Ni wazi kwamba nafasi inayoshikiliwa na Uganda na Rwanda katika roho ya uchumi wa Marekani na Uingereza ni kubwa kuliko nchi yoyote ile katika eneo la Maziwa Makuu kwa sasa.

Hakika Marekani na Uingereza wamelipa gharama kubwa kutengeneza miundo ya kiserikali, nguvu za kijeshi na saikolojia za kisiasa zinazoongoza nchi hizo miaka ya karibuni.

Watu walijiuliza maswali mengi kunako miaka ya tisini juu ya nguvu za Museveni na baadaye kasi ya RPF kuitwaa Rwanda, nchi ambayo ilikuwa imeanza kuimarika kama zilivyokuwa nchi nyingine barani Afrika. Hasa nchi ambazo zilikuwa zimeishi kwa amani toka uhuru mpaka miaka hiyo.

Mwanzoni mwa miaka ya tisini Rwanda ilikuwa na fedha yenye thamani kubwa. Ilikuwa pia na msaada mkubwa wa kijeshi kutoka Ufaransa. Raia wake walikuwa na kipato kizuri cha kutosha. Ilikuwa thabiti.

Matatizo yaliyokuwapo Rwanda miaka ya tisini yaliakisi matatizo yaliyokuwapo kwingineko barani Afrika kama vile vita za wenyewe kwa wenyewe, uongozi mbovu na uamuzi usiyo na tija, ufisadi wa wachache, upendeleo wa kikabila (Wahutu), undugu (nepotism) na zaidi suala la wakimbizi.

Wakimbizi wa Rwanda miaka ya ‘tisini mwanzoni’ walikuwa ni Watutsi waliokuwa wameikimbia nchi baada ya mapinduzi mwaka 1959 yaliyoiondoa dola ya mfalume Kigeri V muda mfupi kabla ya uhuru. Rwanda haikutofautiana na nchi nyingine nyingi barani Afrika.

Ukiilinganisha Rwanda ya sasa ya Kagame ambayo wapinzani wake wanaviziwa na kuuawa hata wakiwa nje ya nchi! Rwanda ambayo wakati wa uchaguzi raia wanapotea kimya kimya na baadhi kuokotwa wakiwa mizoga!

Rwanda ambayo demokrasia na taasisi za umma hazifanyi kazi kwa uhuru isipokuwa kwa maelekezo ya wanasiasa! Rwanda hiyo hiyo ukiilinganisha na ya Habyarimana ya mwaka tisini utagundua kuwa Rwanda ya Kagame inacheza mchezo hatarishi.

Inawezekana wanasiasa kama Kagame, madame Jeanette Kagame, James Kabarebe, Louise Mushikiwabo na tabaka la juu la watawala Watutsi wa Rwanda hawaoni kuwa wao wamerudufu matatizo waliyoyakuta. Ni mchezo mkongwe barani Afrika, hivyo huchukuliwa kama utamaduni fulani.

Rwanda ya mwaka tisini ilikuwa kwa kiwango kikubwa sawa na ya sasa. Kwa mfano, wachache miongoni mwa Wahutu walitawala hasa wale waliotokea mikoa ya Ruhengeri na Gisenyi, wakijiita “akazu”. Leo hii Watutsi wa Rwanda ambao ndio wachache wanakula na kunywa vizuri kuliko Wahutu ambao ndio wengi!

Inachekesha ukichunguza kwa makini jinsi Rwanda inavyoshughulikia changamoto zake za kihistoria. Inazishughulikia kikabila kama kawaida ya enzi na enzi zao.

Katika hao Watutsi wanaotawala bado kuna vikumbo; wapo wanaojiita Watutsi waliokuwa wakimbizi Uganda na kwingineko, lakini pia wapo wale waliokuwamo nchini na hawakupata kukimbia. Cha kusikitisha ni kwamba wale waliokuwamo ndani kabla ya 1990 wanalalama kuwa wametengwa na Watutsi wenzao katika kula keki ya taifa.

