Profesa-Makame-MbarawaVigogo katika Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), wameuziana nyumba katika utaratibu ambao mmoja wao amenunua nyumba 18.

Ofisa Masoko, George Makuke, ambaye kwa sasa amestaafu, amenunua nyumba 18 eneo la Idiga. Ofisa mwingine, Ezekiel Hosea, amenunua nyumba 16 eneo ka Kifuru.

Pamoja nao, imebainika kuwa uuzaji nyumba hizo umekiuka Waraka wa Baraza la Mawaziri Na. 60 wa mwaka 2003 unaohusu uuzaji nyumba za mashirika ya umma.

Taarifa ya Ukaguzi ya Tazara iliyoandaliwa miaka miwili iliyopita, imebaini kuwapo ukiukwaji mkubwa wa uuzaji wa nyumba za Tazara, huku baadhi ya ‘wakubwa’ wakitumia fursa hiyo kujitwalia idadi kubwa ya nyumba.

Taarifa hiyo inaonesha kuwa Godfrey Swale alinunua nyumba tisa eneo la Mpemba; huku Mary Messo ambaye ni Ofisa Ugavi, alijitwalia nyumba nane eneo la Vigama. Mwanasheria Peter Mapunda yeye alinunua nyumba tano; nne zikiwa Mlimba mkoani Morogoro na moja ikiwa Kinyerezi, Dar es Salaam. Ambokile Mwakabinda ambaye amestaafu, aliuziwa nyumba nane – nne zikiwa Msesule, na idadi kama hiyo zikiwa Malamba.

Ofisa Masoko, Alexander Bange, alinunua nyumba tano. Nyumba nne kati ya hizo zikiwa Kiyowela na moja ikiwa Tabata. Ofisa Mwajiri, Evarist Laiderson, alinunua nyumba saba. Nyumba nne zipo Mbingu; nyumba mbili zipo Mlimba na moja ipo Kinyerezi. Andrew Mbakasa ambaye amestaafu, alinunua nyumba tatu zilizopo Mbingu.

Taarifa za Ukaguzi wa Ndani ambazo JAMHURI ina nakala zake (ukaguzi wa mwaka 2011 na mwaka 2014), inapendekeza wahusika wa uuzaji wa nyumba hizo wachukuliwe hatua kwa kukiuka sheria, kanuni na miongozo ya uuzaji na ununuzi wa nyumba za umma. Hata hivyo, hakuna hatua zozote zilizokwishachukuliwa hadi sasa.

Bodi ya Tazara iliporidhia uuzwaji nyumba za Mamlaka hiyo, ilipitisha kanuni na taratibu zilizopaswa kufuatwa.

Kanuni ya kwanza iliagiza kuwapo kwa uwazi na kuhakikisha nyumba zinauzwa kwa kufuata sheria na kanuni za nchi husika. Kwa upande wa Tanzania, mwongozo wa uuzaji nyumba ni Waraka wa Baraza la Mawaziri Na. 60 wa mwaka 2003 ambao pamoja na mambo mengine, unaagiza nyumba iuzwe kwa mtumishi anayeishi katika nyumba husika.

“Wakubwa wameuziana nyumba kwa kukiuka waraka, wamehamisha watumishi na wao wakaamua kuzimiliki na kuzipangisha kwa watu wengine. Wanasingizia kuna nyumba za maporini eti zilikosa watu wa kuzinunua, si kweli. Kuna watumishi walikuwa wakiishi katika nyumba hizo,” anasema mtumishi aliyenyimwa nyumba.

Katika malalamiko hayo, kuna watumishi 15 wanaoendelea kudai kuuziwa nyumba, lakini taarifa zilizopo ni kwamba humo wanamoishi kumeshauzwa.

 

Nyumba za polisi zauzwa

Katika uuzaji huo, nyumba ambazo Bodi ilizuia zisiuzwe ili ziendelee kutumika kwa kazi maalumu, nazo zimeshapigwa bei.

