Home Makala Ndugu Rais, maumivu ya kichwa huanza polepole

Ndugu Rais, maumivu ya kichwa huanza polepole

by Jamhuri

Ndugu Rais, maumivu ya kichwa huanza polepole sana lakini yakiachwa yaendelee hufikia mahali yakawa makubwa sawa na nyundo inayogonga kichwani. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akisalimiana na Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Dk. Inmi Patterson. Marekani imeijumuisha Tanzania katika orodha ya nchi ambazo wahamiaji wake wamezuiwa kuingia nchini humo.

Maumivu yetu ya kichwa yalianza polepole sana mara tu Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani. Tuliruhusu yaendelee na sasa yamekuwa makubwa sawa na nyundo inayogonga kichwani. Hayawezi tena kutulizwa kwa vidonge.

Lakini Baba wa Taifa aliliona hili, alionya akasema: “Watu walio hatarini sana ni wale ambao wanafikiri kuwa wanajua kila kitu, wala hawana haja kujifunza zaidi. Hii ni tabia mbaya ambayo huzuia kabisa maendeleo.” Waonyesheni basi Watanzania maendeleo mliyowaletea katika miaka hii minne yako wapi?

Watanzania na nchi yao hawako tena kama walivyokuwa awali kabla ya ujio wa Serikali ya Awamu ya Tano. Serikali ya Awamu ya Tano katika miaka yake hii minne imebadili mwelekeo wa nchi, imewabadili Watanzania kifikra na mtazamo wao kwa serikali yao na kwa baadhi ya viongozi wao.

Wako baadhi ya wananchi wanaowaona baadhi ya viongozi wao kuwa ni watu hatari! Kiongozi anashiriki kumpakia mgonjwa katika ndege aende kutibiwa nje halafu kiongozi huyo huyo analitangazia taifa kuwa hajui mgonjwa huyo aliko. Wanaotilia shaka umakini wake wanakosea wapi?

Mtazamo wa wananchi kwa serikali yao katika Awamu ya Kwanza ya uongozi wa taifa letu ulikuwa na hofu ya uwepo wa Mwenyezi Mungu. Waumini wa kweli wa dini zote zamani walijua kuwa hapa duniani baada ya Mwenyezi Mungu kimbilio lao la kweli walikuwa viongozi wao wa dini. Nimesema zamani na nimesema viongozi wa dini zote. Walitoa huduma zao, nao walikaripia, wakanena kwa uvumilivu. Bali wao walikuwa na kiasi katika mambo yote.

Baada ya viongozi wa dini ndiyo walifuata viongozi wa serikali. Amani ilitamaliki katika nchi. Na ilitamalaki si katika nchi tu, bali hata katika vifua vyote vya wananchi. 

Wanyama wa porini, samaki wa majini na ndege wa angani ukiwaona hakuna hata mmoja ambaye ungemdhania kuwa hakuwa na amani kifuani mwake. Hii yote iliidhihirisha ile kweli kuwa duniani si mahali pa mateso.

Ole wao kama kuna waliotuletea mateso katika nchi yetu. Watambue kuwa tangu kuumbwa kwa ulimwengu Marekani haijawahi kumwachia mtu iliyomuingiza katika kundi la wauaji wa kidunia.

Zamani, kwetu watu na mizigo, walisafirishwa kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine kwa kutumia malori. Ndani ya kila lori kulikuwa na vifaa vya kusaidia shida ikitokea. Kulikuwa na magogo ambayo wakati wa dharura yalitumika kama breki. Lakini muhimu zaidi ndani ya kila lori kulikuwa na jeki.

Jeki zile zilikuwa kubwa, nzito, abiria wa kawaida hawezi kuibeba peke yake. Sijui zilianzia wapi, lakini zote ziliitwa Tanganyika jeki. Zilikuwa madhubuti kweli kweli.

Polisi wa siku zile walikuwa wanatumia virungu badala ya bunduki. Walipomshika mtuhumiwa walishika sehemu anayovalia mkanda wa suruali yake halafu wanaiinua juu, hivyo mtuhumiwa anakosa balansi, maana juu hayuko na chini pia hayuko! Atakwenda watakako! Hili ndilo lililotusibu! Tutakwenda watakako Marekani. Marekani kututuhumu mbele ya dunia ya Mwenyezi Mungu, tuhuma nzito kuwa tumewanyima baadhi ya wananchi haki yao ya kuishi, ametupiga Tanganyika jeki. Tutapataje kupona? Hapa haponi mtu.

