Virusi vingine hatari hivi hapa

DAR ES SALAAM

Na Aziza Nangwa

Wakati dunia ikiendelea na mapambano dhidi ya ugonjwa wa COVID – 19 unaosababishwa na virusi vya corona; virusi vinavyotambulika kama ‘Human Papilloma’ (HPV) vinatajwa kuwa ni hatari kwa binadamu.

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Dk. Crispin Kahesa, ameliambia JAMHURI kwamba virusi hivyo hueneza kansa ya shingo ya kizazi, ulimi na macho. 

Taarifa zinaonyesha kuwa magonjwa yasiyoambukiza yameshika kasi na kusababisha asilimia 40 ya vifo nchini.

Magonjwa hayo ni shinikizo la damu, saratani, kisukari, ajali, magonjwa ya meno na magonjwa yanayosababishwa na lishe duni.

Dk. Kahesa anautaja ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi unaosababishwa na HPV kama miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza yanayowatesa Watanzania wengi. 

“Mwaka 2020/21 ORCI tumepokea wagonjwa 48,971 wa saratani. Asilimia 21 ni wa saratani ya shingo ya kizazi; wakati saratani ya matiti ni asilimia 16, njia ya chakula asilimia 12, tezi dume asilimia nane, saratani ya shingo na kichwa ni asilimia sita. Asilimia zilizobaki ni saratani za aina nyingine,” anasema.

Sababu za kuenea kwake

HPV husambaa kwa njia ya kujamiiana na Dk. Kahesa anawataja wanawake wenye umri wa kuanzia miaka 25 kama kundi lililo katika hatari zaidi ya kupata maambukizi haya.

“Wanawake hawa ni wale walioanza kufanya ngono mapema na wameambukizwa kutoka kwa wenzi wao wenye wapenzi wengi wanaofanya ngono zembe,” anasema.

Saratani ya shingo ya kizazi husambaa kama magonjwa mengine ya zinaa na hata maambukizi yake hufanana, hivyo mwenye maambukizi ya VVU ambaye hatumii sawasawa dawa za kufubaza virusi, akapata saratani hii anakuwa katika hatari kubwa zaidi.

“Watu wanaweza kuepuka ugonjwa huu wakiacha ngono zembe na kuzingatia usafi baada ya tendo la ndoa. Usafi hudhibiti HPV,” anasema Dk. Kahesa.

Anasema ugonjwa huu upo zaidi katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara kuliko Ulaya kwa kuwa eneo hili limeathiriwa sana na ukimwi huku watu wakizembea kuchukua tahadhari.

Tafiti zinaonyesha kuwa na wapenzi wengi kunamuweka katika hatari ya kupata ugonjwa huo kwa urahisi na maeneo yenye maambukizi makubwa ya ukimwi ndiko saratani ya shingo ya kizazi imeenea.

Anaitaja mikoa ya Iringa, Mbeya, Dar es Salaam na Mwanza kama vinara kwa ugonjwa huo, huku Lindi, Tanga, Pwani na Rukwa ikiwa na wagonjwa wachache zaidi. 

Dalili za saratani ya shingo ya kizazi

Mwanzoni mwa maambukizi ya saratani hii dalili huwa hazionekani hadi kwa vipimo maalumu, lakini kadiri siku zinavyokwenda husambaa mwilini na dalili kuanza kujitokeza.

Dk. Kahesa anasema dalili za awali ni maumivu chini ya kitovu, kutokwa uchafu wenye harufu na damu, mwanamke kupata mzunguko wake usio wa kawaida, maumivu wakati wa tendo la ndoa na uzito kupungua isivyo kawaida.

Anasema iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa, mgonjwa ataanza kuona dalili za figo kufeli ambapo atakuwa akipungukiwa damu, kuvimba miguu, kichefuchefu, kupoteza hamu ya kula na mwishowe mwili kukosa nguvu.

Saratani ya matiti

Mbali na saratani ya shingo ya kizazi, Dk. Kahesa anaitaja saratani ya matiti kwa wanawake na wanaume.

Hata hivyo, asilimia 99 ya wagonjwa wa saratani hii ni wanawake.

