“….Lakini niwaombe viongozi pia na Watanzania wote. Ninajua mmetupima sisi katika siku 100. Inawezekana mnatuonea pia. Kwamba siku mia moja za Magufuli, siku mia moja za Waziri Mkuu, Makamu wa Rais, siku mia moja za Mawaziri na kadhalika. Mmesahau nyinyi kujipima siku 100 mmefanya nini kwa ajili ya Tanzania?”

Si maneno yangu. Ni maneno yaliyotamkwa Rais John Pombe Magufuli, alipozungumza na Wazee wa Dar es Salaam wiki mbili zilizopita kwenye ukumbi wa Diamond Jublee alìpokaribishwa na kupongezwa na serikali yake kwa kazi nzuri aliyoifanya ndani ya siku 100 tangu waingie madarakani, Novemba 5, 2015.

Katika mkutano ule Rais Magufuli alipokea pongezi na kongole kutoka kwa wazee wale kwa furaha na upendo. Na yeye aliwaomba na kuwasisitiza pamoja na vijana wao wenye uwezo wa kufanya kazi  wafanye kazi, wajipime na wajitambue wao ni watu muhimu mno katika kujenga na kuleta maendeleo ya nchi na ya mtu mmoja mmoja.

Kinywa chake hakikujaa mate, wala moyo wake haukujenga hofu kutamka maneno yenye ladha ya asali na shubiri kwa waliomkaribisha na kumsikiliza. Alifanya hivyo kwa sababu amejaa hekima, akili timamu na tambuzi zinazokerwa na maovu na umasikini wa Watanzania ndani ya utajiri wa nchi yao.

Kutokana na msimamo wake wa ujasiri, ukweli, upendo kwa watu na imani kwa  Mwenyezi Mungu alirudia mara kwa mara kaulimbiu yake “Hapa Kazi Tu” na “Asiyefanyakazi Asile.” Mbiu hiyo imewavaa  viongozi wote,  wanataaluma wote, wakulima, wafanyakazi na wafanyabiashara wote nchini. Hakusita, hakupendelea, wala hakuhemewa kueleza hila na udanganyifu unaofanywa na baadhi ya Watanzania wenzetu wanapokabidhiwa madaraka, kazi za ujenzi wa miundombinu  ya uchumi na huduma kwa wananchi wao hufanya inda na choyo. Kutokana na vitendo hivyo vyenye udhalimu na uhujumu wametufikisha Watanzania kwenye uga wa umasikini.

Rais Magufuli alisema kuwa alihuzunika kuona baadhi ya majengo ya serikali hayajakamilishwa kujengwa kwa zaidi ya miaka 20 sasa,  lau kama vipo vijisababu vya ujanja ujanja vyenye asili ya fedha. Hata hivyo, amewaahidi wazee kuwa ataondoa kero hizo na vijisababu vidogo vidogo miundombinu ikamilike na kutumika.

Hotuba ya Rais imenikosha mno kama hotuba ile aliyoitoa Siku ya Sheria Duniani kwa Wanasheria wetu wa Tanzania alipowapa ukweli  kuhusu utendaji kazi wao. Baadhi ya kai zao katika Mahakama  zinafanywa kifigisufigisu ima haki kuchelewa kutolewa au kupotea. Amewataka Majaji, Mahakimu na Mawakili wajirekebishe na waache tabia ya kipurukushani (kijibaraguza). Aliwapa fedha shilingi bilioni  12.5 walizohitaji kuondoa matatizo yao na aliwaahidi katika bajeti ijayo atawajaza mapesa waweze kufanya kazi zao kwa raha na amani.

Katika hotuba ile kwa Wazee wa Dar es Salaam, Rais Magufuli pia alivipongeza na kuvisifu vyombo vya habari kwa asilimia kubwa kwa kazi nzuri vinayofanya na uchunguzi wa mambo maovu yanayofanywa na watumishi wa umma. Aidha alilisifu na kulipongeza gazeti la JAMHURI kwa uchunguzi wa kugundua kufungia mita za kupimia mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam.

Hata hivyo Rais, alisikitika baadhi ya vyombo vya habari havina uzalendo na hupindisha taaluma zao wanapohabarisha mambo yenye dalili ya uvunjifu wa usalama na amani. Haelewi wanafanya hivyo kwa faida ya nani na wao watakuwa wapi usalama utapokuwa mashakani.

Maelezo ya Rais ni ya kweli. Sisi waandishi wa habari tunalijua hilo na baadhi ya Waandishi na Watangazaji wanakubali kuyumbishwa na wanasiasa, wapenda madaraka na wavunjaji wa sheria za nchi. Baadhi ya Wahariri huwa na kinyongo wanapoona chombo fulani kimesifiwa huleta dharau na kubeza.Ni dalili ya kukosa upendo miongoni mwetu.

Hapa kwenye vyombo vya habari yapo ya kuzungumza. Waandishi hasa Wahariri ndiyo tuliokuwa mstari wa mbele kunadi na kuzungumzia siku 100 za Magufuli amefanya nini kwa Tanzania tangu aingie madarakani. Bila ya sisi kujiuliza katika siku hizo tumefanya nini kwa nchi yetu.

Katika siku hizo wapo wahariri waliosifu na wapo waliokejeli na kubeza eti yaliyofanywa na Rais Magufuli na serikali yake  ni yale yale tu. Tulijifanya kama ndege kasuku kukuza na kueneza kauli za viongozi uchwara na wapinga mafanikio ya serikali. Sijui tulikuwa na maana gani hadi leo baadhi yao bado wamo katika mkakati huo.

Ni kweli waandishi tunastahili heko kufichua na kutaja majipu yalipo na kutangaza jinsi yanavyotumbuliwa. Lakini siyo kubeza kasi ya utumbuaji majipu kwani kufanya hivyo ni kufanya songosongo juu ya habari tuzitoazo au kuzitangaza. Je, katika mazingira kama hayo hatustahili kuwa majipu na kutumbuliwa?

Waandishi na Wahariri wa magazeti mnanielewa. Watangazaji na Wasimamizi wa vipindi vya redio na runinga mnanifahamu vyema  ninayosema. Vipi tushindwe kujiuliza ndani ya siku 100 tumefanya nini kwa ajili ya Tanzania?

Nakiri hadharani baadhi ya ripoti, taarifa, makala na vipindi vyetu vipo vyeupe. Tunajua, lakini tunachelea kutumbua kwa sababu  ya kuhofu uchungu, maumivu na lawama. Kuleana huko ndiko kunakosababisha  kushindwa kujipima na kujitambua. Viongozi tupo, wamiliki wa vyombo  wapo, wasimamizi na wadau wapo. Lipi linatusibu  hata kushindwa kutumbua majipu?

Nashauri. Kwa vile siku mia moja za Magufuli hatukujipima, basi Baraza la Habari Tanzania (MCT), Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT) na Jukwaa la Wahariri Tanzania ( TEF) kutaneni mzungumze na mpange mipango ya kueleweka ya kujipima na kujitambua, vyombo vya habari tufanye nini katika siku 100 zijazo.

Huenda ndani ya mazungumzo hayo yatahusu pia viwango vya elimu na taaluma, malipo ya posho za kazi na safari na taratibu za ajira , uwezo na uzoefu wa kazi na kadhalika, hayo si mambo mabaya ni mazuri kwetu, kwani ndiyo tunajipima na kujitambua  kwa aji ya Tanzania. Tafakari.

1582 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!