*ADC yasema ni udhalilishaji uliopindukia

Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) kimetishia kuifikisha Serikali mahakamani, ikiwa haitakomesha utaratibu wa watuhumiwa kujisaidia kwenye mtondoo mbele ya wenzao katika vituo vya polisi nchini.

Kamishna wa ADC Kanda ya Ziwa, Shaban Itutu, amesema huo ni udhalilishaji unaokiuka tamko la kimataifa linalozitaka nchi kulinda haki na utu wa binadamu.


“Watuhumiwa wanadhalilika sana kule polisi, wanajisaidia haja ndogo na kubwa mbele ya wenzao wakiwatazama. Huu ni udhalilishaji mkubwa wa utu na ni kinyume cha haki za binadamu.

 

“ Kama hiyo haitoshi, kila siku asubuhi watuhumiwa hao wanatwishwa mtondoo kuupeleka kuumwaga nje huku kinyesi kikiwamwagikia,” amesema Itutu katika mazungumzo maalumu na Jamhuri, wiki iliyopita.

 

Anaongeza, “Ndiyo maana vituo vyetu vyote vya polisi unapokwenda kumsalimia ndugu au rafiki yako, ukisogeza pua eneo alipo shombo inayotoka humo siyo ya kawaida, na hata mtu akitoka humo nguo alizokuwa amevaa hawezi kuendelea kuzivaa tena hadharani kwa sababu zinanuka kinyesi na mkojo.”

 

Itutu anaeleza kusikitishwa kwake na taswira inayoonesha kuwa wakoloni waliwajali Watanzania kiasi cha kuona umuhimu wa kujenga vyoo vya ndani kwa ajili ya mahabusu, lakini baada ya nchi yetu kupata Uhuru, Serikali imevitelekeza.

 

“Siku hizi kuna vituo vya polisi ambavyo mkoloni aliondoka akaviacha vikiwa na vyoo vya ndani, lakini kwa sasa miundombinu ile imekufa, watu wanadhalilika kwa kujisaidia kwenye mtondoo (ndoo) hadharani,” anasema na kuendelea:

 

“Nimegundua kumbe mkoloni aliwathamini Watanzania pamoja na kwamba alikuwa anawatawala, lakini leo Serikali ya Tanzania inashindwa kuwathamini Watanzania.

 

Kwa sababu wanaposhikiliwa katika vituo vya polisi wanakuta hakuna vyoo, hata chakula ni tabu katika baadhi ya vituo.

 

“Kwa sababu hiyo, nimemwandikia Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi barua ya kumhimiza achukue hatua za kutatua kero hiyo haraka, lakini kama Serikali itapuuza hilo , nitaifungulia mashitaka mahakamani kwa kuvunja haki za binadamu.

 

Jamhuri inayo nakala ya barua hiyo ya Desemba 3, mwaka huu, iliyotumwa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na nakala yake kupelekwa kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) nchini.

 

“Nimeamua kufanya hivyo kwa sababu hata Katiba yetu katika Ibada ya 9, kifungu (f), inatambua Tangazo la Dunia la haki za binadamu, linaloitaka kila Serikali kuhakikisha haivunji haki ya mtu yeyote, wala kumdhalilisha utu wake,” anasema.

 

Mbali ya kudhalilika utu wao, kitendo cha watuhumiwa kujisaidia kwenye ndoo moja kinawaweka katika hatari ya kuambukizana maradhi mbalimbali.

 

“Nilimuuliza RPC (Kamanda wa Polisi wa Mkoa) mmoja kwamba ikitokea wewe ukawekwa ‘ndani’ kama Kamanda Zombe alivyowekwa ‘ndani’ kuhusiana na kesi ya wafanyabiashara wa madini wa mkoani Morogoro (waliouawa kwa kupigwa risasi), ukajisaidia hapo (kwenye mtondoo) na cheo chako hicho, halafu asubuhi ukatwishwa huo mtondoo, utajisikiaje? Kimsingi najua hawezi kujisikia vizuri, kwa kweli ni hali ya kudhalilishwa,” anasema Itutu.

 

Kiongozi huyo wa ADC Kanda ya Ziwa anataka kero hiyo itazamwe kama tatizo la kitaifa, na mamlaka husika zichukue hatua za makusudi kuharakisha ujenzi wa vyoo vya ndani kwa ajili ya mahabusu katika vituo vyote vya polisi nchini.

 

Anaishauri Serikali kwamba kama itakuwa tayari kuanza ujenzi wa vyoo katika vituo vyote vya polisi, iwahamishe watuhumiwa kutoka vituo vya polisi kwenda magerezani ambako kuna vyoo vya ndani; wakati kero hiyo ikitafutiwa ufumbuzi. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, alipoombwa na Jamhuri kuzungumzia suala hilo alimtupia mzigo huo IGP Said Mwema.

 

Kwa upande wake, IGP Mwema amemtaka mwandishi aandike maswali na ayapeleke kwa Msemaji Mkuu wa Jeshi la Polisi, ambaye ni Advera Senso.

By Jamhuri