Idadi ya maambukizi, vifo yaongezeka kila kukicha

Wataalamu watabiri uchumi wa dunia kutetereka

Kwa zaidi ya wiki sita sasa dunia imekuwa kwenye mshikemshike kutokana na kuibuka kwa kirusi hatari kijulikanacho kama Corona. Kirusi hicho, ambacho si kipya katika orodha ya vijidudu vinavyosababisha magonjwa ambavyo vinawasumbua binadamu, kimeibukia nchini China.





Inaaminika kuwa soko linalouza vyakula vya baharini katika Jiji la Wuhan nchini China ndicho chanzo cha kirusi cha Corona ambacho kinaisumbua dunia hivi sasa.

Kutokana na utandawazi, katika kipindi kifupi tu cha wiki mbili, kirusi hicho tayari kimekwisha kusambaa katika nchi

nyingi duniani. Kusambaa kwa kirusi hicho kumezua taharuki katika nchi nyingi. Baadhi zimewatangazia raia wake zikiwaonya kuhusu kusafiri kwenda China katika kipindi hiki.

Kuna baadhi ya mashirika ya ndege makubwa duniani yamesitisha safari kwenda China. Kampuni kubwa za biashara nazo zimeweka breki katika mipango yake ya biashara zinazohusiana na China.

Hayo yote yanatajwa kuwa yanaweza kuathiri na kuyumbisha uchumi wa dunia, iwapo kirusi hicho kitazidi kusambaa. 

Matatizo ya aina nyingi za virusi ni kuwa havina tiba mahususi. Hata kirusi cha Corona nacho kilipobainika  

 hapakuwa na tiba maalumu kwa ajili yake. Bahati nzuri ni kuwa katika kipindi kifupi tu wanasayansi huko huko China wamefanikiwa kugundua tiba ya kirusi hicho. Jambo hilo linaweza kuleta ahueni kwa baadhi ya nchi.

Ni dhahiri kuwa China ambayo ndiyo inaongoza kwa kuathiriwa na virusi hivyo, itaanza kwanza kuzalisha dawa kwa ajili ya wananchi wake. Baada ya hapo ni dhahiri kuwa nchi zenye nguvu kiuchumi ndizo zitaanza kunufaika na dawa hiyo. Itachukua muda kidogo kwa tiba hiyo kuzifikia nchi zetu hizi za dunia ya tatu.

Uchumi kuyumba

Pamoja na masuala yaliyoelezwa hapo juu kuhusiana na biashara, uchumi wa dunia unatarajiwa kuyumba kutokana na kirusi hiki cha Corona. Kama tulivyoona, kampuni na nchi nyingi zimeanza kufanya marejeo ya mipango yao ya kibiashara ambayo inahusu nchi ya China.

Kwa sasa athari za jambo hili zinaweza zisionekane kwa haraka. Wazalishaji wanafanya hivyo kwa sababu kuibuka kwa kirusi hicho kunaweza kusababisha kushuka kwa mahitaji ya bidhaa nyingi, hasa zile zinazouzwa kwa wingi nchini China. Hilo likitokea, wazalishaji watalazimika kupunguza uzalishaji na hilo linamaanisha kupunguza wafanyakazi.

Ingawa hayo hayajaanza kujitokeza kwa wazi hivi sasa, lakini dalili zake zimeanza kuonekana. Katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, idadi ya watu katika mitaa mingi katika majiji mengi nchini China imeanza kupungua. Hivi sasa mitaa mingi inabakia wazi wakati watu wakiitikia wito uliotolewa na wataalamu wa afya kupitia serikali kuwa ili kujikinga kuambukizwa na kirusi cha Corona, ni vema mtu akabaki nyumbani kwake. Watu wanashauriwa kutoka iwapo tu watakuwa na mahitaji ya muhimu.

Hadi wiki iliyopita, zaidi ya watu milioni 45 katika Jimbo la Wuhan walikuwa wametengwa na dunia. Jimbo hilo ndiko ambako virusi hivi viliibukia, hivyo ndilo lililoathirika kwa kiasi kikubwa sana. Ili kudhibiti virusi hivyo kusambaa, China imeweka marufuku ya watu kutoka nje ya jimbo hilo.

Hapo unaweza kuanza kuona athari za kiuchumi zinazotokana na kirusi cha Corona. Na madhara si ya kiuchumi tu kwani hata kijamii, kwa sababu katika kipindi hicho watu hawaruhusiwi kutembeleana, hakuna shughuli za kijamii kama vile burudani na michezo.