“Vyanzo vya saratani hii vinatajwa kuwa ni unene uliopitiliza, kina mama ambao hawanyonyeshi, kutokufanya mazoezi, matumizi holela ya vidonge vya uzazi wa mpango, tumbaku, ulevi uliopitiliza na ni ugonjwa wa kurithi,” anasema Dk. Kahesa.

Dalili zake ni kuwa na matiti makubwa kuliko kawaida, titi kuwa na rangi ya limao na maumivu makali ya kifua.

“Tezi dume ni miongoni mwa saratani hatari zinazowatesa wanaume kwa asilimia kubwa. Waathirika ni wenye umri kuanzia miaka 50,” anasema Dk. Kahesa.  

Kama ilivyo kwa saratani ya matiti, unene mkubwa katika umri huo, kurithi, ulevi, ulaji nyama nyekundu kupita kiasi,  matumizi ya tumbaku na ukosefu wa mazoezi vinatajwa kama sababu za ugonjwa huo.

Anazitaja dalili zake kuwa ni kupungukiwa nguvu za kiume, kwenda haja ndogo mara kwa mara, mkojo kushindwa kutoka na maumivu ya mifupa na nyonga.

Saratani nyingine ni ya njia ya chakula inayoathiri wanaume kwa asilimia 60, kutokana na matumizi ya vimiminika vikali.

“Vimiminika hivi huchubua koo. Lakini pia matumizi ya tumbaku, historia ya kuwa na chachu nyingi (kiungulia) husababisha kupata vidonda vya tumbo,” anasema na kuongeza:

“Dalili zake ni kupata matatizo wakati wa kumeza chakula na baadaye kushindwa kabisa kumeza chakula chochote, maumivu kwenye kifua na mgongo,” anasema.

Maumivu hayo huwa ni makubwa hadi yatakapopatiwa tiba stahiki baada ya vipimo sahihi hospitalini.

Tatizo linalowakabili wataalamu wa afya katika kupambana na saratani hii ni wagonjwa, hasa wa vijijini, kwenda hospitalini wakiwa tayari wamekwisha kuchelewa.

“Wengine baada ya matibabu wakipangiwa tarehe ya kurudi, hawarudi tena,” anasema Dk. Kahesa.

Saratani, isipokuwa ile ya mlango wa kizazi, ni magonjwa yasiyoambukiza ambayo yapo katika makundi kama kisukari, ajali, magonjwa ya akili, ya meno na ya lishe. 

Magonjwa haya hayana madhara kwa mtu mwingine; mgonjwa aliye nao anabaki kuwa nao peke yake. 

Takwimu za magonjwa yasiyoambukiza zinaonyesha ugonjwa wa moyo ukiongoza kwa asilimia 12; saratani (10), magonjwa ya akili (8), ajali (8), mfumo wa fahamu (6), mfumo wa chakula (6), mfumo wa misuli na mifupa (5) na magonjwa sugu ya mfumo wa njia ya hewa (8).

Upande mwingine ni ajali (4), magonjwa yanayosababishwa na mtu mwenyewe (4), magonjwa ya ngozi (4), magonjwa ya mfumo wa fahamu kama ulemavu wa masikio, macho na kutoongea (3).

Pia takwimu zinaonyesha kupanda kwa mwelekeo wa ugonjwa wa saratani katika miaka kumi iliyopita kwa asilimia 60, ukiwaathiri wenye umri chini ya miaka 40.

Duniani, saratani mbalimbali zinaongezeka kutokana na  mfumo wa maisha na watu kutobadili tabia hatarishi kama uvutaji tumbaku, ulevi uliokithiri na ukosefu wa mazoezi.

Tabia nyingine hatarishi ni ulaji wa vyakula vinavyoongeza uzito, vyakula vilivyosindikwa viwandani, milo isiyo na uwiano wa chakula bora sanjali na kunywa maji ya kutosha kwa siku.

“Watu wengi wamesahau kula vyakula vya asili vilivyochanganyika na matunda na mboga za majani. Chakula cha usiku kinapaswa kuliwa saa tatu kabla ya kwenda kulala ili kutoa muda wa chakula kusagika,” anasema Dk. Kahesa.

Mkurugenzi Idara ya Kinga Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dk. Crispin Kahesa