Vita yanukia

Hatari na wasiwasi uliokuwapo mwaka 2014 kwamba dunia ilikuwa na uwezekano wa kuingia katika Vita Kuu ya III ya Dunia, umerejea na wakati wowote dunia inaweza kuingia vitani.


Pamoja na kwamba Rais wa Marekani, Donald Trump, wakati wa kampeni alisema Marekani haitaingia vitani katika nchi ya kigeni, wiki iliyopita imeingia vitani na kutumia nguvu kubwa.
Hali ya wasiwasi imetanda katika eneo la Mashariki ya Kati baada ya Urusi kuonekana kujiandaa kukabiliana na mashambulizi ya makombora yanayofanywa na majeshi ya Marekani.
Rais Trump wa Marekani alitoa amri ya kushambuliwa kwa mji wa Khan Sheikhoun uliko kaskazini-magharibi mwa Syria, kwa kile alichodai kuwa mji huo unatumiwa kuhifadhi silaha za sumu zilizotumiwa na majeshi ya Syria kuua mamia ya raia, hasa watoto.
Siku ya kwanza ya mashambulizi hayo, Marekani ilirusha makombora 59 yaliyoteketeza baadhi ya silaha na nyumba zinazodaiwa kutumiwa na majeshi ya Syria yanayoungwa mkono na Urusi.
Urusi ambayo imekuwa mshirika mkuu wa Rais Bashar el-Assad wa Syria, imekasirishwa na hatua ya Marekani, na sasa imepeleka meli yake kubwa ya kivita karibu na ‘uwanja wa vita’ kwa kile kinachoelezwa kuwa ni hatari ya kuibuka kwa mapigano kati ya wababe hao wa dunia kijeshi.
Wakati Marekani ikidai kuwa utawala wa Assad ndiyo uliohusika kuwaua watu zaidi ya 80 kwa kutumia silaha za sumu, hadi sasa hakuna upande wowote ulioweza kuthibitisha madai hayo. Hata hivyo, majeshi ya Urusi yanayoshirikiana na Syria yanatajwa kuwa ndiyo yamekuwa yakiushambulia mji huo ulio katika Jimbo la Idlib, na unaotajwa kuwa ngome ya waasi wanaotaka kumpindua Rais Assad.
Mashambulizi mapya yameifanya Urusi ipeleke meli ya kivita yenye makombora ya masafa marefu kama kuonesha nguvu za kijeshi ilizonazo.
Jeshi la anga la Syria lilirejesha huduma zake za safari za anga kwenye ngome yake iliyoshambuliwa na Marekani mwishoni mwa wiki iliyopita.
Makao Makuu ya Jeshi la Marekani, Pentagon, yanachunguza uwezekano wa Urusi kushiriki kwenye mashambulizi ya silaha za sumu yanayotajwa kuwa chanzo cha uamuzi wa Rais Trump kuagiza kuishambulia Syria.
Maofisa wa Marekani wamesema shambulizi la kwanza wiki iliyopita liliteketeza ndegevita 20 katika kambi ya Shayrat. Ndege nyingi kati ya hizo zinatajwa kuwa ni za Urusi.
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa (UN), Nikki Haley, amesema nchi yake inajiandaa ‘kufanya makubwa zaidi’ nchini Syria.
Rais Vladimir Putin wa Urusi amesema mashambulizi ya Marekani ni “kitendo cha uchokozi.”
 Vyombo vya habari vya Urusi vimesema meli ya nchi hiyo yenye makombora imeonekana katika Bahari ya Mediterranean ikiwa njiani kuelekea eneo la ‘kimkakati’ nchini Syria.
Baada ya mashambulizi ya Marekani katika ngome ya jeshi la anga ya Shayrat iliyoko magharibi mwa Syria, Urusi ikaahidi mara moja kuliimarisha jeshi la anga la Syria.
Vyombo vya habari vya Serikali ya Urusi vimesema Mnadhimu Grigorovich, atakuwa kwenye ngome ya majeshi ya nchi hiyo katika mji wa Tartus, Syria. Meli hiyo inatarajiwa kuwapo nchini humo kwa kipindi kisichopungua mwezi mmoja.
Meli hiyo inayotajwa kuwa na makombora na silaha za kisasa kabisa, ilikuwa kwenye mazoezi ya kijeshi katika Bahari Nyeusi (Black Sea).
Shirika la Kujihami la Nchi za Ulaya Magharibi (NATO), limesema hii ni mara ya kwanza, kwa miongo mingi, kwa Urusi kupeleka silaha nyingi na ‘nzito’ katika eneo hilo.
Luteni Jenerali mstaafu wa Jeshi la Marekani, Mark Hertling, amesema kinachofanywa na Urusi ni kutaka kuonesha silaha zake ambazo tangu mwishoni mwa mwaka 2015 zimekuwa zikitumika kwenye mashambulizi ya anga dhidi ya vikosi vya waasi nchini Syria.
Utawala wa Rais Trump bado haujaweka wazi kama mashambulizi ya sasa yanalenga kumng’oa madarakani Rais Assad. Ikulu ya Marekani imekataa kutangaza hatua inayofuata. Mwandishi wa Ikulu, Sean Spicer, amesema Rais Trump hatatangaza “kitakachofuata.”
Ameelezea mashambulizi hayo kwamba ulikuwa uamuzi sahihi, wa haki na sawia.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Rex Tillerson, anasema Urusi imeshindwa kuhakikisha Syria inaondokana na silaha za kemikali.
“Hakika, Urusi imeshindwa wajibu wake katika jambo hili tangu mwaka 2013,” amesema.
 
