Makala hii ilianza wiki iliyopita ambapo ilielezwa kuwa kiujumla kuwa neno ‘Wasatwiyya’ linapata maana ya wastani, usawa, ukati na kati na ubora. Uislamu unahimiza ‘Wasatwiyya’ katika kila jambo kwa kuwa hata dini yenyewe ni dini ya ‘Wasatwiyya’; Dini ya Wastani; Dini ya Kati na Kati.

Mifano inayoonyesha kuwa ‘Uislamu ni Dini ya Wasatwiyya’ ilitolewa ikiwemo namna Uislamu ulivyokusanya pande zote mbili za kimaada na kiroho; namna ilivyoweka mazingira wezeshi ya kutekelezwa kwa sheria mbalimbali na kwa mkabala wake makala ilieleza changamoto inayowakabili wanaume Waislamu pale wanapowaacha wake zao kwa mujibu wa mafundisho ya dini ya Uislamu na ikathibitika kidini kuwa wameachika, wakati kwa mujibu wa Sheria ya Ndoa ya Tanzania ya Mwaka 1971, wanawake hao wanakuwa hawajaachika, kwani mahakama pekee, kwa mujibu wa sheria hiyo, ndiyo yenye mamlaka ya kutoa talaka au kuvunja ndoa.

Makala iliwaomba viongozi wa dini, wanasheria na serikali kukaa pamoja na kuiangalia changamoto hii ambayo inawatesa wengi na kuwaingiza katika kuvunja sheria ya nchi huku wakiwa wametekeleza sheria ya dini yao.

Leo tuendelee kuangazia ‘Wasatwiyya’ katika Uislamu.

Wasatwiyya katika Uislamu unadhihiri katika suala la kuitangaza dini ya Kiislamu na kuwalingania watu kufuata njia inayomridhisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani). 

Katika hili, mlinganiaji (muhubiri wa Kiislamu) hana budi kutumia njia iliyo bora na ya wastani inayozingatia kanuni aliyoielekeza Mwenyezi Mungu itumike kwenye kazi hii. Kanuni hii adhimu tunaisoma katika Qur’aan Tukufu Sura ya 16 (Surat An-Nahl), Aya ya 125 kuwa: “Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako Mlezi kwa hekima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora. Hakika Mola wako Mlezi ndiye anaye mjua zaidi aliyeipotea njia yake, na Yeye ndiye anayewajua zaidi walioongoka.”

Hivyo wajibu wa mlinganiaji ni kuzungumza na watu kwa njia ya wastani katika mambo yote yanayoihusu dini, iwe katika elimu, utoaji wa hukumu na kulingania, kwa kuwa Uislamu unakataza kufanya mambo kwa kupita kiasi, misimamo mikali na ushadidivu katika maeneo yote na kuacha kufanya haraka ya kutaka kuchuma matunda ya kazi ya kulingania, akizingatia kuwa wajibu wa mlinganiaji ni kufikisha ujumbe tu, si kuongoka kwa yule aliyemfikishia ujumbe.

Na hili ndilo alilolibainisha Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake kama tunavyosoma katika Qur’aan Tukufu Sura ya 5 (Surat Al-Maida), Aya ya 99 kuwa: “Haimlazimu Mtume ila kufikisha ujumbe tu. Na Mwenyezi Mungu anajua mnachokidhihirisha na mnachokificha.”

