Ndugu Watanzania wenzangu na Wizara ya Maliasili na Utalii, kwanza naomba kusema jambo moja kama Mtumishi wa Mungu, ambaye nimeitwa naye kwa maslahi ya mbingu, ili kuijenga jamii na umma kimaadili. Nitasimama siku zote katika “kweli” na hiki ndicho “kiapo changu” ee Mungu tusaidie.

Baada ya kiapo kinachoashiria ushindi mkubwa katika kampeni ya kutokomeza ujangili, sasa tupeane pole sisi kwa sisi kama wadau wakuu wa uhifadhi na wanyamapori na tuendelee kuelimishana katika kweli na kupata taarifa kupitia vyombo vya habari hususani Gazeti JAMHURI kuhusu wanyamapori wetu huko maporini.

Lakini pia niwape hongera wadau kama TANAPA, NCAA hasa kwa viongozi waadilifu tunaowafahamu, zaidi askari pori waadilifu. Tuna kila sababu za kusema kilio cha wanyamapori kimepata majibu, sasa ujangili kwa heri.

Huenda jambo hili linaweza kutokuingia mara moja akilini mwako maana bado una picha kamili ya ujangili na vitisho vingi vya mauaji kimtandao, na wakati mwingine ukiamini kuwa mtandao unaojihusisha na hali hii ni kama Boko Haram, au watu wenye nguvu na mamlaka ambao baadhi yao wamejificha nyuma ya madaraka ya nchi na kadhalika.

Ni kweli sina sababu ya kuihukumu akili yako au fikira zako, ila sasa amini, “na wala si kwamba nawafariji wadau”, hapana.  Kauli hii inaashiria amani kwa uhifadhi na wanyamapori wetu kwa ujumla, na ni vizuri tuwe tayari ndani ya mioyo yetu kuona ushindi kabla ya mechi, hatuwezi kuendelea kila wakati kuongelea ujangili, tuna sababu kamili za kuanza kuongelea ongezeko la pato la sekta ya utalii wa Tanzania.

Kabla ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kumpiga nduli Idi Amin Dada, alisema hivi; “Uwezo tunao, nia tunayo na sababu tunayo.” Kwa kauli hiyo fupi, matokeo ya vita ya Uganda tuliyaona wote, si kwamba hatukupata madhara, hapana, kwa sehemu tuliwapoteza mashujaa wetu, lakini mikononi mwetu tuliimiliki nchi ya Uganda baada ya Idi Amin kukimbilia Libya.

Nasi kama Watanzania, uwezo tunao na sababu za kutokomeza ujangili tunazo huko maporini kurudisha amani ya uhifadhi na wanyamapori wa Tanzania, ili tupokee tuzo ya World Wildlife Day ya kila mwaka, ambayo mwaka kesho itasherehekewa Machi 3.

Na ili upate matokeo safi ya uhifadhi, usichoke kufuatilia ukweli huu ndani ya JAMHURI kila wiki. Wakati huu unaweza kujiuliza ni nani huyu anayetoa tamko hili zito wakati hata wenyewe mamlaka ya nchi akili zao wakati mwingine zimefika mwisho bila suluhisho kamili? Usiwe na shaka, utamjua mkombozi wa maliasili zetu, amewasili mwenye kauli fupi “Ujangili Tanzania sasa basi,” na anayetuwazia Tanzania na Watanzania amani na utulivu kwa kila Mtanzania na kusahau kabisa suala la ujangili.

Tumekuwa na misuguano mikubwa kati ya rasilimali wanyamapori wetu na tuhuma za ujangili tangu siku nyingi. Tukianzia ukoloni hadi sasa kumekuwa na kero za uwindaji haramu wa viumbe adimu kama tembo, faru, simba kuendelea kutoweka na uuzwaji wa twiga, uvuvi haramu kwa kasi kubwa sana kuliko tunavyoweza kutathmini.

Mungu akiwa amenyamaza mkafikiri ni mjinga sana, si kwamba ni kwamba muumba hayaoni machozi na mateso ya wanyamapori huko maporini, anayaona na amekusudia kuwainua watu waadilifu kushika nyadhika Wizara ya Maliasili na Utalii na ndiyo maana nikasema ujangili sasa basi, hata wale mliwacheka kwa misimamo yao ili muendelee kufyeka misitu.

Mungu amekusudia kuwatumia tena na hii yote ni kwa sababu ya maombi ya watakatifu na wazalendo, ambao habari zao mnazisoma mara kwa mara magazetini, ambao kwa nia moja vita hii wameamua kumshirikisha na kumkabidhi kabisa Mungu ndiye awe mwamuzi wa kuleta amani Wizara ya Maliasili na Utalii hasa kwa wanyamapori, isiwe ni kazi ya Bunge au wanasiasa tu, ambao pia kila kukicha wanaonekana kutokidhi viwango vya utumshi wa umma.

Kitu ambacho naamini Tanzania kuna watu makini sana, waadilifu sana na weledi sana wenye maono makubwa ila uongozi na utawala, bado haujawapa nafasi watu wa namna hii, ambao kwa kampeni ya ‘Jitokeze Tuongee’ tumefanikiwa kukutana nao baadhi na kuketi pamoja  na watu hawa. Ni watu makini na wana maono makubwa kuhusu suluhisho la ujangili Tanzania.