Kuna kasi kubwa ya Kagame kuchukiwa na Watutsi wenzake ndani na nje ya nchi. Fuatilia ‘facebook’ ukurasa wa mwanasiasa “Theogene Rudasingwa” utaona hayo. Ni kama ‘mlokole’ Rudasingwa amekuwa nguzo ya mamilioni ya Watutsi wanaokwazwa na dola ya RPF. Wengi wamekatishwa tamaa na mfumo wa siasa anaoufanya Kagame.

Hili kundi linamwona Rudasingwa na chama chake, Rwanda National Congress (RNC), kama ‘masia’ wao ajaye na wana hasira sana na Kagame. Mungu saidia isitokee vita!

Si hilo tu, yapo mengi ya kuonesha kuwa kijamii na kimfumo wa siasa Rwanda imebadilika kidogo mno toka ilivyokuwa miaka ya tisini. Kwa mfano, wakati wa Habyarimana Ufaransa na Ubeligiji ndio waliokuwa mabwana ‘ukoloni mamboleo’ wa Rwanda wakifadhili jeshi na kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa Rwanda. Rwanda ilikuwa ikitumia Kifaransa, hivyo kuwa mwanachama wa ‘Francophone’.

Toka miaka ya tisini RPF na Jeshi la Rwanda wamebadilisha mabwana wa ukoloni mamboleo. Marekani na Uingereza ndio wanaolifundisha Jeshi la Rwanda, wanalifadhili na hata mfumo wa jeshi hilo umekuwa wa Kimarekani zaidi. Kama haitoshi, Rwanda imeminywa ikatoka ‘Francophone’ na kuwa ‘Anglophone’.

Rwanda kwa kifupi imesafiri toka Paris kwenda Washngton DC. Nadhani hapa unauona unafiki wa hayo mataifa. Inawezekana ule msaada wa kijeshi wa mwaka 1994 kuiteka Rwanda ulikuwa ni uwekezaji fulani ambao Marekani ilikuwa inaufanya. Tusonge mbele.

Tatizo la kitaalamu lililojitokeza kutokana na uamuzi huo wa kubadili lugha na mtazamo wa ufuasi kwa wana Magharibi ni kubwa. Linamaanisha kuwa Wahutu wengi wamekuwa ‘useless’ katika kulikuza na kulielekeza taifa kwa sababu walikuwa na mtaala wa Kifaransa. Walisoma wakiwa wana dola, lakini ulikuwa ni mfumo wa Kifaransa, hivyo mabadiliko haya yamewatenga!

Wapo wataalamu wanaodhani kuwa kubadilishwa kwa mfumo huo kulikuwa ni hesabu ya makusudi kuhakikisha kuwa Watutsi waliokuwa wamekimbilia Uganda na Tanzania ambako Kiingereza ndiyo lugha ya taaluma wanakuwa na uwezo wa kiushindani, hivyo kupata nafasi katika Rwanda tunayoiona leo.

Hili limewafanya wawe bora kuliko wengineo ambao ni ‘Francophone’. Madhara ya hili tunatarajia yatakuwa makubwa kiuchumi na kijamii.

Rwanda ya miaka ya kabla ya tisini ilikuwa na demokrasia ya aina yake! Habyarimana amepata kushinda chaguzi kwa takwimu kama: 98.99% ya kura zilizopigwa Disemba 24, 1978, 99.97% ya kura zilizopigwa Disemba 19, 1983 na 99.98% asilimia ya kura zilizopigwa Disemba 19, 1988. Takwimu hizi hutia shaka.

Vivyo hivyo, Kagame amepata kushinda kwa takwimu kubwa. Takwimu ambazo huashiria udanganyifu kwa wataalamu wengi wa demokrasia: 95.1% ya kura zilizopigwa Agosti 25, 2003 na 93.08% ya kura zilizopigwa Agosti 9, 2010. Kuna siri zinazofanana katika chaguzi za Habyarimana na za Kagame.