Tunasoma pia katika Qur’aan Tukufu Sura ya 42 (Surat Ash-Shuraa), Aya ya 48 kuwa: “Na wakipuuza, basi Sisi hatukukupeleka ili uwe mwangalizi wao. Si juu yako ila kufikisha Ujumbe tu…”

Tunasoma pia katika Qur’aan Tukufu Sura ya Pili (Surat Al-Baqara), Aya ya 272 kuwa: “Si juu yako wewe kuwaongoa, lakini Mwenyezi Mungu humwongoa amtakaye…”

Naam, Mwenye kuongoa ni Mwenyezi Mungu tu, kama tunavyosoma pia katika Qur’aan Tukufu Sura ya 28 (Surat Al-Qasas), Aya ya 56 kuwa: “Kwa hakika wewe humwongoi umpendaye, lakini Mwenyezi Mungu humwongoa amtakaye. Na Yeye ndiye anawajua zaidi waongokao…”

Mpaka hapa Uislamu umedhihirisha ni Dini ya Wasatwiyya kwa kumuelekeza mlinganiaji anayewaita watu katika Uislamu kuzingatia kanuni kuu ya kutumia hekima na mawaidha mema na kujadiliana kwa njia iliyo bora.

Ukimuona mlinganiaji wa Kiislamu amejitenga na hekima na anatumia kwenye mawaidha yake lugha za kuudhi, kukejeli na kuamsha hamaki, basi huyo hauwakilishi Uislamu kwa sababu hafuati mafunzo ya Uislamu na kanuni ya kulingania kwa hekima na mawaidha mema.

Kadhalika, ukimuona mlinganiaji hazingatii kuwa wajibu wake ni kufikisha ujumbe tu na kuongoka ni kutaka kwake Mwenyezi Mungu, basi ujue huyo ni mlinganiaji aliyevamia kazi ya kulingania bila ya kuwa na elimu na mafunzo ya kutosha kufanya kazi hiyo.

Wasatwiyya katika Uislamu unadhihiri pia katika maadili na tabia njema. Uislamu umechukua msimamo wa kati na kati katika maadili na tabia njema baina ya makundi mawili; kundi lililochupa mpaka likamtukuza mwanadamu kwa kiwango asichostahili na kundi lililomdhalilisha mwanadamu na kumhesabu kama mnyama.

Uislamu ukasisitiza kuwa ubinadamu wa mtu, yaani utu wa mtu, utapimwa kwa kuwa kwake ni mwenye tabia njema na si vinginevyo. Hivyo Uislamu ni tabia njema na Mtume Muhammad amesifiwa na Mola wake Mlezi kuwa ni mwenye tabia njema mno kama tunavyosoma katika Qur’aan Tukufu Sura ya 68 (Surat Al-Qalam), Aya ya 4 kuwa: “Kwa hakika una tabia njema mno.”

Tabia njema ndizo zinazouweka Uislamu na Muislamu kwenye daraja ya juu kabisa. Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) amesema: “Kwa hakika nimeletwa ili nikamilishe tabia njema.” Maneno haya ya Mtume Muhammad yanaonyesha kuwa suala la tabia njema limekusanya umuhimu wote aliokuja nao. Ni kusema kuwa: Dini hii yote ni tabia njema. Itoshe pia kwamba tabia njema ndiyo itakayopelekea watu kuingia peponi kwa wingi kama alivyosema Mtume Muhammad katika hadithi iliyopokewa na Abu Hurayrah (Allaah Amridhie), amesema: “Na aliulizwa ni kitu gani kitakachowaingiza watu kwa wingi peponi?” Akasema: “Kumcha Allah na tabia njema” na akaulizwa tena ni kitu gani kitakachowaingiza watu wengi kwa wingi motoni? Akasema: “Kinywa (mdomo) na utupu.” (Hadithi hii inapatikana katika kitabu cha Hadithi za Mtume Muhammad kiitwacho Sunanu At-Tirmidhiy).

Kinyume cha tabia njema ni tabia mbaya, ambayo humsababishia mtu kuchukiwa na Mwenyezi Mungu. Tunasoma katika hadithi iliyopokewa na Abu Dardaa (Allaah Amridhie) kwamba Mtume (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) amesema: “Hakuna kitu kizito katika mizani ya muumini siku ya Qiyaama kuliko tabia njema. Hakika Allah humchukia mtu muovu mwenye tabia mbaya.” (Hadithi hii inapatikana katika kitabu cha Hadithi za Mtume Muhammad kiitwacho Sunanu At-Tirmidhiy).

