NA CLEMENT MAGEMBE

DAR ES SALAAM

Sakata la kuwaondoa kazini watumishi waliokuwa na vyeti `feki’ linadaiwa kuitesa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) jijini Dar es Salaam, kwa wafanyakazi waliobaki kuzidiwa na utoaji huduma kwa wahitaji hususani wagonjwa.

Taarifa zimedai kuwa kitengo kilicholemewa zaidi ni watumishi wa chumba cha maiti (mochwari) ambao wako wawili, baada ya wenzao watatu kuondolewa kazini kutokana na kuwa na vyeti `feki’ vya kidato cha nne.

Vyanzo vyetu kutoka ORCI vimeeleza kuwa kutokana na upungufu huo, inawalazimu wafanyakazi wa taasisi hiyo kufanya kazi kwa muda mrefu bila kupumzika na hivyo kujikuta katika  mazingira yanayohatarisha afya zao.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, kitengo kingine kilichoelemewa katika utoaji wa huduma ni tiba ya mionzi ambapo idadi ya wahudumu haikidhi wingi wa wagonjwa wanaofika kutibiwa.

“Tumelazimika kuwapa wagonjwa ratiba ya siku za kuanza matibabu, kwa kuwa wagonjwa ni wengi mno kuliko wahudumu wa afya,” amesema mmoja wa wafanyakazi wa taasisi hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dk. Julius Mwaiselage, amekana kuhusu taasisi hiyo kuzidiwa katika utoaji wa huduma baada ya waliokuwa wafanyakazi wake kuondolewa katika kashfa ya vyeti ‘feki’.

“Ni kweli kuna upungufu wa watumishi lakini siyo kwa kiwango cha kusababisha kuelemewa ama kushindwa kutoa huduma,” amesema Dk. Mwaiselage.

Dk. Mwaiselage ORCI hivi sasa ina watumishi 246 kati ya 300 wanaohitajika hivyo kusababisha mahitaji ya watumishi 54.

Kwa mujibu wa Dk. Mwaiselage, watumishi walioondolewa katika taasisi hiyo kutokana na kashfa ya vyeti feki ni 15 na kwamba watumishi 13 wameshaajiriwa kuziba nafasi hizo.

Pia Dk. Mwaiselage amesema ORCI imepata bajeti ya kuajiri watumishi 42 katika mwaka huu wa fedha, hivyo wanatarajia kuondokana na upungufu huo.

mwisho

1601 Total Views 9 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!