Moja kati ya vikwazo vya kisiasa barani Afrika toka miaka ya sitini, ni pamoja na tatizo la viongozi kutawala kwa kushirikiana na maswahiba badala ya kuzifuata sheria na katiba. Hili lilimkumba Habyarimana wa Rwanda ambako wakati wa miaka ya 1990 hao maswahiba wake wanaojiita ‘akazu’ walikuwa na nguvu sana.

Mke wa Habyarimana, Agathe Habyarimana, akawa kama ‘malkia’ na akatoa amri na kuheshimiwa si na mawaziri tu bali pia makamanda wa jeshi, wabunge na viongozi wengine.

Hebu tembelea hiyo ‘facebook’ ya Rudasingwa niliyokutajia ustaajabu ya Musa! Hilo hilo la Agathe Habyarimana limejirudia Rwanda. Anayelifanya sasa ni mke wa rais aliyepo – Kagame, Jeannette Kagame.

Theogene Rudasingwa alikuwa mkuu wa watumishi wa Ikulu, “Urugwiro village” Rwanda kwa cheo cha “presidential chief of staff” na analalama kuwa Madame Jeannette Kagame ndiye mtu mwenye nguvu kuliko wote baada ya mume wake. Anatukuka kwa kuheshimiwa, ‘madame’.

Huyo mama anaogopwa, anaamuru na akikushika mkono basi we umeula. ‘Wapo watu sasa ni mawaziri, mabalozi au maofisa wakubwa Rwanda ambao ni matokeo ya kujuana au kuwa na undugu na Jeannette’.

Rudasingwa, ambaye pia ni Mtutsi, amemuorodhesha Jeannette katika wale anaowaita wafanya uamuzi na wauaji wa wapinzani Rwanda. Soma pale kwenye ‘wall’ yake uhakikishe mwenyewe au mwandikie huyo mheshimiwa atakujibu vizuri sana. Haongei kwa kuhisia au maoni, anaongea yaliyomkuta kwa cheo chake na kazi zake akiwa kiongozi mkubwa serikalini na katika chama tawala cha RPF.

Naomba nikumbushe kwamba katika sehemu ya pili ya makala hii nilieleza kuwa ili kujua kwanini mwaka 1994 walipa kodi wa Marekani walikuwa wamepoteza fedha nyingi kuifadhili RPF, lazima kwanza ujue Kagame ni nani. Lazima uuangalie udhaifu wake ndipo ujue kuwa aliteuliwa ili aonewe kwa kutumiwa awaonee wengine!

Aliandaliwa ili awekwe kwenye mtego ambao kujitoa kutamuweka pagumu. Elimu na maarifa aliyonayo kitaaluma bwana Kagame ni madogo! Ana elimu ndogo, ujeshi mwingi! Kwa hili Wamarekani walimchagua wakijua lengo lao. Unafiki wa Marekani na Uingereza utauona kupitia kuichambua haiba ya Kagame, ambayo kwa kiasi kikubwa imejengwa na hofu na pia jazba.

Nadhani katika makala hii utakuwa umeona kabisa kuwa hakuna tofauti kati ya alivyotawala Habyarimana na anavyotawala Kagame leo hii. Ni mwendo ule ule wa kuwagawa raia na kuwafanya baadhi waishi maisha yanayotengeneza chuki kwa wenzao. ‘Wahutu sasa wamenywea, Watutsi tunakula’, ndiyo falsafa.

Je, kwanini Marekani ‘ilimtaka’ Kagame tu na mpaka sasa inaendelea kumbeba? Je, gharama za miaka minne kupigana msituni RPF toka mwaka 1990 mpaka 1994 zimefidiwa vipi? Kumbuka Marekani ni mabepari! Hawawezi kutoa bure. Kamwe hawawezi! Hata wakitoa misaada ya ki-utu daima wana lao jambo wamelificha.