Kati ya hizo, nyumba 13 za polisi eneo la Tazara, Dar es Salaam zimeuzwa kwa mfanyabiashara na polisi wameondolewa. Nyumba alizonunua amezimoboa na kujenga Bandari Kavu (ICD).

Duru za uchunguzi zimebaini kuwa licha ya kuuzwa kwa nyumba hizo, si wanunuzi wala wauzaji walioweza kulipa kodi mbalimbali serikalini kwa mujibu wa sheria. Wakili aliyehusika ambaye tunahifadhi jina lake kutokana na kutompata, mihuri yake inayopaswa kufanana kwa jina, ina majina yanayotofautiana herufi. JAMHURI ina baadhi ya nakala za hati za mauziano.

Wakati nyumba hizo zikiwa zimeshatwaliwa na eneo kubadilishwa kwa matumizi mengine, JAMHURI imebaini kuwapo kwa mkataba na mpango mwingine wa kuuzwa nyumba nyingine wanazoishi polisi kupitia kampuni ya Easy Network yenye nasaba na kampuni ya Al Hushoom Investment Limited.

Uongozi wa Polisi Tazara ndiyo uliochelewa mpango huo kutokana na madai yake kwamba nyumba hizo hazistahili kuuzwa, kwani kufanya hivyo ni kudhoofisha ari na utendaji kazi wa askari.

Lakini Meneja Mkuu Tazara Mkoa wa Tanzania, Abdallah Fuad, anatetea uuzaji nyumba hizo akisema ulifanywa na watumishi wenyewe baada ya kuzinunua.

Tofauti na mwongozo wa Bodi ya Tazara, Fuad anasema uuzaji nyumba hizo haukutakiwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi husika, isipokuwa ule uliowekwa na Bodi.

“Hizi habari zinapotoshwa sana, huwezi uziwa nyumba sita Dar es Salaam. Kuna nyumba nyingine ziko katika stesheni zilizo maporini, hakuna wa kuzinunua. Kuna stesheni zimefungwa, watu wakavamia na kuishi katika nyumba hizo. Mimi nipo Tazara kuanzia mwaka jana kwa hiyo sina cha kuficha. Nyumba zilianza kuuzwa mwaka 2008. Walionunua nyumba za Tazara hawakubanwa na masharti kama ya kutoziua ila baada ya miaka 25. Hilo halikuwabana Tazara.

“Kuna kampuni ya Al Hushoom, ambayo imeuziwa nyumba na wafanyakazi wa Tazara. Kama Tazara iliuza nyumba maana yake umiliki ulikoma, mikataba ya walionunua haikuwazuia kuziuza. Tazara is not part ya Waraka Na. 60 wa Baraza la Mawaziri wa mwaka 2003.

“Ule waraka ulihusu nyumba za TBA. Nyumba za Tazara ziliuzwa kupitia Bodi ya Wakurugenzi ambayo wenyeviti ni makatibu wakuu wa wizara mama za nchi husika. Waraka huo haukuhusu nyumba za Tazara, kwa hiyo waliozinunua walikuwa na uhuru wa kuamua kuzitumia au kuziuza,” anasema Fuad.

Katika namna inayoibua mkanganyiko, Fuad, anaponda taarifa ya Mkaguzi wa Ndani iliyoibua tuhuma za ufisadi, akisema ina kasoro nyingi. Pengine ni kwa kuamini hivyo, Meneja huyo amekuwa akiunda timu za wataalamu wake mara kwa mara kupitia masuala mbalimbali yanayolalamikiwa.

 

Eneo jingine la Tazara lamegwa

Jengo la karakana ya Tazara lenye mitambo ya kutengeneza ‘injector pumps’ za injini za treni za Tazara na wateja wengine, limemegwa na kupewa ‘mwekezaji’ ambaye amezungushia ukuta.

Hatua hiyo imesababisha ‘injector pumps’ zisitengenezwe hapo, bali zipelekwe nje ambako kiasi kikubwa cha fedha kinatumika.

2071 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!