Nani wanaiunga mkono Marekani?
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Boris Johnson, mwishoni mwa wiki alifuta ziara yake nchini Urusi, akitaka kushughulikia hali ya mambo nchini Syria.
Kwenye taarifa yake, amesema kipaumbele chake ni kuendelea kuwasiliana na Marekani na mataifa mengine kwa ajili ya maandalizi ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa wanachama wa G7 nchini Italia. Lengo la mkutano huo ni kuweka mkakati wa kupata kuungwa mkono na mataifa mengine ili kumaliza mapigano na kutoa fursa ya mazungumzo kwa pande zinazopingana.

Je, Urusi imehusika?
Maofisa wa Serikali ya Marekani wanasema Pentagon inatafuta ushahidi ili kubaini kama kweli Serikali ya Urusi inatambua au ilishiriki kwenye mashambulizi ya silaha za sumu nchini Syria.
Kwenye uchunguzi huo, Marekani inataka kupata ukweli baada ya kuwapo taarifa zinazoeleza kuwa ndege ya Urusi ilirusha makombora katika hospitali ya Khan Sheikhoun, saa tano baada ya mashambulizi ya silaha za sumu kama mbinu ya kufuta ushahidi.
Marekani imesema taarifa za kiitelejensia zinaonesha kuwa ndege ya Urusi isiyo na rubani iliruka juu ya hospitali walimokuwa wakitibiwa majeruhi.
Msemaji wa Ikulu ya Urusi (Kremlin), Dmitry Peskov, amekanusha madai hayo.
Mgogoro wa Syria
Kwa miaka sita sasa, mgogoro wa Syria umekuwa kaa la moto. Hapa chini kuna uhusika wa nchi mbalimbali kwenye mgogoro huu.

Marekani
Tangu mwaka 2014, Marekani imekuwa ikisaka nguvu za kimataifa za kufanya mashambulizi ya anga ikilenga kundi la Dola ya Kiislamu (IS) nchini Syria. Chini ya utawala wa Rais Barack Obama, Marekani imeendesha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya IS nchini humo na Iraki. Rais Trump ameendelea na mpango huo, lakini mashambulizi ya wiki iliyopita yalilenga moja kwa moja kumdhoofisha Rais Assad.
Uongozi wa Obama mara zote ulisisitiza kuondoka madarakani kwa Rais Assad. Lakini uongozi wa Trump unasema hatima ya rais huyo iko mikononi mwa wananchi wa Syria wenyewe.

Urusi
Rais Putin wa Urusi anasema mashambulizi ya Marekani nchini Syria ni kitendo cha uchokozi kinachovunja sheria za kimataifa. Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, amenukuliwa akisema mashambulizi hayo yanafifisha uhusiano kati ya Urusi na Marekani.
“Ushirikiano kati ya Urusi na Marekani kijeshi unaweza kufutwa baada ya mashambulizi haya ya Marekani,” amesema Viktor Ozerov, ambaye ni kiongozi wa Kamati ya Ulinzi.
Amesema Urusi inahitaji kuwapo kwa kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la UN kujadili hatua ya Marekani ambacho amekiita ni cha uchokozi dhidi ya mwanachama wa UN.
Urusi ndiye mshirika mkuu wa Syria, na imekuwa ikimsaidia kijeshi Rais Assad. Urusi ina maslahi ya kiuchumi na kijeshi nchini humo kama vile ngome yake ya kijeshi ya Tartus. Kwa miaka mingi imekuwa ikiikingia kifua Syria dhidi ya maazimio mbalimbali ya Baraza la Usalama la UN.
Rais Putin ameshangaza ulimwengu kuwa vyovyote iwavyo atahakikisha anamsaidia Rais Assad kuendelea kuwa madarakani dhidi ya tishio la waasi wanaotaka kumng’oa.

