Viongozi wa michezo, leteni mabadiliko

Wadau wa michezo hapa nchini, wametakiwa kuacha tabia ya kutoa pongezi pale timu inapofanya vizuri, badala yake waje na mbinu pamoja na mikakati ya kuhakikisha Tanzania inarudisha makali yake katika michezo ndani na nje ya nchi.

Akizungumza na JAMHURI wiki hii, mwanariadha mkongwe, Juma Ikangaa, anasema mtindo wa zimamoto unaoendelea nchini hauwezi kuleta manufaa katika micheo.

Anasema viongozi wengi wa michezo nchini wamekuwa wepesi wa kutoa pongezi mara timu inapofanya vizuri, bila kutoa michango yao katika kuhakikisha timu zinapata matokeo mazuri.

“Unapoona timu inaingia katika mashindano bila kuwa na maandalizi, ikitokea imepata ushindi viongozi wanaanza kusogea na kuyateka kana kwamba yamepatikana kwa mipango thabiti, huu ni udhaifu,” anasema Ikangaa.

Anasema mwaka 1974, Rais Julius Nyerere alipoanzisha Wizara ya Utamaduni na Michezo kwa makusudi aliamua  kumteua Jenerali Mirisho Sarakikya kuwa waziri wa wizara hiyo.

“Baada ya kuanzishwa kwa wizara hiyo, mara moja Serikali ilianzisha kitu kinachoitwa ‘culture exchange’ hapo ndipo wanamichezo wengi kutoka Tanzania walipoanza kubadilishana ujuzi na mataifa mengine,” anasema Ikangaa.

Anasema mara baada ya Jenerali Sarakikya kukabidhiwa wizara, kitu cha kwanza alichokifanya ni kuanza kuimarisha vyuo vilivyokuwa vikizalisha walimu wa michezo nchini.

Anasema vyuo kama Butimba TTC, Kleruu TTC, Korogwe TTC na vingine vingi nchini vilivyokuwa vikitoa wataalamu wa michezo hapa nchini.

“Wataalamu hawa wote kutoka katika vyuo hivi mara baada ya kumaliza mafunzo yao walipelekwa katika shule zetu kuanzia ngazi ya chini hadi juu, kwa lengo la kuhakikisha michezo inachezwa katika shule zetu,” anasema Ikangaa.

Ikangaa anasema katika kipindi hicho ndani ya shule za hapa nchini kulikuwapo na vipindi vya michezo kila siku huku Serikali kwa kupitia wizara husika ikihakikisha uwepo wa vifaa vya michezo kila wakati.

Anasema mara baada ya kukamilika kwa mpango huo, Serikali ilihakikisha wataalamu hao wanabadilishana ujuzi na wataalamu wengine kutoka nchi mbalimbali.

“Hapo ndipo tulipowaona wataalamu wetu wa michezo wengi wakienda Ujerumani, Cuba,Uingereza, Urusi na nchi nyingine kwa lengo la kwenda kubadilishana ujuzi,” anasema Ikangaa.

Anasema matokeo ya uwekezaji huu ulikuja kuanza kulipa pale Tanzania ilipoanza kuwashuhudia wanamichezo kama Juma Ikangaa, Filbat Bayi, Abdallah Kibaden, Peter Tino, Leodegar Tenga na wengine wengi waliokuja kuifanyia nchi mambo makubwa.

Anawataja wanamichezo wengine waliotokana na mikakati hiyo ya michezo katika miaka hiyo kuwa ni Francis Naali, Christopher Isegwe, Suleiman Nyambui, Mwinga Mwanjala waliotisha duniani na kuifanya Tanzania kujulikana vizuri.

Anasema kutokana na Serikali kuwa na mipango na mikakati ya hali ya juu, haikushangaza Tanzania kuwa tishio katika ukanda huu lilipokuja suala la michezo.

“Mwaka 1980, Nigeria ilikuwa mwenyeji wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, mashindano ambayo Tanzania ilishiriki na wenyeji kufanikiwa kulibakisha kombe baada ya kuilaza Algeria katika fainali,” anasema Ikangaa.

Anasema hata katika riadha ni wakati huo ambapo wanariadha wengi walifanya vizuri katika mashindano  mbalimbali ndani na nje ya nchi, rekodi ambayo haijavunjwa hadi leo.

“Kwa mfano, mwaka 1988 nilifanya vizuri katika mashindano ya Boston Marathon nchini Marekani, kwa kushinda medali na mwaka uliofuata nilishinda New York City Marathon, hii yote ilitokana na Serikali kupitia wizara husika kuwa na mipango endelevu katika michezo.

 “Hebu jaribu kufikiria uzalendo aliouonesha kwa nchi yake mwanariadha mkongwe John Stephen Akwari mwaka 1968 katika mashindano ya Olympics nchini Mexico,” anakumbuka Ikangaa.

Anasema katika mashindano hayo, Akhwari aliumia mguu, hali iliyosababisha kushindwa kufanya vizuri katika mashindano hayo na kukataa kupanda gari la wagonjwa.

“Alipoulizwa sababu zilizofanya akatae kupanda gari la wagonjwa, alijibu kuwa nchi yake haikumtuma maili nyingi kuja kuanza mashindano ila kuja kumaliza mashindano,” anasema Ikangaa.

Anasema uzalendo kama huo ndani ya nchi yetu umebaki kama historia ndani ya nchi yetu, hiyo ni kuanzia kwa wanamichezo wenyewe, hali inayoendelea kudidimiza michezo mpaka leo.

Anasema hata katika michezo kama ngumi ni wakati huu walipopatikana watu kama akina Emmanuel Mlundwa, Titus Simba, Willy Isangura na wengine wengi waliokuwa tishio katika mchezo huo.

Ikangaa anasema klabu inaweza kuwa na kocha mzuri lakini akakabidhiwa klabu  isiyo na mfumo imara wa kiuongozi, hapo hakuna kitakachofanyika, hivyo hivyo hata kwa wachezaji, wanaweza kuwa wachezaji wazuri lakini wakakutana na viongozi wabovu mambo yakaenda kombo.

Mwanariadha huyo anasema katika miaka ya hivi karibuni, vyama vya michezo vimegeuka kuwa vichaka kwa watu wa aina mbalimbali wasiokuwa na nia ya dhati ya kuendeleza michezo na matokeo yake michezo imekuwa inadidimia.

 Ikangaa aliyezaliwa mwaka 1957 mjini Dodoma, anasema ni ndoto kwa Tanzania kupata mafanikio katika michezo kama hali ilivyo sasa ndani ya vyama vyetu vya michezo itaendelea kuwa kama ilivyo.

“Lazima tuelewe kuwa hakuna njia ya mkato katika kuyafikia mafanikio, katika mchezo wa aina yoyote ni lazima kama nchi tuwekeze katika michezo kuanzia ngazi ya chini,” anasema Ikangaa.

Anasema wakati majirani zetu wakiendelea kupata mafanikio katika michezo mbalimbali, kwa upande wetu vyama vyetu vya maichezo vimeendelea kugubikwa na migogoro isiyokuwa na mwisho.

“Ndani ya vyama hivi kila kukicha ni kufikishana mahakamani huku Serikali nayo ikiwa imeipa kisogo michezo, hali ambayo imeendelea kutuchimbia kaburi,” anasema Ikangaa.

Anasema kilichobaki kwa viongozi wetu ni kusubiri juhudi za mtu binafsi, halafu utawasikia wakitoa pongezi za kujikosha, hali inayoonesha aina ya viongozi tulio nao.