Vijiji 23 katika Wilaya ya Longido mkoani Arusha, vimepokea Sh 106,927,900 kutoka Mfuko wa Uhifadhi unaojulikana kama Friedkin Conservation Fund, unaomiliki kitalu cha uwindaji wa kitalii cha Natron Kaskazini.

Mfuko huo umefikia uamuzi wa kutoa fedha hizo, baada ya kuridhishwa na ushiriki mzuri wa wakazi wa vijiji hivyo katika uhifadhi wa mazingira na wanyamapori.

 

Makabidhiano ya hundi ya kiasi hicho cha fedha yalifanyika kati ya Mratibu wa Vikosi vya Kuzuia Ujangili, Clarence Msafiri, na Ofisa Maendeleo ya Jamii, Aurelia Mtui, mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Longido, James ole Millya, madiwani na wenyeviti wa vijiji husika, hivi karibuni.

 

Mtui amefafanua kuwa fedha hizo ni sehemu ya mapato yaliyotokana na uwindaji wa kitalii, unaofanywa na kampuni yao ya Wingert Windrose Safaris katika kitalu hicho.

 

Millya ameishukuru kampuni hiyo, na kuwataka wenyeviti wa vijiji kuzifikisha fedha hizo kwa wananchi husika na kuzipangia matumizi sahihi.


“Fedha hizi zisaidie vijiji na kuleta mabadiliko katika maisha ya wanavijiji, hatutaki suala hili la mapato na matumizi kuwa ndiyo ajenda ya malalamiko katika uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa hapo mwakani,” amesisitiza.


Awali, Mtui alisema mgawanyo huo wa mapato umezingatia juhudi binafsi za kila kijiji katika suala la uhifadhi wa mazingira na wanyamapori.

 

“Sidhani kama ni vizuri baada ya miaka 10 hivi ijayo, watoto wetu wapate simulizi tu kwamba hapa kulikuwa na simba, tembo au twiga…tunawaomba tuendelee kutunza mazingira na kuwadhibiti majangili,” amesema.

 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Joseph ole Saadira, amewahimiza wenyeviti wa vijiji hivyo kujenga utamaduni wa kuandaa ripoti ya mapato na matumizi, za fedha za umma na kuziweka wazi kwa wananchi.

 

Vijiji vilivyonufaika na kiasi cha fedha kikiwa katika mabano ni Alaililai (Sh 4,418,365), Eworendeke (Sh 4,348,365), Gelai Lumbwa (Sh 5,268,365), Gelai Merugoi (Sh 4,518,365), Kimoukouwa (Sh 4,225,865), Longido (Sh 4,418,365), Magadini (Sh 4,418,365), Mairowa (Sh 4,418,365), Matale ‘A’ (Sh 4,418,365) na Matale ‘B’ (Sh 4,418,365).


Vingine ni Mundarara (Sh 4,418, 365), Ngoswak (Sh 4,418,365), Orgira (Sh 4,418, 365), Orkejuloongishu (Sh 6,761, 365), Sinonik (Sh 4,418,365), Kiserian (Sh 4,418,365), Armanie (Sh 6,818,365), Kimwati (Sh 4,388,365), Lesingita (Sh 4,398,365), Loondoluo (Sh 4,418,365), Ranch (Sh 4,118,365) na Ilchang’it Sapuki (Sh 5,643,365).


1147 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!