihojiwa kuhusu vitabu hivyo feki vinavyotumika kuiibia mapato halmashauri hiyo walikiri kupewa vitabu na maofisa hao na kwamba fedha zinazokusanywa zinakabidhiwa kwa wahusika badala ya kuingia serikalini.

“Fedha zinazokusanywa hukabidhiwa kwa wakuu wa idara ambao hugawana kulingana na idadi ya vitabu vinavyotumika kukusanyia mapato hayo na mapato yanayotokana na vitabu halali ndiyo yanaingizwa halmashauri japo ni sehemu ndogo ikilinganishwa na mapato haramu yasiyoingia serikalini,” kimeeleza chanzo chetu cha habari.

Uchunguzi wa JAMHURI, umebaini kwamba vitabu hivyo feki huwaingizia mapato baadhi ya wakuu wa idara wilayani humo yanayokadiliwa kufikia zaidi ya Sh. milioni 100 kati ya wiki moja hadi mbili ambazo hazifikishwi ndani ya manispaa husika wala wilaya ya Sumbawanga ambako fedha hizo zinakusanywa.

Wavuvi na wafanyabiashara ya samaki katika ziwa Rukwa wameeleza kusikitishwa na vitendo hivyo vilivyodumu kwa muda mrefu kwa kupewa stakabadhi hizo “feki” kutoka Manispaa wakati wao wako halmashauri.

Wanasema hata kwa upande wa leseni za uvuvi vitabu vya stakabadhi za malipo vimechanganywa, wanapewa vya Manispaa ya Sumbawanga na halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kwa pamoja jambo linaloonesha wazi mapato yanayokusanywa yanaingia katika mifuko ya wajanja wachache.

Wafanyabiashara wa samaki kutoka kambi ya wavuvi ya Nankanga, Ilanga na Zimba ambao wamehojiwa na JAMHURI kwa sharti la kutoandikwa majina yao kwa hofu ya kuandamwa ama kukwamishwa katika biashara zao za uvuvi ziwani humo, wamesema kitendo cha kupatiwa stakabadhi za ushuru na leseni kwa kutumia vitabu feki vya kutoka Manispaa ya Sumbawanga ni wizi wa waziwazi unaofanywa kwa makusudi na viongozi wa halmashauri ya wilaya.

Wanasema matumizi ya vitabu hivyo ambavyo kazi yake ni kuhujumu mapato ya serikali ni mradi haramu wa wakuu wa idara wa halmashauri hiyo akiwemo Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi, Dennis Maghalla, Ofisa Uvuvi wa Wilaya, Kulwa Lukuba na Mhasibu wa Mapato wa Wilaya, Thobias Shija.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanasema wanashangazwa na kitendo hicho cha kuiibia serikali mapato yake kilichodumu kwa muda mrefu huku wahusika uongozi wa mkoa ukishindwa kukemea jambo linaloonesha wazi kuna idadi kubwa zaidi ya wahusika katika wizi huo.

“Hapa kuna mchezo mchafu sana na viongozi wote wa mkoa wa Rukwa wanaufahamu lakini wao wanaona mkoa huu ni kama nchi inayojitegemea nje ya serikali ya Tanzania, kama wana serikali yao vile,” anasema mmoja wa wafanyabiashara hao katika mahojiano na JAMHURI.

“Hili jambo ni la muda mrefu sana na mwaka 2014, liliwekwa wazi kwamba kwa nini halmashauri itumie vitabu vya Manispaa kukusanya ushuru kwenye maeneo yasiyowahusu? Hakuna majibu yanayoeleweka yaliyotolewa na wahusika zaidi ya kuendeleza ubabe huu wa kutuibia,” anasema.

“Huu ni wizi wa aina yake ambao umeendelea kwa muda mrefu sana ukiwahusu baadhi ya watendaji wa manispaa na halmashauri hiyo na baadhi ya maofisa kutoka ofisi ya Waziri Mkuu wanaodaiwa kupelekewa sehemu ya mapato hayo ambayo hayaingii serikalini,” kimeeleza chanzo chetu.

Imeelezwa kuwa wahusika wa wizi huo wamejiwekea imaya yao kiasi kwamba hawawezi kuguswa kwa namna yoyote ile na watu wanaothubutu kuhoji wanajiweka katika wakati mgumu katika kazi zao ama biashara zao.

JAMHURI limezungumza na Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi, Dennis Maghalla, kuhusu tuhuma zilizoelekezwa kwake kuhusu matumizi ya vitabu “feki” vya malipo ya ushuru na leseni za uvuvi wilayani Sumbawanga lakini amekana kwamba ahusiki navyo.

Maghalla amedaiwa kuwa ni miongoni mwa maofisa wa wilaya hiyo ambao wanatumia vitabu bandia kukusanyia ushuru na malipo ya leseni za uvuvi huku mapato hayo yakiishia katika mifuko ya wajanja wachache badala ya kuingia serikalini.

Maghalla anasema suala la vitabu hivyo lilikuwepo na taarifa zilitolewa katika vyombo vya habari na hatua iliyofuata ni kuondolewa kwa vitabu hivyo katika matumizi ya kukusanyia mapato yatokanayo na uvuvi katika ziwa rukwa.

“Hili suala la kuchanganya vitabu vya Manispaa na Halmashauri ya Wilaya kukusanyia mapato ya uvuvi lilipatiwa ufumbuzi, labda kama kuna baadhi vilibaki na anayeweza kulielezea hilo ni mweka hazina wa halmashauri au msaidizi wake,” anaeleza Maghalla.

Naye, Mweka Hazina wa Halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga, Credo Nduhie alipotafutwa kuelezea suala hilo hakupatikana. Hata hivyo gazeti hili lilifanikiwa kuzungumza na mhasibu wa mapato ambaye ndiye mhusika mkuu kwa upande wa mapato yatokanayo na shughuli za uvuvi katika ziwa hilo, Thobias Shija, ambaye alijibu kwa ukali, “Mimi sio msemaji wa halmashauri, mtafute DED (mkurugenzi).”

Hata alipoulizwa kuwa anahusika na vitabu hivyo kwa lengo la kujinufaisha wao binafsi badala ya mapato hayo kuingia serikalini, hakutaka kuzungumza chochote.

Ofisa Uvuvi wa Wilaya ya Sumbawanga, Kulwa Lukubi alipohojiwa kuhusu tuhuma hizo za kutumia vitabu vya stakabadhi vya Manispaa ya Sumbawanga kukusanyia ushuru wa uvuvi na ununuzi wa samaki kutoka ziwa rukwa  wilaya humo, amesema hiyo sio sheria na wala hairuhusiwi.

Wakati akilieleza JAMHURI, kuhusu kutokuwepo kwa vitabu hivyo ‘feki’, Lukubi amesaini moja ya risiti hizo ambazo zinadaiwa kuwa zinatoka katika vitabu hivyo vinavyotumika kuiibia mapato halmashauri ya wilaya hiyo.

“Labda kama kuna baadhi ya watu wameamua kuingiza vitabu hivyo kwa lengo la kuiibia mapato halmashauri, tunafuatilia suala hilo ili tufahamu kinachofanyika,” anasema Lukubi. 

Mkurungenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Adamu Missana, amekana kuhusika na vitabu hivyo ‘feki’ vya mapato ambayo huishia kunufaisha mifuko ya wajanja wachache badala kuingia serikalini.

“Mimi sielewi, silifahamu suala hilo, niache nilifanyie kazi, nasema sihusiki na vitabu hivyo,” anasema Missana.