Tuzingatie kuwa ubora wa mwanadamu na hususan muumini ni kujipamba kwake na tabia njema. Tunasoma katika hadithi itokanayo na Abdullaah bin Amru bin Al-Aaswi (Allaah Amridhie) amesema, alikuwa Mtume (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) akisema: “Hakika aliye bora kati yenu ni yule mwenye tabia njema.”

Kama nilivyotangulia kueleza, Wasatwiyya (wastani) katika Uislamu umeenea katika mambo yote ikiwemo ibada.

Katika ibada tunasoma hadithi kutoka kwa Anas (Allaah Amridhie) amesema: Wageni watatu walikuja katika nyumba za wake wa Mtume (Allaah Awaridhie) kuja kuuliza kuhusu ibada ya Mtume (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) na walipoelezwa wakawa kama kwamba wamejiona ni wadogo wakasema: “Tuko wapi sisi na Mtume? Amekwishasamehewa madhambi yaliyotangulia na yaliyochelewa.”

Na mmoja wao akasema: “Ama mimi nitaswali swala za usiku milele. Mwingine akasema: “Mimi nitafunga na wala sitofuturu. Na wa mwisho akasema: “Ama mimi nitajiepusha na wanawake na sitooa milele.”

Mtume (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) akawaendea akasema: “Ni nyinyi mliosema hivi na hivi. Ama mimi naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu ninamuogopa Mwenyezi Mungu kuliko nyinyi nyote lakini ninafunga na kufuturu, ninaswali na kulala na ninaoa wanawake, na mwenye kujiweka mbali na mwenendo wangu basi hayuko nami.” (Hadithi hii inapatikana katika kitabu cha Hadithi kiitwacho Sahih Al-Bukhari.)

Tuhitimishe makala hii kwa kusisitiza kuwa Wasatwiyya, kwa mujibu wa Uislamu, unatakiwa uwepo katika kila kitu hata katika kula, kunywa, kuvaa na matumizi ya maji.

Uislamu unamtaka mtu asifuje wala asijinyime. Mfano mzuri unaoieleza Wasatwiyya tunausoma katika Qur’aan Tukufu Sura ya 17 (Surat Al-Israa), Aya ya 29 kuwa: “Wala usiufanye mkono wako kama uliofungwa shingoni mwako, wala usiukunjue wote kabisa, utabaki ukilaumiwa mufilisi.”

Naam! Kwa kuwa ubora wa mambo ni wastani (kati na kati) basi tukumbushane kufanya mambo katika kiwango cha wastani. Ukila kula kwa wastani na zingatia mafundisho yasemayo: “Sisi ni watu, hatuli hadi tuwe na njaa, na tukila hatushibi.” Shime tuwe watu wa wastani hata katika kuvaa kwetu. Na kutokana na umuhimu wa maji kama tunavyosoma katika Qur’aan Tukufu Sura ya 21 (Surat Al-Anbiyaa), Aya ya 30 kuwa: “…Na tukajaalia kwa maji kila kilicho hai…”

Naam! Maji ni uhai, basi tufanye Wasatwiyya katika matumizi yetu ya maji. Uislamu umehimiza hilo na tunamuona Mtume Muhammad akimtaka Swahaba Sa’ad asitumie maji zaidi ya mahitaji (Israaf). Swahaba Sa’ad alimuuliza Mtume: “Katika kuchukua Udhu kuna Israaf pia.” Mtume akasema: “Ndiyo hata ukiwa katika maji ya mto yanayopita.” Imepokewa hadithi kuwa Mtume Muhammad alitawadha mara tatu tatu kisha akasema: “Huu ndio Udhu, atakayezidisha basi atakuwa amefanya vibaya, amevuka mpaka na amedhulumu.”

Haya tukutane Jumanne ijayo In-Shaa-Allaah.

Sheikh Khamis Mataka ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata).

Simu: 0713603050/0754603050

660 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!