Kutuhumiwa si kuhukumiwa. Lakini tuhuma za mauaji ni nzito mno. Tangu kupatikana kwa Uhuru katika nchi hii tulikuwa hatujawahi kutuhumiwa na dunia kwa kuua watu. Hili ni kubwa mno. Wanasema tumewanyima watu haki yao ya kuishi, yaani kwa maneno sahihi, tumeua watu!

Hawajasema ni wangapi lakini wamesema ushahidi wanao! Nchi imefika penye fundo! Walisema mwanadamu ni mnyama ambaye akiamua kuwa mwovu anakuwa mwovu kuliko shetani.

Wanawema nchi inahitaji mchango mkubwa, tena sawa na ule alioutoa Kinana. Leo Abdulrahman haupo, lakini elewa kuwa kama unakashfiwa hiyo ni kazi uliyoifanya kwa mikono yako. Ungeiacha CCM iende hao ungekutana nao wapi mpaka wakutukane?

Kama ni kuihubiri habari njema ya upendo, mshikamano na maridhiano katika nchi hii, tumeihubiri sana na nyinyi wote ni mashahidi. Mahubiri yetu yamekuwa sawa na yale ya mpanzi aliyekwenda shambani mwake kupanda mbegu. Ziko zile mbegu zilizoanguka juu ya mwamba nao ndege walikuja na kuziokota wakazila. Zipo zile zilizoanguka katika udongo mkavu zikanyauka kwa kukosa maji. Lakini baadhi kama Abdulrahman Kinana zilianguka katika udongo mzuri lakini zilipoanza kuota miiba ilizisonga nazo hazikuendelea kukua.

Ilikuwa haijawahi kutokea, lakini Kinana hakunong’ona, alitamka hadharani na kila maskini na mnyonge wa nchi hii alisikia na kuwaona mawaziri aliowaita kuwa ni mizigo kwa maskini wa nchi hii. Wenye mamlaka hawakuziondoa nta katika masikio yao.

Mtu huyu aliviacha vyote vyema na vitamu vya nyumbani kwake pamoja na familia yake, akatembea kijiji hadi kijiji nchi nzima akiwagusa maskini na wanyonge kwa mikono yake. Kinana hakuwapa fedha kama tunavyoshuhudia baadhi ya viongozi wanavyomwaga fedha nyingi zilezile za maskini katika ziara zao ambazo zingewasaidia. Bali aliwapa faraja!

Aliwaambia iko siku taabu zao zitapata mtu wa kuzitatua. Walipomuuliza unataka nini kwetu huku kwa maana mioyo yetu imepondekapondeka? Wakila matembele pamoja, alilalia vitanda vya kamba kama wao huku akioga maji ya ndoo kama wao, Kinana aliwaomba maskini na wanyonge wa nchi hii wakilegezee Chama Cha Mapinduzi mioyo yao. Walikuwa wamekwisha kifuta katika vifua vyao. Maskini na wanyonge wa nchi hii walimsikiliza, wakamwamini, wakampa alichokitaka.

Kama leo ziko habari kuwa mtu huyu anakashfiwa na walewale aliowafanya wawe vile walivyo sasa, Abdulrahman Kinana pamoja na imani yako katika dini, waulize wanaomwamini Yesu Kristu, Yesu alikosa nini mpaka astahili adhabu kali ile ya kifo cha msalaba?

Waliosema huyu ni Nabii na wengine wakasema huyu ni mtabiri wakumbuke vema kuwa ni mchezaji hodari tu wa bao. Kesho njooni wote tuicheze kete ya mwisho itakayomaliza mchezo. Tuwashuhudie wale waliokataa ushauri tulipowaambia kuwa mpapai hauwezi kuwa nguzo ya kushika nyumba watakavyokuwa wanahangaika kuziokoa roho zao kutoka katika hii Tanganyika jeki ya Marekani.

You may also like