Ulowassamoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), imetamba kuwa na uhakika wa kuunda Serikali zijazo kwa kupata wabunge zaidi ya 130 kati ya 264 ya Tanzania nzima.

Hayo yamethibitishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Sheria katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu  wakati akizungumza na JAMHURI katika mahojiano maalumu.

Serikali hizo ni za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ambazo kwa pamoja uchaguzi wake umepangwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.

“Watanzania kwa sasa wanatuelewa sana. Tayari tuna uhakika wa kupata wabunge wasipungua 130 wa majimbo 264 ya Bara na Visiwani. Hivyo, Serikali ya Mseto haiepukiki,” anasema Lissu.

Lissu amelidhihirishia JAMHURI katika mahojiano hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam kwamba kwa Tanzania Bara peke yake, Ukawa ina uhakika wa kushinda zaidi ya majimbo 101 wakati Zanzibar itavuna majimbo 30 kati ya 50. Jumla ya majimbo ya Bara ni 214.

“Hii ya 101 ni idadi ya majimbo ya Bara tu, kule Zanzibar ambako CUF imeota mizizi ambako upinzani umekubali, CUF itashinda kule na angalia tu rekodi tayari wana Serikali ya Mseto, imeanza kule, huku haiepukiki,” anasema.

Vyama hivyo ni pamoja na Chadema ambacho kimechukua majimbo mengi katika mikoa ya Kanda ya Kati na Kaskazini wakati Chama cha Wananchi (CUF), imejikita zaidi mikoa ya Pwani na Kusini mwa Tanzania.

Lissu anasema kwamba, licha ya makombora na kubezwa kunakofanywa dhidi ya Ukawa, lakini umoja huo umejipanga kushinda Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

“Ninachoweza kukwambia ni kwamba, hii ni vita kubwa, vita ya mabadiliko, tunatukanwa sana na makada wachache wa CCM na wale wanaoipenda CCM, lakini nikuhakikishie tu ni kwamba tumejipanga,” anasema.

Kwa mujibu wa Lissu, Kanda ya Magharibi kuna vyama vya NLD, CUF na NCCR-Mageuzi ambavyo vimejikita zaidi kwenye majimbo ya Mkoa wa Kigoma.

“Hatutapoteza majimbo tunayoshika kwa sasa, ndiyo maana tumeachia CUF majimbo mengi Zanzibar ambapo wao wana nguvu nyingi sana huko, CUF imewekeza sana Unguja na Pemba ambako kuna majimbo zaidi ya 50. CUF ina uhakika za kushinda,” anasema.

Anasema kwa kupata majimbo hayo, vyama vinavyounda Ukawa, watapata wabunge wengi wa viti maalumu mbali ya madiwani, “Na shabaha yetu kubwa ni kushika dola.”

Lissu anaongeza kuwa mwaka mwaka huu CUF haitaachia hata jimbo moja Pemba kama ilivyofanya katika uchaguzi wa mwaka 2010. Pemba ina majimbo 18 wakati Unguja kuna majimbo 32.

“Pale Unguja CUF ilipata majimbo manne. Ikawa na 22. Kuna uwezekano wa kuongeza 10 hivyo 30 hatukosi. Sasa ukichukua majimbo haya ya Bara na Zanzibar, hatukosi majimbo zaidi ya 130,” anasema.

Akijibu hoja ya namna wanavyohujumiwa, anasema kwamba, “Moja kubwa ni kuondoka kwa Profesa Ibrahim Lipumba katika wadhifa wa uenyekiti wa CUF. Hatuamini kama Lipumba amefanya haya kwa akili yake. Ni hujuma, lakini tutashinda.”

Lissu anasema kwamba kuondoka kwa Profesa Lipumba hakuna tofauti na Jenerali wa Jeshi aliyeamua kukaa kando wakati brigedia yake inakaribia kushinda vita katika uwanja wa mapambano.

Anasema kwamba Ukawa itabaki kuwa imara kwani jana Jumatatu, mgombea waliyeamua kumteua kuwania urais, Edward Ngoyai Lowassa na mgombea mwenza, Juma Duni Haji walitarajiwa kwenda Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuchukua fomu.

Lissu alikwenda mbali zaidi akisema kwamba tayari kuna mizengwe ya kutaka kuchafua upinzani au vyama vinavyounda Ukawa kwamba wataleta vurugu wakati wa uchaguzi au matokeo.

“Ma-CCM wanahangaika sana kwa sasa. Wanataka kuzima ndoto za Watanzania. Tume imetangaza wamejiandikisha watu zaidi ya milioni 20, hawa wakipiga kura, kwa jinsi walivyoelewa, Ukawa itashinda.

“Ili sisi tujiweke kwenye nafasi nzuri ya kushinda kwa kishindo, tumepanga na tumetangaza kwamba tutafanya kampeni za kistaarabu, hatutaki patokee dosari yoyote, ili Watanzania wapate Serikali yao mpya ijayo,” anasema.

Lissu anasema kwamba tathmini na tafiti zilizofanywa ndani ya Chadema na ripoti nyingine kutoka vyama vya Ukawa zinaonyesha kwamba nafasi ya ushindi ni kubwa.

Tume, chini ya uenyekiti wa Jaji mstaafu, Damian Lubuva na Mkurugenzi mpya wa uchaguzi, Kailima Ramadhani wametangza majini 214 ya Tanzania Bara.

