Wa-Bahá’í ulimwenguni kote wanasherehekea miaka 200 ya kuzaliwa kwa Bab – Mtume Mtangulizi wa dini ya Bahá’í.

Taarifa ya Baraza la Kiroho la Mahali la Bahá’í imesema sherehe za kilele zitakuwa Oktoba 29, mwaka huu.

‘Bab’, wadhifa ambao maana yake ni ‘Lango’ au ‘Mlango’ katika lugha ya Kiarabu, alizaliwa katika Jiji la Shiraz, Uajemi, mwaka 1819 A.D. Yeye alitoka kwenye ukoo uliokuwa maarufu kwa uungwana wake. Mada kuu ya kazi yake kubwa, Kitabu cha Bayan, ilikuwa ujio tarajiwa wa Mjumbe wa Pili kutoka kwa Mungu, yule ambaye angekuwa mkubwa sana zaidi ya Bab, na ambaye dhima yake ingekuwa ya kuleta zama za amani na haki kama ilivyoahidiwa katika Uyahudi, Ukristo, Uislamu na dini nyingine zote za ulimwengu.

Ujio wa Bab unaashiria mwisho wa ‘Duru la Utume’ la historia ya kidini, na kukaribisha ‘Duru la Ukamilisho’.

Bab, ambaye mafundisho yake yaliwavutia makumi ya maelfu ya wafuasi, aliteswa na kufungwa kwa miaka sita baada ya tangazo lake la ujumbe mpya kutoka kwa Mungu. Hatimaye aliuawa mwaka 1850 katika uwanja wa umma mjini Tabriz, Iran, kwa amri ya serikali.

Baadaye sana, mabaki yake yalisetiriwa katika Mlima Karmel mjini Haifa, Israel, na kaburi takatifu lake sasa ni mahali pa kuhiji kwa Wa-Bahá’í ulimwenguni kote.

Miaka 19 baada ya tangazo la Bab, mwaka 1863, mmoja wa wafuasi wa Bab, mwenye wadhifa wa Baha‘u’llah, Utukufu wa Mungu, alitangaza kuwa yeye alikuwa yule Mwahidiwa aliyetabiriwa na Bab.

Imani ya Bahá’í ni dini inayojitegemea, inayomwamini Mungu mmoja. Inakubali chimbuko tukufu na kusudi moja la dini zote kuu za ulimwengu, na hufundisha kuwa Mungu amefunua ujumbe mpya katika siku hii kwa ajili ya kustawisha umoja wa jamii ya wanadamu. Ni dini ya pili kuenea kijiografia ulimwenguni kote, ikiwa na wafuasi zaidi ya milioni 7 wanaoishi katika maeneo zaidi ya 118,000 katika zaidi ya nchi na majimbo muhimu zaidi ya 230.

Takriban makabila, mbari na vikundi vya wenyeji 2,112 vinawakilishwa katika jumuiya ya Bahá’í . Ndani ya Tanzania, Wa- Baha‘u’llah wanapatikana katika kila mkoa.

Wa-Bahá’í wa Dar es Salaam watasherehekea katika jumuiya zao na sherehe ya kilele itafanyika Jumanne ya Oktoba 29, 2019 kuanzia saa 7:00 mchana hadi saa 9:00 alasiri katika Kituo cha Bahá’í, jirani na makao makuu ya SIDO, Mtaa wa Mfaume, Upanga Magharibi.

Kwa taarifa zaidi kuhusu Imani ya Bahá’í, unaweza kupekua katika tovuti ya www.bahai.org, au kuwasiliana na Baraza la Kiroho la Mahali la Wa-Bahá’í wa Dar es Salaam. Simu namba: +255 766 376 286 / +255 784 381565 au baruapepe: [email protected].

By Jamhuri