Hivyo, athari za kirusi cha Corona zinaweza kuwa za kijamii na kisiasa pia. Kwa upande wa siasa tayari tumekwisha kushuhudia baadhi ya nchi zikitumia nguvu zao kidiplomasia kuweka marufuku ya watu waliosafiri kwenda China katika

kipindi cha wiki chache zilizopita kuingia kwenye nchi hizo.

Kwa upande mwingine, tumeshuhudia viongozi wa kisiasa kutoka nchi mbalimbali wakianza kujadili namna bora zaidi ya kukabiliana na virusi hivyo vinavyosambaa kwa kasi duniani. Serikali ya China iliahirisha sherehe kubwa za mwaka mpya wa Kichina, pia ikasogeza mbele tarehe ya kufunguliwa kwa masoko ya hisa. Masoko hayo yalipofunguliwa wiki iliyopita, bei ya hisa ikashuka kwa kiasi kikubwa kabla ya kuanza kupanda taratibu siku zilizofuata.

Hata hivyo, kama tahadhari, Serikali ya China imeingiza Yuan trilioni 1.2 katika mifumo ya kifedha. Hiki ni kiasi kikubwa sana kuwahi kutolewa na serikali ili kuhakikisha masoko ya hisa hayaathiriki. Kwa upande mwingine, serikali hiyo pia imefuta kodi zote za vifaa ambavyo vinatumika katika kupambana na ugonjwa huo.

Biashara zafungwa

Si masoko ya hisa tu ndiyo yameathitika. Mahitaji ya bidhaa nchini China yamepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na kuibuka kwa kirusi hicho. Matukio makubwa ya sherehe za Mwaka Mpya yalifutwa.

Matukio haya ni moja ya matukio ambayo yanapandisha mahitaji ya bidhaa mbalimbali nchini humo. Vivutio vingi vya utalii na majumba ya kuonyesha sinema vimefungwa. Takriban migahawa 2,000 ya Starbucks na mamia ya migahawa ya McDonald nayo imefungwa. Maduka makubwa kama vile Uniqlo na Ikea nayo yamefungwa.

Kama tulivyoona awali, sekta ya usafiri, hasa usafiri wa anga, nayo imeathiriwa sana na ugonjwa huu. Nchi kadhaa zimetoa maonyo kwa raia wake kuhusiana na kusafiri kwenda China.

Mashirika kadhaa ya ndege yamesitisha safari zake kwenda China. Mashirika ya Lufthansa, Swiss na Austria yamefuta safari zake za ndege kwenda China Februari 29 mwaka huu. Mashirika hayo hayawezi kulaumiwa kwani hata Serikali ya China yenyewe imewaonya raia wake dhidi ya kusafiri nje ya nchi. Pia China imepiga marufuku watu kusafiri katika makundi makubwa ndani ya nchi.

Hadi wiki iliyopita ofisi kadhaa na viwanda viliendelea kufungwa. Kampuni kadhaa za kutengeneza magari kama vile Volkswagen, BMW, Volvo, Toyota na Tesla, waliendeleza muda wao wa kusitisha uzalishaji katika kipindi cha mwanzo wa mwaka. 

Aidha, kampuni kubwa ya kusafisha mafuta ya China imepunguza uzalishaji kwa takriban mapipa 600,000 kwa siku kutokana na kushuka kwa mahitaji.

Funzo kutoka kwa SARS

Homa ya SARS ilipoikumba China miaka 17 iliyopita, biashara katika nchi hiyo ziliathirika sana na masoko ya hisa yakaporomoka. Athari wakati huo zilikuwa kwa China tu, lakini hivi sasa uchumi wa China umeunganika sana na wa dunia, hivyo athari zinaweza kusambaa katika nchi nyingi sana. Wakati wa SARS, China ilikuwa inamiliki asilimia tano tu uchumi wa dunia lakini hivi sasa China inamiliki zaidi ya asilimia 16 ya uchumi wa dunia.

Hivi sasa China, ambayo ni nchi ya pili kubwa kiuchumi duniani, ni mzalishaji, msafirishaji na mwagizaji wa bidhaa muhimu sana. Mathalani, China ni soko kubwa la bidhaa kutoka Ujerumani, pia China ina viwanda kadhaa ambavyo vinazalisha bidhaa kwa ajili ya viwanda vya Ujerumani. Kwa ujumla, China ni mzalishaji wa bidhaa nyingi zinazosambazwa duniani leo hii.

Mtaalamu mmoja wa uchumi nchini Ujerumani, Timo Wollmershäuser, anaamini kuwa madhara ya kirusi cha Corona kiuchumi yatakuwa makubwa zaidi ya madhara yaliyotokea kipindi cha SARS. Ugonjwa wa SARS, ambao ulidumu kwa miezi sita kabla haujadhibitiwa, ulishusha ukuaji wa pato (GDP) la China kwa asilimia moja, kiasi ambacho ni kidogo sana na nchi nyingi duniani hazikutikisika kutokana na hilo.