Majimbo hayo ambayo Lissu amesema yako katika nafasi kubwa ya Ukawa kushinda na mikoa yake kwenye mabao ni pamoja na Arusha Mjini, Arumeru Magharibu, Karatu, Arumeru Masharibi na Monduli (Arusha).

Mengine ni Segerea, Ukonga, Kawe, Kibamba, Ubungo na Mbagala (Dar es Salaam) wakati kwa Mkoa wa Dodoma yamo majimbo ya Mtera, Kondoa na Chemba ilihali Geita wanatarajiwa kuvuna ubunge katika majimbo ya Geita Mjini, Bukombe, Busanda na Geita yenyewe.

Kwa mkoa wa Iringa Ukawa inajivunia kuwa na ngome katika majimbo ya Iringa Mjini, Isimani, Kilolo na Mafinga wakati Kagera yamo majimbo ya Bukoba Vijijini, Karagwe, Kyerwa na Muleba Kusini.

Katika Mkoa mpya wa Katavi, Ukawa imetamba kutwaa majimbo ya Mpanda Vijijini na Mpanda Mjini huku Kigoma yamo ya Kigoma Mjini, Buhigwe, Kasulu, Kasulu Mjini, Buyungu, Muhambwe, Kigoma Kaskazini na Uvinza zamani likifahamika kwa jina la Kigoma Kusini.

Katika Mkoa wa Kilimanjaro, Ukawa imejipanga kutetea majimbo ya Hai, Rombo, Moshi Mjini huku wakijipanga kuchukua majimbo ya Moshi Vijijini, Same Mashariki na Vunjo wakati Lindi imejipanga kutetea majimbo ya Lindi Mjini, Kilwa Kusini na kuchukua majimbo ya Mtama na Liwale.

Huko Manyara, Ukawa imetia tiki katika jimbo la Kiteto, Mbulu Vijijini, Mbulu Mjini na Simanjiro na kwa Mkoa wa Mara wamejipanga kuchukua majimbo ya Musoma Mjini, Musoma Vijijini, Bunda Mjini, Bunda yenyewe, Tarime Vijijini na Tarime Mjini.

Ukawa imesema kwa Mkoa wa Mbeya itachukua majimbo ya Mbeya Mjini, Songwe, Kyela, Mbarali, Mbeya Vijijini, Mbozi, Momba na Tunduma wakati Morogoro Ukawa imepania kuchukua majimbo ya Kilombero, Mlimba, Mikumi na Mvomero.

Mtwara imetaja majimbo ya Mtwara Mjini, Masasi, Mtwara Vijijini, Nanyumbu, Newala Mjini na Newala Vijijini wakati Mwanza imejipanga kutetea majimbo ya Ilemela, Nyamagana na kutwaa jimbo la Ukerewe.

Kwa Mkoa wa Njombe Ukawa imejipanga vema kutwaa majimbo ya Njombe Mjini, Wanging’ombe na Makambako wakati Mkoa wa Pwani imepania kutwaa majimbo ya Kisarawe, Mafia na Mkuranga.

Kadhalika kwa Mkoa wa Rukwa, Umoja huo wa Katiba ya Wananchi wamelipania jimbo la Kalambo wakati Mkoa wa Ruvuma Ukawa imesema ina nafasi kubwa Mbinga Mjini, Madaba, Songea Mjini, Tunduru Kaskazini na Tunduru Kusini.

Shinyanga yako majimbo ambayo wana nafasi nayo ni Kahama Mjini, Kishapu, Itilima, Maswa Magharibi, Maswa Mashariki na Meatu wakati Singida imetupia macho majimbo ya Singida Kaskazini na Singida Magharibi.

Mkoa wa Tabora imetaja majimbo ya Igunga huku Tanga majimbo yaliyotajwa ni Korogwe Mjini, Kilindi, Bumbuli na Tanga Mjini.

Kuhusu Zanzibar kuna taarifa za mgogoro wa kikatiba, kwani Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imeongeza majimbo mapya manne, jambo ambalo linapingwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa Tanzania nzima (NEC).

NEC imetoa hoja kwamba haijafanya tathmini ya kutosha na utafiti kuona kama kuna vigezo kuruhusu majimbo mapya Zanzibar ingawa tume hiyo inategemea kutumia daftari ya kudumu la wapiga kura kutoka ZEC ambayo imepanga kuendesha uchaguzi kwa majimbo 54.

Katika hatua nyingine, Lissu amesema kwamba mara baada ya kuchukua fomu ya kuwania urais, mgombea wa Chadema kwa mwavuli wa Ukawa, Lowassa anatarajiwa kuwa na ziara ya kutambulishwa.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Lowassa huenda akagongana na Rais Jakaya Kikwete kesho wakati wa mazishi ya kada mahiri wa CCM, Peter Kisumo aliyefariki dunia wiki iliyopita. Mzee Kisumo anatarajiwa kuzikwa kesho.

Mara baada ya mazishi, Lowassa atakwenda kutambulishwa Mbeya Ijumaa wiki hii (Agosti 14), kisha kwenda Arusha siku inayofuata (Agosti 15), kabla ya kwenda Mwanza Agosti 16 na kumalizia Zanzibar Agosti 17 na anatarajiwa kurejesha fomu NEC Agosti 21, mwaka huu.

Katika ziara hizo, Lowassa atapokea wanachama wapya akiwamo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Onesmo ole Nangole aliyejitoa CCM mwishoni mwa wiki iliyopita.

5934 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!