Saudi Arabia
Saud Arabia yenyewe imetangaza kuiunga mkono Marekani kwa asilimia 100 kwa hatua inazochukua dhidi ya utawala wa Rais Assad.
Saudi Arabia ni miongoni mwa nchi zinazounga mkono makundi yanayopambana na waasi wanaoipinga serikali pamoja na kundi la IS. Ni miongni pia mwa nchi zinazoshirikiana na Marekani kwenye mashambulizi ya anga nchini Syria.

Jordan
Serikali ya Jordan kupitia msemaji wake, Mohammad Momani, inasema taifa hilo linaunga mkono hatua ya Marekani kwa kile inachosema inalenga kuwalinda raia wasio na hatia wanaouawa na serikali ya Syria.
Jordan ni miongoni mwa washirika wanaopigana dhidi ya IS na imepokea maelfu ya wakimbizi kutoka Syria.

Uturuki
“Tunakaribisha operesheni ya Marekani nchini Syria,” hii ni kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mevlut Cavusogulu.
Anasema nchi yake inayakaribisha mashambulizi hayo kwa kuwa ni hatua chanya dhidi ya utawala wa Assad.
Ibrahim Kalin, msemaji wa Rais wa Uturuki, anasema: “Kuteketezwa kwa ngome ya kijeshi ya Shayrat, kunaashiria hatua muhimu dhidi ya mashambulizi ya silaha za kemikali dhidi ya raia.”
Ametoa mwito wa kutengwa kwa eneo la anga lisiloruhusiwa kuruka ndege, na maeneo mengine salama kwa ajili ya kuruka ndege.
Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, anamtaja Rais Assad kama “muuaji “. Uturuki kwa muda mrefu imeruhusu ardhi yake itumiwe na wapinzani wa Assad kwa ajili ya kufanya mashambulizi dhidi ya utawala wake.

Japan
Waziri Mkuu wa Japan,  Shinzo Abe, amewaambia waandishi wa habari kuwa nchi yake inaunga mkono hatua ya Marekani nchini Syria.
Uingereza, Hispania, Ujerumani, Ufaransa na Italia zote zinaunga mkono hatua ya Marekani kuishambulia Syria.

Iran
Kwa ujumla Iran imekuwa mpinzani mkuu wa matumizi ya nguvu za kijeshi dhidi ya utawala wa Rais Assad. Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Bahram Qasemi, anasema: “Tunalaani matumizi ya nguvu za kijeshi katika ngome ya kijeshi ya Al Shayrat nchini Syria yanayofanywa na Marekani… mashambulizi haya yanalenga kuwapa nguvu magaidi ambao tayari walishaanza kuwa dhaifu.”
Iran ni miongoni mwa washirika wakuu wa Urusi katika kuhakikisha Rais Assad anaendelea kuwa madarakani.
Iran, ambayo raia wake wengi ni wa madhehebu ya Shiite, haitaki kuona waumini wa madhehebu ya Sunni ambao ndiyo wengi nchini Syria, wakitwaa madaraka. Madhehebu hayo yanaungwa mkono na Qatar na Saudi Arabia. Iran inapendekeza mgogoro wa Syria umalizwe kwa njia za kisiasa/mazungumzo.

China
Waziri wa Mambo ya Nje wa China amesema nchi hiyo haiungi mkono hatua zozote za kutatua migogoro kwa njia za kijeshi.
“China mara zote imekuwa ikipinga matumizi ya nguvu kwa masuala ya kimataifa na tumekuwa tukishauri migogoro imalizwe kwa njia ya mazungumzo, mara zote tumesema mgogoro wa Syria utamalizwa kisiasa.”
Makundi ya aina hii yalitokea wakati wa Vita Kuu ya I na ya II ya Dunia, yakifahamika kama ‘Triple Alliance’ na ‘Triple Entente’, suala lililoifanya dunia kushuhudia uharibifu mkubwa wa mali na maisha ya watu na hilo sasa kupitia Syria linaweza kutokea tena.