Lakini baada ya hapo, umuhimu wa China katika uchumi wa dunia umekua sana, kasi ya kusambaa kwa virusi hivyo ni kubwa na serikali nyingi duniani, ikiwamo ya China, zimekwisha kuanza kuchukua hatua kali za tahadhari. Hii yote inadhihirisha kuwa madhara ya Corona yanaweza kuwa makubwa sana.

Hata hivyo, wataalamu wengi wanaamini kuwa hivi sasa ni mapema mno kuanza kufanya uchambuzi wa kiwango cha athari za kiuchumi zitakazotokana na kirusi cha Corona. Jens Hildebrandt, Mkurugenzi wa Baraza la Biashara nchini Ujerumani aliiambia DW kuwa hivi sasa China ni kama imesimama kiuchumi kutokana na sherehe za mwaka mpya na sherehe za kipindi cha machipuo.

Kwa kawaida, shughuli nyingi za kiuchumi husimama katika kipindi hiki nchini China isipokuwa sekta ya utalii. Hivyo, inabidi kusubiri hadi kipindi ambacho shughuli za kiuchumi zinaanza kushamiri na hapo ndipo madhara ya Corona yanakapodhihirika.

Madhara hasa ya kirusi cha Corona yatajulikana baada ya kumalizika kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka nchini China, pale viwanda vingi vitakapofunguliwa nchini humo. Serikali ya China ilisogeza mbele sherehe hizo hadi Februari 2 na Februari 9 katika maeneo mengine.

Baada ya sherehe hizo ndipo viwanda vinatarajiwa kufunguliwa. Kwa kawaida, wafanyakazi wengi viwandani wanatokeo katika Jimbo la Wuhan na majimbo ya karibu. Jimbo hilo hivi sasa limo katika karantini, kwa maana kuwa hakuna mtu anaruhusiwa kutoka au kuingia karika eneo hilo.

Hivyo, viwanda vitakapofunguliwa ndipo itajulikana ni kwa kiasi gani shughuli za uzalishaji viwandani zitaathirika kutokana na kukosa wafanyakazi. Kuathirika kwa uzalishaji nchini China kunamaanisha pia usambazaji wa bidhaa kwenye masoko duniani kote utaathirika pia.

Kirusi kilivyoibuka

Kwa mara ya kwanza China ilitoa taarifa kwa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kuhusiana na kirusi cha Corona Disemba 31, mwaka jana. China ilisema kulikuwa na watu kadhaa walioshambuliwa na matatizo ya kupumua katika jimbo la Wuhan, ambalo lina jumla ya wakazi milioni 11.

Wakati huo, chanzo cha ugonjwa hakikujulikana na watalaamu wa afya ulimwenguni wakaanza kufanya utafiti ili kubaini chanzo hicho. Ikaja kubainika kuwa kirusi hicho kilianzia katika soko linalouza vyakula vya baharini katika jiji hilo, ambalo lilifungwa mara moja. Wakati huo, idadi ndogo tu ya watu 40 ndio waliripotiwa kuwa na matatizo hayo.

WHO imetangaza kuwa tayari virusi vya Corona vimegundulika katika nchi 24 duniani nje ya China ambako watu 176 wameathirika. Watu wawili tayari wamekwisha kupoteza maisha katika nchi hizo, akiwamo mmoja kutoka Hong Kong na mwingine huko Philippines. 

Hao wote walishawahi kutembelea Jimbo la Wuhan, ambako kirusi hicho kilianzia. Wataalamu wa afya wa Hong Kong waligoma wiki iliyopita kushinikiza mpaka kati yake na China ufungwe kabisa ili kupunguza kasi ya virusi hivyo kusambaa katika nchi yao. 

Mgomo huo ulishika kasi baada ya kufariki dunia mtu aliyeambukizwa virusi hivyo. Hadi wiki iliyopita, tayari watu 18 walikuwa wamekwisha kuthibitishwa kuambukizwa kirusi hicho huko Hong Kong, wakiwamo watu wanne ambao waliambukizwa kutoka kwa watu wengine nchini humo.

Kuibuka kwa kirusi cha Corona kunawakumbusha watu wa Hong Kong kuibuka kwa kirusi kingine kilichojulikama kama Severe Acute Respiratory Syndrome (SARS) mwaka 2003, ambapo karibu watu 300 walifariki dunia. Carrie Lam, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Jiji la Hong Kong, ameagiza kufungwa kwa vivuko vingi vya mipakani upande wanaopakana na China, lakini bado baadhi ya vivuko vinafanya kazi.