Ni ukweli usiopingika kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii, tena iliyo maarufu, inatumia gharama kubwa sana kuwalinda wanyamapori na mazingira ya uhifadhi, wakati Watanzania wanaendelea kuwa maskini. Poleni sana kwa mikakati mizuri hiyo na inaonesha dhahiri kuwa wawekezaji wanajitahidi sana kuonesha mchango mkubwa wa “ufadhili” wa uhifadhi na kuthamini umuhimu wa wanyamapori na mazingira ya uhifadhi wa Tanzania. Hongera wadau wakuu huko ng’ambo ya nchi.

Acha tuwe wazi, tuna sababu ya kutoa pongezi kwa wizara. Yapo mazuri mnayafanya, ila tu baadhi yenu hamtaki kuheshimu ile hotuba ya Baba wa Taifa, kuwa hakuna Serikali isiyokuwa na “miiko”, shida huenda nanyi baadhi yenu hamtaki kuishi chini ya miiko ya nchi.

Kampeni ya ‘Jitokeze Tuongee’, inayoratibiwa na taasisi ya Rafiki Wildlife Foundation ya jijini Arusha kuhusu umuhimu wa uhifadhi na wanyamapori sanjari na kupinga mauaji ya wanyamapori, tumefanikiwa kukusanya maoni kwa wadau mbalimbali pamoja na kuelimisha jamii.

Tumefanikiwa kuonana na uongozi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hasa Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, mawaziri, wabunge (wanasiasa], viongozi wa dini,  vyombo vya ulinzi na usalama, watumishi wa umma, wanafunzi na wanavyuo, wanahabari, wakulima kwa wafungaji.

Katika maoni yao, karibu asilimia 85 walikiri na kukubaliana nasi, kuwa maono tuliyonayo ya elimu ya uhifadhi ni nuru, ipewe fursa ndani ya jamii ili kukabiliana na janga la ujangili au zaidi ya ujangili, ni kweli kutokana na uelewa mdogo wa Mtanzania kuhusu kujua moja kwa moja umuhimu wa uhifadhi na wanyamapori unaochangia asilimia kubwa kuongeza wimbi la ujangili.

Ni aibu kuona Mtanzania hajui sera za maliasili na utalii, tofauti kati ya hifadhi na vitalu, hajui tofauti ya TANAPA na NCAA, hajui nini maana ya TAWIRI na inafanya nini, hajui CITES, IUCN, UNDP, TATO ni chombo kinachohusika na nini, au ana mchango gani na vitengo hivyo kifursa.

Hawajui sekta ya utalii inachangia kwa kiasi gani pato la nchi, hajui haki zake zinazotokana na wanyamapori, kuhusu taarifa za sera za maliasili na utalii, majibu yao ni kubahatisha. Wako gizani. Katika mazingira kama hayo unadhani Mtanzania wa namna hiyo ataweza kukabiliana na ujangili? Au naye atakuwa sehemu ya jangili kwa kutokujua, na je, katika hili nani alaumiwe?

Kampeni ‘Jitokeze Tuongee’, iliyounda kikosi cha mabalozi wenye maadili wa maliasili na uhifadhi [volunteers] chini yangu imekusudia kwa dhati kuunga mkono Wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi nyingine husika, kuzunguka nchi nzima kuelimisha jamii na umma kwa ujumla kuhusu umuhimu wa uhifadhi na wanyamapori, sanjari na kupiga vita mauaji dhidi ya tembo na wanyamapori wengine.

Tunaomba wadau mbalimbali, wizara, taasisi, kampuni, watu binafsi kujitokeza kutuunga mkono na kutuwezesha kifedha, kivifaa ili tuweze kutokomeza ‘Ebola’. Hii ya ujangili huko porini kwa njia ya elimu ya jinsi ya kupambana na ujangili.

Nikukumbushe kidogo kuhusu janga hili. Mengi tayari yalishazungumzwa kupitia vyombo mbalimbali — Serikali na Bunge. Mengine yenye tija yameibuliwa na gazeti mahiri la JAMHURI ambalo kwa sasa wadau wanaliita mkombozi wa wanyamapori.

Waandishi wa habari wa gazeti hili hapa nchini na hata nje nchi wanaendelea kupambana na viongozi wasio waadilifu ambao ndiyo wakati mwingine wamekuwa vyanzo vya kuangamia kwa wanyamapori.

Mkakati wa Serikali wa kuwaokoa wanyamapori kwa njia za helikopita, vikao vya wadau, kuongeza nguvu kazi kwa kuajiri askari pori zaidi ya malengo, ni sawa, lakini bado havitazamiwi kukabiliana na changamoto la janga hili. Wadau jiulizeni na kumbukeni ‘Oporesheni Tokomeza’ na madhara yake kijamii na kisiasa kabla ya utendaji mpya.  Je, jamii imehamasika kusaidiana na mikakati teule? Tuonane wiki ijayo.

By Jamhuri