Naamu. Hakika waandishi wa ki-Magharibi wamelijibu hilo kwa ufasaha. Haijalishi kuwa unamsoma Gerald Prunier, Bridgette Kasuka, Hassan Suror, Asad Ismi au wengi wengine; wote wanatoa jibu moja.

Jibu hilo ni kwamba wakati Museveni akimuandaa Kagame na wakati RPF ikitwaa madaraka Rwanda, wote labda hawakujua kuwa lengo lilikuwa ni wao “kuwa vibaraka” wa kuikosesha amani Zaire!

Lakini pia wasomi wengine wanaizungumzia Sudan Kusini kama sehemu ya picha kubwa iliyokuwa ikiandaliwa. Wanaonesha kuwa Marekani na Uingereza kumdhamini Museveni na muda mfupi baada ya hapo, yaani mwaka 1986 mpaka 1990 kuanzisha vugu vugu Rwanda lilikuwa jambo lenye u-wili kimatokeo – it featured a double impact.

La kwanza, Uganda ilipewa silaha na fedha nyingi kuimarisha vurugu Kusini mwa Sudani. Huko ndiko kwenye asilimia 60 ya mafuta ambayo Khartoum ilikuwa inajivunia. Mafuta ambayo Marekani na washirika wake waliyatamani mno.

Sudan ilikuwa imebana mafuta yake ikashirikiana na OPEC kujipangia bei ipendavyo, jambo ambalo liliwakasirisha ‘wakubwa’ pale Washington DC. Hivyo, kukawa na mchafuko wa kisiasa Sudan miaka yote hii toka Museveni ashike usukani wa Uganda. Lengo limetimia, Sudan imemegwa na taifa changa, dhaifu na tegemezi, lakini lenye rasilimali kubwa ya mafuta limezaliwa. Linaitwa Sudan Kusini!

La pili, miaka miwili baada ya RPF kuitwaa Rwanda, yaani 1996 akavamiwa Mobutu Sese Seko, ‘kibaraka aliyemaliza zama zake’ wa Zaire na majeshi ya Rwanda na Uganda – wakijiita Banyamulenge – Watutsi wa Kongo.

Mbabe huyo aliondolewa madarakani kwa aibu kubwa huku akiachwa kwenda kufa kwa mateso jijini Rabat, nchini Morocco. Amezikwa katika makaburi ya Wakristo ambayo kwa Morocco yenye Uislamu mkubwa ni makaburi ya watu wa daraja la chini na wasiostahili heshima.

Historia ya kusikitisha ya Mobutu inaonesha kuwa alikufa kwa kansa ya kibofu ‘prostate cancer’ tena akiwa hana hata pa kwenda maana ‘wakubwa’ wa Ulaya walishapanga akitua tu kwao wanamfikisha mahakamani kwa ubadhirifu na kupora utajiri wa nchi yake! Hivyo, mabilioni ya fedha aliyokuwa ameweka kwenye benki za Ulaya yakaendelea kutumiwa na mabepari huku yeye akibaki na ‘labda’!

Zaidi ya yote kile tunajifunza kuwa mfumo wa ‘ukoloni mamboleo’ ni mfumo katili ambao humchukua kibaraka, humuandaa, humhadaa, humuwezesha na kumpa hatamu wakati akitumiwa.

Katika kuficha aibu na kuondoa ushahidi, mabwana hao wa Magharibi huishia kumsaliti na kumdhalilisha kibaraka. Ni kama vile ambavyo baraza la wanasheria ‘sanhaidren’ la Kiyahudi lilivyomdhihaki na kumdhalilisha msaliti ‘Yuda’ mara walipomtwaa ‘Yesu’ huku wakimwacha Yuda Iscariot na vipande thelathini vya fedha. Vipande ambavyo visingemsaidia tena! Yuda alibaki na ‘labda’. Wamefanyiwa hivyo viongozi wengi wa Kiafrika.

Itaendelea

[email protected]

By Jamhuri