Vituko vya DC Geita

Na Victor Bariety, Geita

Sehemu ya kwanza ya makala hii ilielezea vituko vinavyofanywa na Mkuu wa Wilaya ya Geita, Omari Manzie Mangochie, vikiwamo vya kuzuia ujenzi wa mnara wa simu za mkononi na kutangaza vita na waandishi wa habari. Sasa endelea na sehemu hii ya pili.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Omari Manzie Mangochie ambaye anatajwa kama kiongozi anayezalisha migogoro na kukwamisha shughuli za maendeleo wilayani hapa. Anatuhumiwa pia kumng’oa Mwenyekiti wa Chama chake cha Mapinduzi (CCM) wa kijiji cha Mnyara, hivyo kuwapatia wapinzani mwanya wa uongozi.

Katika tuki hilo la aina yake, Mangochie baada ya kumvua uongozi Mwenyekiti wa Kijiji cha Mnyara, Makoye Roboyanke, aliitisha uchaguzi mdogo na kuwaamuru wananchi kupiga kula za wazi mgongoni mwa wagombea kinyume cha taratibu za uchaguzi.

Kitendo hicho kilizua tafrani kubwa kwani pamoja na wananchi kukubali matakwa ya Mkuu huyo wa wilaya kwa kuwachagua viongozi wao nyuma ya migongo, CCM kilichokuwa kimeweka mizizi eneo hilo kilibwagwa na kusababisha msimamizi wa uchaguzi kukimbia na matokeo ili kujinusuru na kipigo kutoka kwa wananchi hao.

Inadaiwa kuwa uamuzi huo wa Mangochie wa kumvua uongozi kada huyo wa CCM bila kufuata utaratibu umesababisha wananchi wa eneo hilo kukihama chama hicho tawala na kujiunga na vyama vya upinzani ambavyo hapo awali havikuwa na nguvu kwenye kijiji hicho ambapo wameiomba Serikali kuingilia kati mgogoro huo.

Akizungumza na JAMHURI kijijini hapo hivi karibuni, mwenyekiti huyo wa kijiji alisema uamuzi huo wa Mangochie umemdhalilisha na umeonesha ni jinsi gani asivyoheshimu vikao halali vya CCM.

Chanzo cha DC kumvua madaraka

Roboyanke aliyekuwa pia mwenyekiti wa kitongoji cha Makurugusi kilichopo kijijini hapo, alidai kuwa chanzo cha DC kumng’oa ni ajali ya gari la tajiri, Lazaro Msenya, lililoondoa uhai wa mwananchi wake.

Alifafanua kuwa mwaka 2013 Msenya ambaye ni rafiki mkubwa wa Mkuu huyo wa wilaya alimgonga na gari lake mwanamke aliyetajwa kwa jina la Maria, akafariki dunia.

Mfanyabiashara huyo ambaye pia ni kada wa CCM katika kata ya Nkome wilayani, alipomgonga mwanamke huyo na gari hilo lililokuwa limebeba mbao, saa 2:30 za usiku hakusimama eneo la tukio, badala yake alikimbia.

Kufuatia hali hiyo, baada ya askari polisi kufika eneo la tukio baadhi ya wananchi walionekana kutaka kuficha ukweli kwa kuhofia ‘mguvu’ ya tajiri huyo isipokuwa Roboyanke ambaye alieleza ukweli kwamba marehemu aligongwa na tajiri huyo, ndipo uhasama ukaanzia hapo. Mfanyabiashara huyo alimtumia Mangochie kujinasua kwenye kesi hiyo na kuandaa mkakati wa kumng’oa ili kumdhoofisha asifuatilie mwenendo wa kesi hiyo.

“Baada ya polisi kufika eneo la tukio wananchi walihofia kumtaja mfanyabiashara huyo kwamba ndiye amemgonga mwanamke huyo na kufa, lakini mimi kwa kuwa huwa napenda haki siku zote niliwaeleza ukweli polisi hao ambao baadaye walifanikiwa kumkamata na kumfikisha kituoni na uhasama ukaanzia hapo. Lakini hiyo kesi iliyeyuka, ndipo akamtumia DC kuning’oa ili kudhoofisha harakati zangu,” amesema Roboyanke.

Alipoulizwa na JAMHURI, Msenya alikiri kulitambua tukio hilo huku akijitetea kuwa wakati mwanamke huyo akigongwa, gari hilo lilikuwa na dereva na kwamba kesi hiyo iliishia Kituo Kikuu cha Polisi cha Wilaya ya Geita baada ya kuonekana hana hatia.

“Unajua hilo gari lilikuwa na dereva na baada ya tukio hilo gari lilikamatwa na kufikishwa polisi… walikuja wapelelezi kutoka wilayani wakachunguza na kunikuta sina hatia,” amesema Msenya huku akimtaka mwandishi wa habari hizi kuonana naye ana kwa ana ili wayazungumzie vizuri suala hilo.

Itaendelea toleo lijalo