Mkutano wa mwaka huu wa Barrick Gold Mine uliofanyika Toronto, Canada, umeingia dosari ya maandamano.
Maandamano hayo yamefanywa na wanaharakati wanaopinga uporaji rasilimali, unaofanywa na kampuni hiyo katika mataifa kadhaa ikiwamo Tanzania.

Waandaaji wa mkutano huo uliofanyika Mei 3, mwaka huu, walimzuia mwanaharakati wa haki za binadamu na mwanasheria wa masuala ya maliasili, Amani Mhinda, kuingia ukumbini.

Mhinda pia ni Mkurugenzi wa asasi ya kijamii ya HAKIMADINI, inayoshughulika na haki za binadamu katika maeneo ya machimbo ya madini.

Mhinda alikuwa amedhamiria kueleza umuhimu wa kujenga uwezo kwa wachimbaji wadogo na jamii, zinazoishi katika maeneo ya machimbo ili ziweze kunufaika na rasilimali ya madini nchini Tanzania.

Uongozi wa Barrick Gold ulimzuia kabisa kuingia ukumbini.

Gazeti la The Canadian lilimnukuu Mhinda akieleza ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na Barrick katika migodi yake nchini Tanzania

“Tunataka kuona mauaji na uvunjwaji wa haki za binadamu unaohusishwa na kampuni za uchimbaji madini za Canada yanamalizwa. Niko hapa kuwakilisha Watanzania wengi walioathirika wa migodi ya Barrick, na Mama Otaigo, aliyefariki Aprili, mwaka huu, kwa kunywa maji yenye sumu yaliyopo karibu na Mgodi wa North Mara nchini Tanzania,” alinukuliwa akisema Mhinda.

Hatua ya Barrick Gold Mine kuwazuia wanaharakati wa Tanzania na kuwaruhusu wenzao wa Papua New Guinea na Chile iliwashitua wengi.

Mhinda alishutumu hatua iliyochukuliwa na Barrick Gold ya kumzuia kuingia katika mkutano huo, akisema ni juhudi za kampuni hiyo za kuficha uvunjwaji wa haki za binadamu.

Mhinda na wenzake walipata fursa ya kuieleza hadhira kubwa iliyokuwa nje ya eneo la mkutano, juu ya unyanyasaji unaofanywa na Barrick nchini Tanzania.

Miongoni mwa wajumbe wa bodi ya kampuni hiyo ni Waziri Mkuu wa zamani wa Canada. Barrick hupata fedha za serikali na misaada ya kidiplomasia. Makao makuu yake yapo Toronto.

1214 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!