Ifahamu Coronavirus

Kwa mujibu wa Kituo cha Kudhibiti Magonjwa nchini Marekani (CDC), maambukizi ya kirusi cha Corona (2019-nCoV) yalionyesha dalili chache za wazi wakati kwa watu wengine walioambukizwa hawakuonyesha dalili kabisa. Dalili za wazi zilizoainishwa ni pamoja na: homa, kikohozi na kubana kwa pumzi. Lakini zipo dalili nyingine nyingi kama inavyoonyeshwa kwenye mchoro.

CDC inaamini kuwa dalili za maambukizi zinaweza kuanza kujionyesha baada ya kati ya siku mbili na siku 14 baada ya mtu kuambukizwa.

Kinga

Hadi wiki iliyopita hakukuwa na kinga mahususi kwa ajili ya kirusi cha Corona. Njia kubwa ya kujikinga ni kujiweka katika mazingira ambayo hayatakuwezesha kukutana na kirusi hiki. Hata hivyo, CDC inapendekeza kuwa katika maeneo ambayo yana maambukizi, watu wakahikikishe wanajikinga kila mara kwa kufanya yafuatayo:

– Kuosha mikono kwa sabuni na maji kwa takriban sekunde 20. Hii ifanyike baada ya kwenda maliwato, kabla ya kula na baada ya kupenga makamasi, kukohoa na kupiga chafya.

– Kama maji na sabuni havipo, unaweza kutumia pombe kali ambayo kiwango chake cha kilevi kinazidi asilimia 60.

– Jizuie kushika macho na mdomo iwapo mikono yako ni michafu.

– Jizuie kushikana na watu walioambukizwa.

– Kama umeambukizwa, usitembee ovyo nje, kaa ndani.

– Unapokohoa au kupiga chafya, hakikisha unaziba kinywa na pua kwa kitambaa au karatasi na tupa kitambaa au karatasi hiyo mara moja.

– Safisha vema vitu ambavyo umevigusa.

Kusambaa

Hadi wiki iliyopita, wataalamu walikuwa hawana taarifa za uhakika jinsi coronavirus mpya inavyosambaa. Taarifa zilizopo zinatokana na taarifa za jumla kuhusu coronavirus.

Coronavirus vipo katika familia ya virusi ambavyo vinapatikana katika aina nyingi za wanyama kama vile ngamia, ng’ombe, paka, popo na wengineo. Hata hivyo, ni jambo la nadra sana kwa coronavirus kutoka kwa wanyama hawa kumwambukiza binadamu kama ilivyo kwa virusi vingine kama vile MERS, SARS na sasa kirusi kipya cha coronavirus.

Kwa kawaida, virusi hivi huambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine kwa kukaribiana sana (kwa umbali wa kama futi sita hivi). Maambukizi kutoka mtu kwenda kwa mtu mwingine hufanyika kupitia matone ya majimaji yanayotoka kwa mtu anapokohoa au kupiga chafya, kama ambavyo mafua yanaambukiza.

Wataalamu bado hawajathibitisha iwapo mtu anaweza kuambukizwa kirusi kipya cha coronavirus kwa njia ya kugusana.

Lakini ni muhimu kufahamu kuwa njia za maambukizi kutoka kwa mtu kwenda kwa mtu mwingine zinatofautiana. Baadhi ya virusi vinaambukiza kwa kasi (kama surua) wakati vingine haviambukizi kwa kasi.

Matibabu

Hadi wiki iliyopita hakukuwa na matibabu mahususi ya coronavirus. Lakini wataalamu kutoka China walitangaza wiki iliyopita kuwa wamegundua tiba ya virusi hivyo.

Hata hivyo, wataalamu wanashauri kuwa mara mtu anapoanza kuona dalili za ugonjwa huu ahakikishe anakwenda hospitali na kuonana na wataalamu ili kufanyiwa vipimo. Ni muhimu kufanyiwa vipimo ili kuthibitisha maambukizi kwa sababu dalili za coronavirus zinafanana na dalili za aina nyingi za maambukizi mengine.

Ili kuzuia kuwaambukiza watu wengine, fanya yafuatayo:

– Usisafiri ukiwa na maambukizi.

– Mara zote, toka nje kama ni muhimu kufanya hivyo.

– Hata ukiwa nyumbani usichangamane na watu wasioambukizwa.

– Unapotoka nje vaa mask ya kuzuia kinywa na pua. 

– Unapokohoa na kupiga chafya, zuia kinywa kwa karatasi au kitambaa.

– Kila mara osha mikono yako.

– Usitumie vitu na watu wengine katika familia iwapo umeambukizwa.

– Usiguse wanyama wa kufugwa nyumbani kama vile paka.

By Jamhuri